.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumamosi, 25 Novemba 2017

DR. NTUYABALIWE FOUNDATION YAKABIDHI CHUMBA CHA MAKTABA SHULE YA MSINGI MUUNGANO

Taasisi ya Dr Mtuyabaliwe imekabidhi Chumba cha maktaba, ilichokikarabati na kukisheheni vitabu, kwa shule ya Msingi Muungano iliyopo Manispaa Temeke, ambayo tangu kuanzishwa kwake miaka 30 iliyopita haikuwahi kuwa na maktaba.

Akikabidhi Maktaba hiyo Mkurugenzi na Muasisi wa Taasisi ya Dr Ntuyabakiwe Jacquiline Mengi amesema Taasisi hiyo, iliyoanzishwa mwaka 2015 kumuenzi marehemu baba yake aliyekuwa mpenzi mkubwa wa kusoma vitabu, inahimiza usomaji wa vitabu kwa wanafunzi,ikiwa ni kuunga mkono jitihada za serikali za kutoa elimu bora nchini:

Katika salaamu zao za shukrani Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa Bw. Bakari Makele, Mwalimu Mkuu Esther Matowo na Dada mkuu Veronika Mruma wameshukuru kwa msaada huo na kuahidi kuitunza na kuitumia ipasavyo.

Wakati wa hafla hiyo Mwakilishi Taasisi ya Sema-Tanzania Itanisa Mbise alikabidhi kwa Dada Mkuu wa shule Veronica Mruma nakala 100 za jarida linalochapishwa na Taasisi hiyo kwa matumizi ya maktaba hiyo.

Makabidhiano ya Makataba hiyo kwa shule ya Msingi Muungano yamefanyika wakati ambao Wizara ya elimu imeingiza somo la Maktaba katika mtaala wa elimu baada ya kuona umuhimu wake katika kufanikisha utoaji wa elimu katika shule za msingi.

Dr Ntuyabaliwe Foundation ni taasisi pekee binafsi nchini inayojihusisha na utoaji wa misaada ya vitabu vya maktaba kwa shule za msingi nchini, na hadi sasa imekwishatoa misaada kama huo kwa shule mbili za msingi za jiji la Dar es Salaam.
Mgeni rasmi Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Temeke, Bakari Makele akizungumza wakati wa makabidhiano ya Makataba iliyokarabatiwa na kwa shule ya Msingi Muungano iliyopo Manispaa Temeke jijini Dar es Salaam yaliyofanyika leo
Mwalimu Mkuu ya Msingi ya Muungano, Esther Matowo akisoma risala kwa mgeni rasmiwakati wa zoezi la uzinduzi wa maktaba shuleni hapo leo. wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Dr. Ntuyabaliwe Foundation, Jacqueline Mengi na wapili kulia ni Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Temeke, Bakari Makele.
Mwakilishi Taasisi ya Sema-Tanzania Itanisa Mbise akizungumza wakti wa uzinduzi wa maktaba katika shule ya msingi ya Muungano pamoja na kumkabidhi Dada Mkuu wa shule Veronica Mruma nakala 100 za jarida linalochapishwa na Taasisi hiyo kwa matumizi ya maktaba hiyo.
Mkurugenzi wa Dr. Ntuyabaliwe Foundation, Jacqueline Mengi akisoma moja ya vitabu vya hadithi kwa baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Muungano waliowakilisha wenzao katika uzinduzi huo.

Dada mkuu wa Msingi ya Muungano, Veronika Mruma akisoma risala kwa mgeni rasmi wakati wa ufunzi wa maktaba iliyokarabatiwa na Dr. Ntuyabaliwe Foundation leo.
                                                                                      Wanafuzi wakifanza igizo

TAMWA WAANZA MAADHIMISHO YA SIKU 16 KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Bi. Edda Sanga akizungumza leo na wanahabari akutoa kauli ya maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa chama hicho. Kushoto ni Ofisa Habari wa TAMWA, Happines Bagambi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Bi. Edda Sanga akizungumza leo na wanahabari akutoa kauli ya maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa chama hicho. Kulia ni Afisa Mipango wa TAMWA, Strategic Manager.
Baadhi ya wanahabari na wasaidizi wa sheria ngazi za jamii wakifuatilia hotuba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Bi. Edda Sanga katika mkutano huo.

CHAMA cha Wanahabari Wanawake (TAMWA) kimebaini kuwa matukio ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa chama hicho, kwa kupaza sauti dhidi ya vitendo vya ubakaji kuwa bado ni changamoto, kwa kile kuendelea kushamiri ndani ya jamii.

Kwa mujibu wa taarifa ya TAMWA iliyotolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Bi. Edda Sanga amesema Kitengo cha Usuluhishi, CRC cha TAMWA kuanzia mwezi Januari hadi Agosti 2017 kimepokea kesi za ukatili wa kijinsia hasa ubakaji 57 tofauti na ilivyokuwa mwaka jana kwa kipindi hicho kupokewa kesi 9 tu.

Bi. Sanga alisema hali hiyo ya ongezeko inashamiriana na taarifa ya utendaji kazi ya Kituo cha One Stop Centre cha Hospitali ya Amana, Dar es Salaam ambapo imeonyesha kiwango cha matukio ya ubakaji kwa mwaka huu kiko juu kwa idadi ya watoto 141 waliochini ya miaka 18, huku watu wazima matukio kama hayo yakiwa ni 27 tu.

Alifafanua kuwa kuanzia Julai 2016 hadi Juni 2017 kituo hicho kilipokea jumla ya 420 huku matukio ya watoto yakifikia 316 sawa na asilimia 75 na watu wazima wakiwa 104 sawa na asilimia 25 ya ukatili wa kijinsia.

"...Taarifa hiyo imeonesha idadi ya waliolawitiwa na kuripoti katika kituo hicho ni 44 sawa na asilimia 10.47 kati ya hao watoto ni 39 ukilinganisha na watu wazima ambao ni 5 kwa mwaka. Hali hii ya ukatili iko juu sana kwani watoto waliofanyiwa vitendo hivi wana uwezekano mkubwa wa kufanyia wengine katika kipindi cha makuzi yao.

Hata hivyo Mkurugenzi huyo Mtendaji wa TAMWA, Bi. Sanga aliongeza kuwa jukumu la ulinzi na malezi bora kwa watoto ni la jamii nzima wakiwemo marafiki, wazazi, ndugu, walezi, majirani na viongozi wakishirikiana na Serikali kuboresha na kusimamia utekelezaji wa sera na kubadilisha sheria kandamizi ili wahusika wa ukatili huu hasa kwa watoto wa kike wawajibishwe kwa mujibu wa sheria.

Siku 16 ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia ni kampeni ya kimataifa inayoongozwa na kituo cha Kimataifa cha wanawake katika uongozi tangu mwaka 1991 kutokana na mauaji ya kinyama ya akinadada wa Mirabelle yaliyofanyika nchini Dominica 1960, Kauli mbiu ya mwaka huu ni 'Funguka! Ukatili dhidi ya wanawake na watoto haumuachi mtu salama. Chukua Hatua'

WAZIRI MKUU AKIWA KATIKA ZIARA YA KIKAZI .NAMTUMBO,TUNDURU MKOANI RUVUMA

Wananchi wa Wilaya ya Namtumbo wakimsikiliza kwa makini Waziri Mkuu. Kassim Majaliwa akihutubia Mkutano wa hadhara katika Uwanja wa michezo wa Rwinga uliopo Wilaya ya Namtumbo Mkoa wa Ruvuvuma jana Novemba 23/2017. PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ampa mwezi mmoja afisa Aridhi wa Wawilaya ya Namtumbo Bwana Maurus Year kuhakikisha ametatua tatizo la Ardhi lilio dumu miaka kumi katika Wilaya ya Namtumbo.Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana Novemba 23/2017 katika mkutano wa hadhara Wilayani Namtumbo Mkoa wa Ruvuma. PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
Waziri Mkuu. Kassim Majaliwa akiongea na Wananchi wa kijiji cha Chomolo Wilaya ya Namtumbo wakati walipo simamisha msafara wake leo Novemba 24/2017 wakati alipo kuwa akielekea katika ziara ya kikazi katika wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma. PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU

Ijumaa, 24 Novemba 2017

TUTAMALIZA KERO YA MAJI TUNDURU-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa miradi miwili ya maji katika vijiji viwili vya Rahaleo na Mbungulaji kwenye kata ya Kalulu yenye thamani ya sh. Milioni 112 na kuahidi kumaliza kero ya maji wilayani Tunduru.

Amesema Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, hivyo amewaomba wananchi kuendelea kuwa na imani na Serikali yao.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Novemba 24, 2017) mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa miradi ya maji katika vijiji hivyo kwa lengo la kumaliza changamoto ya umatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo hayo.

Amesema ujenzi wa miradi hiyo ni utekelezaji wa Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani yenye lengo la kuwafikishia wananchi huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.

“Nataka maji haya yaende kwa wananchi si wananchi wayafuate, hivyo mara baada ya kukamilika ujenzi wa mradi huu Halmashauri ijenge mtandao wa mabomba yatakayosafirisha maji kutoka eneo la mradi hadi kwenye vioksi na kuyafikisha katika makazi ya wananchi.”

Pia ametoa wito kwa wazee wa vijiji hivyo kwa kushirikiana na vijana kuhakikisha wanalinda mradi huo kwa kutokata miti kwenye maeneo yote yanayozunguka vyanzo vya maji ili kuepusha ukame. Ameagiza ipandwe miti kwenye maeneo hayo ili kuhifadhi mazingira.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma kuhakikisha wanatekeleza ipasavyo majukumu yao ikiwa ni pamoja na kufanya kazi ya kuwatumikia wasnanchi bila ya ubaguzi wa dini, rangi na itikadi za vyama.

Amesema Serikali haitaki kusikia mwananchi anakwenda kufuata huduma katika ofisi zao na kuzungushwa kwa muda mrefu bila ya kuhudumiwa. “Serikali hii haitaki wananchi wake hususan wanyonge wasumbuliwe tukikubaini tunakuondoa.”

Waziri Mkuu ameongeza kwamba “Serikali hii haidekezi wala kuwaonea aibu watumishi wasiowajibika katika kuwatumikia wananchi. Serikali hii haitamuhifadhi mtu atakayeshindwa kufanya kazi, tunataka kazi tu na asiyefanya kazi na asile ndiyo maana tunawaondo watumishi wazembe wote.”

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, NOVEMBA 24, 2017.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO MHE MWANJELWA AFANYA MKUTANO NA WAHARIRI ILI KUONGEZA UELEWA WA MIFUMO MIPYA KUHUSU UAGIZAJI WA MBOLEA KWA PAMOJA

Na Mathias Canal, Dar es salaam

Wanahabari kote nchini wametakiwa kutoa ushirikiano kwa Wizara ya Kilimo ili ifanikiwe katika jitihada zake za kuhakikisha kwamba Tanzania inafikia lengo la Azimio la Maputo la kumwezesha mkulima kufikia matumizi ya kilo 50 za virutubisho kwa hekta badala ya hali ya sasa ambapo anatumia kilo 19 tu au asilimia 38 ya lengo la Maputo.

Mwito huo umetolewa Leo Novemba 24, 2017 na Naibu waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa wakati akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini kwenye Mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Jijini Dar es salaam.

Mkutano huo ulikuwa na dhamira ya kujifunza na kuongeza uelewa kwa wahariri juu ya Mifumo mipya iliyoanzishwa na Serikali kuhusu Uagizaji wa Mbolea kwa Pamoja (Bulk Procurement System - BPS) na Usimamizi wa bei Elekezi ya Mbolea (Indicative Pricing Structure - IPS) kwa lengo la kumwezesha Mkulima kupata mbolea bora na kwa bei nafuu ili kuongeza matumizi ya mbolea yatakayo chochea, ongezeko la uzalishaji nchini ili kukidhi mahitaji ya familia na kuuza ziada ndani na nje ya nchi.

Mhe Mwanjelwa alisema Wizara ya Kilimo imebaini kuwa wafanyabiashara wadogo wa mbolea wanaokiuka bei elekezi kutokana na wafanyabiashara wakubwa kuwauzia wafanyabiashara hao wadogo kwa bei elekezi ya rejereja badala ya bei ya jumla licha ya kufahamu kuwa wanatakiwa kugawana faida na wauzaji wa rejareja lakini bado wanakiuka taratibu za kisheria hivyo aliwasihi kuacha tabia hiyo ili mawakala wauze kwa rejareja na kwa bei elekezi bila kuathiri biashara zao.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ina Mkakati wa kuongeza matumizi ya mbolea ambao umekuwa na umuhimu wa pekee hasa ikizingatiwa kwamba imeweka lengo la kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati unaoendeshwa kwa viwanda.

Alisema Kwa sehemu kubwa, viwanda hivyo vitategemea malighafi itokanayo na mazao ya kilimo. Hivyo ili, kufikia lengo hilo, lazima kila mmoja kutumia nafasi yake kuhakikisha kwamba tija itokanayo na Kilimo inaongezeka kwani Mbolea ni moja ya vichocheo vikubwa.

“Pamekuwepo na Mifumo mbalimbali iliyoanzishwa kwa lengo la kumsaidia Mkulima kupata mbolea za kutosha ili aongeze tija na uzalishaji katika kilimo ambayo ni pamoja na ruzuku ya usafirishaji ili kuwezesha mbolea kuuzwa kwa bei moja nchi nzima (Pan Territorial Prices). 

Baadae ulifuata Mfumo wa wauzaji kulipwa sehemu ya bei na hivyo mbolea kuuzwa kwa bei chini kuliko bei ya Soko. Sambamba na Mfumo huo, kulikuwa na jitihada za kutengeneza mbolea hapa nchini ili kuepuka gharama kubwa za uagizaji” Alikaririwa Mhe Mwanjelwa

Alisema taarifa zinabainisha kuwa Mikoa ya Ruvuma, Lindi, Mtwara, Mwanza na Geita wafanyabiashara hufungua mifuko na kuuza mbolea ya kupandia (DAP) kwa Tshs 2,000/= kwa kilo ili wapate Tshs 100,000/= kwa mfuko wa kilo 50 badala ya bei elekezi ya Tshs 51,000 – 56,000/=.

Aidha, Mbolea ya kukuzia (Urea) wanaiuza kwa Tshs 1,500/= kwa kilo ili wapate Tshs 75,000/= kwa mfuko wa kilo 50 badala ya bei elekezi ya Tshs 41,000 – 45,000/=. Pamoja na kuwauzia wakulima mbolea iliyopoteza ubora kwa kufunguliwa na kuachwa wazi, wafanyabiashara hawa wanawaingizia wakulima hasara kubwa ya mavuno.

Naibu Waziri Mhe Mwanjelwa alisisitiza, “Ofisi yangu ina taarifa kwamba baadhi ya wafanyabiashara wanatunza mbolea bila kuzingatia viwango vilivyowekwa na TFRA. Haya ni makosa mabubwa sana kisheria kwani yanasababisha mbolea kumfikia mkulima ikiwa imepungua ubora au kuharibika kabisa na hivyo kumfanya mkulima asipate tija inayotokana na matumizi ya mbolea. Huu ni uhujumu mkubwa sana wa uchumi wa Mkulima pamoja na Taifa kwa ujumla”

Mbolea ni kemikali ambayo virutubisho vyake huyeyukia hewani ikiachwa wazi kwa muda mrefu. Kwa maana nyingine, kitendo cha kufungua mfuko wa mbolea hufanya virutubisho (Nutrients) kuanza kupotea mara tu vinapokutana na hewa. 

Hivyo kinachobaki kwenye mfuko ni makapi yasiyo na manufaa katika kuongeza uzalishaji wa mazao. Aidha, mbolea ya kupima inaweza ikageuka sumu kwa mimea na hata udongo na hivyo kufanya usifae tena kwa matumizi ya kilimo.
Mkutano huo wa Naibu Waziri wa Kilimo na wahariri wa vyombo vya habari nchini ni mwanzo wa mahusiano chanya baina ya Waandishi wa habari na Wizara ya kilimo ili kuinua sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kuunga mkono kwa vitendo juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli katika kuimarisha uuchumi wa Wananchi kupitia kilimo ambao ni uti wa mgongo.
Mgeni Rasmi-Naibu waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini kwenye Mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Jijini Dar es salaam, Leo Novemba 24, 2017.
Mgeni Rasmi-Naibu waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini kwenye Mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Jijini Dar es salaam, Leo Novemba 24, 2017.
  Baadhi ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini wakimsikiliza kwa makini Mgeni Rasmi-Naibu waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa wakati akizungumza kwenye Mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Jijini Dar es salaam, Leo Novemba 24, 2017.
  Baadhi ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini wakimsikiliza kwa makini Mgeni Rasmi-Naibu waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa wakati akizungumza kwenye Mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Jijini Dar es salaam, Leo Novemba 24, 2017.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI TOKA TASWA

KAMATI ya Utendaji ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), iliyokutana Dar es Salaam hivi karibuni, imeteua wanahabari tisa kuunda Kamati ya Marekebisho ya Katiba ya chama. 

Wengi wa walioteuliwa ni wanachama wa TASWA na wengine ni viongozi wa zamani wa chama na pia baadhi ni wanahabari wa michezo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo atakuwa ni Mwenyekiti wa zamani wa TASWA, Boniface Wambura ambaye licha ya kuwa mwanahabari pia ana taaluma ya sheria na kwa sasa ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB) na Katibu wa Kamati atakuwa Wakili Emmanuel Muga.

Wajumbe ni Katibu Mkuu wa zamani wa TASWA, Abdul Mohammed wa gazeti la Mwananchi, Mhazini Msaidizi wa zamani wa TASWA ambaye kwa sasa ni Mhariri wa michezo wa gazeti la Daily News, Nasongelya Kilyinga.

Wajumbe wengine ni Florian Kaijage kutoka Azam Media, Mahmoud Zubeyri kutoka Bin Zubeiyr Blogs, Tunu Hassan wa EFM Redio, Benny Kisaka wa Jambo Concept na Majuto Omary wa gazeti la Citizen.

Hatua ya kuunda kamati hiyo inatokana na maelekezo kutoka Baraza la Michezo la Taifa (BMT), ambalo limetaka chama kifanye marekebisho ya katiba kwanza ili iwe rahisi kwa mambo mengine yafanyike katika utaratibu mzuri ikiwa ni pamoja na Uchaguzi Mkuu wa chama.

Kutokana na hali hiyo, Kamati ya Utendaji imekabidhi jukumu hilo kwa Kamati Maalum ambayo itapanga utaratibu wake wa namna ya kufanyia marekebisho katiba hiyo, ikimaliza itawasilisha rasimu ya Katiba kwenye Mkutano Mkuu wa chama kwa hatua nyingine.

Ni imani ya Kamati ya Utendaji kwamba Kamati ya Katiba inaweza kukamilisha rasimu hiyo katika muda usiozidi siku 90, ikiwa chini ya hapo itakuwa vizuri zaidi.

Tunaomba wadau wote tuipe ushirikiano wa namna mbalimbali kwa kadri itakavyowezekana ili tupige hatua katika kuimarisha chama chetu.

Nawasilisha,

Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
24/11/2017

HAYA NDIYO MAAJABU YA KIMONDO CHA MBOZI KILICHOPO MKOANI SONGWE, NAIBU WAZIRI WA MALIASILI AELEZA MIPANGO YA SERIKALI YA KUKIENDELEZA

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (wa pili kulia) akiwa ameshikilia kivutio cha utalii cha Kimondo leo wakati wa ziara yake ya kikazi katika kijiji cha Ndolezi wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe.

Kimondo hicho kinachokadiriwa kuwa na tani 12 kiligunduliwa wilayani Mbozi mwaka 1930 na kimeundwa kwa madini ya Chuma 90%, Nickel 8.69%, Copper 0.66%, Sulphur 0.01% na Phosphorus 0.11.

Aidha, kimondo hiki ni cha pili kwa ukubwa kati ya 35 vilivyopo barani Afrika na cha nane kati ya 578 vilivyopo duniani kote ambavyo vimeundwa kwa chuma. Sifa kuu ya kimondo hiki ni kuwa na ubaridi wakati wote hata mchana wa jua kali.

Pamoja na mambo mengine katika ziara hiyo, amekagua ujenzi unaoendelea wa jengo la kituo cha taarifa (Information Centre) katika kivutio hicho ambalo linagharimu Shilingi milioni 400.

Alisema Serikali kupitia wizara yake ina mpango thabiti wa kuendeleza kivutio hicho pamoja na vivutio vya ukanda wa kusini ambapo kupitia Benki ya Dunia imepata mkopo nafuu wa Dola za Kimarekani milioni 150 sawa na shilingi bilioni 340 kwa ajili ya kuendeleza vivutio vya ukanda wa kusini ikiwemo kuimarisha miundombinu.

Vivutio vingine vya utalii vilivyopo Mkoani Songwe ni pamoja na chemchem ya maji moto, vitalu vya uwindaji vyenye wanyamapori mbalimbali, mifupa ya shingopana songwensis, unyayo wa mtu wa kale, mapango ya popo, maporomoko ya maji, mbega weupe, kituo cha kwanza cha polisi Tanzania, mabaki ya nyumba za kufua chuma, na ziwa Rukwa.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akisikiliza maelezo kutoka kwa Muhifadhi wa Mambo ya Kale, Winnie Msacky kuhusu kivutio cha utalii cha Kimondo wakati wa ziara yake ya kikazi katika kijiji cha Ndolezi wilaya ya Mbozi Mkoani wa Songwe jana.
Jengo la kituo cha taarifa katika eneo la kivutio hicho (Information Center) ambacho ujenzi wake unaendelea. Ujenzi wa kituo hiki unagharimu Shilingi Milioni 400.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akizungumza na baadhi ya watumishi wa kituo hicho na wananchi wa vijiji jirani.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga akizungumza na watumishi pamoja na wananchi hao.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akipata maelezo kutoka Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Kale, Bi. Digna Tilya kuhusu jengo la kituo hicho cha taarifa katika kivutio hicho. (Picha na Hamza Temba-Wizara ya Maliasili na Utalii)

ROBINHO AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA TISA JELA KWA UBAKAJI

Mchezaji soka wa Brazil Robinho amehukumiwa kifungo cha miaka tisa jela kwa kuhusika katika tukio la ubakaji lililohusisha kundi la wanaume huko Milan nchini Italia mnamo mwaka 2013.

Mahakama ya nchini Italia imetoa huku kwa mchezaji huyo mwenye miaka 33 na wenzake watano raia wa Brazil kwa kumbaka mwanamke raia wa Albainia aliyekuwa na miaka 22 wakati huo baada ya kumlewesha kwenye klabu ya usiku.

Mshambuliaji huyo aliondoka AC Milan mwaka 2015 baada ya kuitumikia kwa miaka mitano na wakati hukumu hiyo ikitolewa hakuwepo Mahakamani na alikanusha shtaka hilo kupitia kwa wakili wake.

Hata hivyo Robinho hataanza kutumikia kifungo hicho kwanza hadi hapo rufaa yake ya hukumu hiyo itakaposikilizwa.

KOCHA ARSENE WENGER AMESEMA ARSENAL INAKAZI YA KUFANYA

Kocha Arsene Wenger amesema Arsenal inakazi ya kufanya ili iweze kusonga mbele katika hatua ya mtoano ya Ligi ya Europa baada ya jana kufungwa goli 1-0 na FC Cologne.

Mkwaju wa penati uliopigwa na Sehrou Guirassy baada ya Mathieu Debuchy kuonekana amemchezea rafu mshambuliaji huyo wa Ufaransa lilitosha kuwapa ushindi Cologne.

Ukiwa umebakia mchezo mmoja, Arsenal inapointi 10 katika michezo mitano, pointi nne mbele ya Cologne na Red Star Belgrade iliyotoa sare na Bate Borisov.
                          Sehrou Guirassy akiwa amefunga goli pekee lililoizamisha Arsenal
                    Mabeki wa FC Cologne wakimdhibiti Danny Welbeck asilete madhara

TIMU YA EVERTON YAPIGWA MKONO NYUMBANI NA ATALANTA

Timu ya Everton imepigwa magoli 5-1 na Atalanta katika Ligi ya Europa katika mchezo ulioshuhudiwa na mashabiki karibu na nusu ya watazamaji katika dimba la nyumbani la Goodison Park.

Everton walikuwa tayari wameshatolewa katika michuano hiyo kabla ya mchezo huo hata hivyo kocha aliyeitwaa timu hiyo David Unsworth alipanga kikosi kigumu wakiwemo Wayne Rooney, Kevin Mirallas naAshley Williams.

Wageni walipata goli la kwanza katika dakika ya 12 kupitia kwa Bryan Cristante na kisha baadaye kuongeza la pili kabla ya Sandro Ramirez kuifungia Everton goli pekee. Robin Gosens aliifungia Atalanta goli la tatu na Andreas Cornelius akatupia mawili.
                         Mchezaji Bryan Cristante akifungua akaunti ya magoli ya Atalanta
                                    Mshambuliaji Robin Gosens akiifungia Atalanta goli la tatu

KONGAMANO LA WASOMI WANATAALUMA KUFANYIKA KESHO HOTELI YA LANDMARK UBUNGO JIJINI DAR ES SALAAM

Mratibu wa Kongamamo la Wasomi Wanataaluma wa Kikristo liitwalo Tanzania for Jesus Prayer Movement ambalo mlezi wake ni Huduma ya I Go Africa for Jesus, Ephrahim Mwambapa akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Kanisa la Abundant Bressing Center (ABC), Tabata Matumbi jijini Dar es Salaam, kuhusu kongamano hilo litakalofanyika Hoteli ya Landmark siku ya Jumamosi. Kulia ni Katibu Mkuu  wa Kongamano hilo, Lendian Bigoli.

                                                                                         Na Dotto Mwaibale

WANAFUNZI waliohitimu vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini kesho wanatarajia kufanya kongamono kubwa la kihistoria kujadili namna watakavyoweza kutumia taaluma zao kusaidia jamii, kanisa na taifa kwa ujumla.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mratibu wa Kongamamo hilo, Ephrahim Mwambapa alisema kongamanao hilo linaundwa na muungano wa wasomi wa kristo uitwao Tanzania for Jesus Prayer Movement ambao mlezi wake ni Huduma ya I Go Africa for Jesus.

Alisema licha ya muungano huo kuundwa na vijana wa kikristo lakini vijana wote wasomi kutoka katika vyuo na shule za sekondari na madhehebu mbalimbali wanaalikwa ili kuchangia mada zitakazo jadiliwa na mgeni rasmi atakuwa ni Kiongzi Mkuu wa Kanisa la Abundant Bressing Center nchini, Askofu Flaston Ndabila.

Mwambapa alisema kuwa katika kongamano hilo kutakuwepo na mada mbalimbali na kuona ni jinsi gani kila mmoja na taaluma yake ataweza kusaidia jamii badala ya taaluma hiyo kuachwa bila ya kuifanyia kazi.

"Tunapokuwa vyuoni tunakuwa na mipango mingi ya maendeleo lakini baada ya kumaliza masomo kila mtu anakuwa kivyake wakati tunapaswa kushirikiana na jamii na ndio maana tumeona ni vizurio kuazisha muungano huu lengo likiwa kujumuika na jamii katika shughuli za maendeleo ya nchi na dini" alisema Mwambapa.

Alisema wazo la kuanzisha muungano huo nimatunda ya mkutano ya mkutano mkuu wa kitaifa wa kuliombea taifa ulioratibiwa na Askofu Flaston Ndabila na kuhudhuriwa na watu mbalimbali na vijana kutoka vyuo vikuu uliofanyika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Mwambapa alisema kongamano hilo litahudhuriwa na wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali,sekondari baadhi wa viongozi.

(Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com-simu namba 0712727062)

WAZIRI MKUU AMPA OFISA ARDHI MWEZI MMOJA KUFIDIA WANANCHI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amempa mwezi mmoja Ofisa Ardhi wa wilaya ya Namtumbo Bw. Maurus Yera awe ametafuta ardhi ya kuwafidia wakazi wa kijiji cha Lwinga wilayani Namtumbo.

Wakazi hao 21 mwaka 2008 eneo lao lenye ukubwa wa ekari 101 lilitwaliwa na Serikali kupitia halmashauri ya wilaya hiyo kwa ajili ya kupisha ujenzi wa shule ya sekondari ya mkoa wa Ruvuma na waliahidiwa kulipwa fidia.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana jioni (Alhamisi, Novemba 23, 2017) alipozungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Lwinga akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma.

Alitoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi hao kupitia mabango, ambapo walimuomba awatatulie kero hiyo ya madai ya fidia ya ardhi iliyodumu kwa miaka 10 bila kupatiwa ufumbuzi.

Waziri Mkuu alisema haoni sababu ya Halmashauri hiyo kushindwa kuwafidia wananchi hao sehemu ya ardhi kwa muda wote huo ukizingatia wilaya hiyo ina hifadhi ya ardhi.

“Nataka wananchi hawa wawe wamelipwa fidia yao ya ardhi kabla ya siku kuu ya Krismasi ya mwaka huu. Serikali haiko tayari kuona wananchi wake waliotoa ardhi kupisha maendeleo wakisumbuliwa.”

Waziri Mkuu alisema Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli inataka kila mtumishi ahakikishe anatumia taaluma yake vizuri kwa kuwahudumia wananchi ikiwa ni pamoja na kutatua kero zinazowakabili kwa wakati.

Pia Waziri Mkuu alitoa wito kwa wananchi hao kuhakikisha hawakubali kutoa rushwa pale wanapohitaji kupata huduma mbalimbali kutoka kwa watumishi kwa kuwa ni haki yao kuhudumiwa.

Aliwataka wananchi kuwa na imani na Serikali yao na kuiunga mkono katika mapambano dhidi ya rushwa kwani vitendo hivyo vinakwamisha shughuli za maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka watendaji kuhakikisha miradi wanayosimamia inakuwa na thamani inayolingana na kiasi cha fedha kilichotolewa na iwapo watabainika kwenda kinyume hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

“Lazima kiasi cha fedha kinachotolewa kugharamia mradhi kilingane na thamani ya mradi husika. Mfano tumetoa sh. milioni 70 kugharamia mradi na kukuta mradi uliojendwa ni wa sh. milioni 30 aliyeshughulikia ujenzi huo nasi tutamshughulikia hatutamuacha salama.”

Awali, Waziri Mkuu alifungua ghala la kuhifadhiia mpunga na mchele katika wilaya ya Namtumbo lililojengwa na MIVARF na kisha alizungumza na watumishi wa halmashauri hiyo na kuwataka wafanye kazi kwa bidii na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Bibi Christine Mndeme alisema mkoa huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa masoko kwa mazao ya mahindi na mbaazi, ambapo Waziri Waziri Mkuu alisema sula hilo linashughulikiwa hivyo wananchi waendelee kuwa na subira.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, NOVEMBA 24, 2017.

SERIKALI KUWAPATIA MATIBABU BURE WAZEE WA WILAYA YA HANDENI

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe amewahamasisha wazee kuanzia umri wa miaka 60 na kuendelea kujitokeza kwenye zoezi la upigwaji picha ili waweze kupatiwa kadi za bima ya afya zitakazowawezesha kupatiwa matibabu bure kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali.

Hayo ameyazungumza mara baada kuwasili katika Ofisi za Mtendaji Kata ya Kabuku Nov 23, 2017 kuhamasisha huduma za afya.

Hatua hiyo ni muendelezo wa agizo la serikali ya awamu ya tano ya rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuhakikisha wazee kuanzia umri wa miaka 60 na kuendelea wanapatiwa matibabu bure. PICHA/HABARI NA KAJUNASON/MMG -KABUKU, HANDENI.
                                                                          Wazee wakisikiliza kwa makini. Diwani wa Kata ya Kabuku, Amina Mnegelo akizungumza machache mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe huku wazee wakimfuatilia kwa makini.

RAIS DKT. MAGUFULI AMTEUA DKT. SLAA KUWA BALOZI


MBUNGE WA SONGEA MJINI, MH. LEONIDAS GAMA AFARIKI DUNIA

Mbunge wa Songea Mjini mkoani Ruvuma Mh. Leonidas Gama amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya Peramiho mjini Songea. 

Taarifa za awali zinasema Mh. Gama alijisikia vibaya akiwa nyumbani kwake na kukimbizwa hospitali ya Peramiho ambako mauti yalimkuta majira ya saa sita usiku wa kuamkia leo. Tutaweletea taarifa zaidi hapo baadaye

CHUO KIKUU ARDHI MARUFUKU KUKODI MAKAMPUNI-MAJALIWA

Waziri Mkuu. Kassim Maliwa,(kulia) akisalimiana na Waziri Mkuu Mstaafu na Mkuu wa Chuo Kikuu Aridhi Tanzania. David Cleopa Msuya .wakati wa uzinduzi wa Sherehe ya miaka Kumi ya Chuo Kikuu cha Ardhi ambayo yameanza leo Novemba 23/2017 Jijini Dar es salaam.katikati ni Rais wa Jumuia ya wahitimu Chuo Kikuu cha Aridhi. PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (katikati )akimuelekeza jambo Makamu Mkuu wa Chuo cha Ardhi (kushoto)Profesa Evaristo Liwa .kulia kwa Waziri Mkuu, ni Waziri wa Elimu,Sayansi,Teknolojia,na Ufundi. Profesa Joyce Ndalichako
Waziri Mkuu leo Novemba 23 /2017 alikuwa mgeni Rasimi katika Sherehe za Miaka 10 ya Chuo cha Aridhi Dar es salaam. PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU

Alhamisi, 23 Novemba 2017

KOZI YA GRASSROOTS YAPELEKWA MBEYA

Kozi ya Grassroots kwa Vijana kuanzia miaka 6-12, itafanyika mkoani Mbeya kuanzia Novemba 27, 2017 mpaka Desemba 1, mwaka huu.

Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Salum Madadi amesema kozi hiyo itahusisha walimu wa Shule za Msingi za mikoa ya Songwe, Katavi, Rukwa na wenyeji Mbeya.

Jumla ya washiriki 30 watahudhuria kozi hiyo ambapo kila mkoa utatoa washiriki saba (7) isipokuwa wenyeji Mbeya ambao watatoa washiriki tisa (9).

Kozi hiyo imezingatia jenda kwa kila mkoa unatakiwa kutoa idadi sawa au Wanawake wawe wengi zaidi ya Wanaume ili kutoa hamasa zaidi kwa Wanawake kujifunza.

Kozi hiyo ya Grassroots itakwenda sambamba na Kampeni ya ‘Live Your Goal’ ikiwa na maana ya ‘Ishi ndoto zako’ itayofanyika Novemba 29, 2017 ikiwa na lengo la kutoa hamasa kwa soka la Wanawake.

Kampeni hiyo ya Live Your Goal inalenga kutoa hamasa kwa wadau waujue, waupende na kuheshimu soka la Wanawake kama ilivyo kwa upande wa Wanaume ambapo kampeni hiyo itaambatana na shughuli mbalimbali za soka kuanzia asubuhi na itamalizika kwa kuchezwa mchezo mmoja Uwanja wa Sokoine siku hiyo jioni baina ya timu za Wanawake za Mkoa wa Mbeya.

Mwenyekiti wa Soka la Wanawake Tanzania (TWFA), Amina Karuma akizungumzia kozi hiyo kwenda kufanyika Mbeya, amesema: “Tumetoka Lindi na sasa tunakwenda Mbeya, mpango huu utasaidia kuwajengea vijana wetu kujiamini hasa Wanawake.”

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Mbeya (MREFA), Elias Mwanjala amewakaribisha washiriki watakaohudhuria kozi hiyo mkoani Mbeya akisema Mkoa huo upo tayari nkupokea ugeni huo kwa maendeleo ya mpira wa miguu.

Mpango wa Grass roots kabla ya kwenda kufanyika Mbeya ulifanyika huko Mkoani Lindi.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

CHUO KIKUU ARDHI MARUFUKU KUKODI MAKAMPUNI-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekipiga marufuku Chuo Kikuu Ardhi kukodi makampuni ya kufanya kazi mbalimbali kwa niaba yake.

Amesema kitendo hicho kinaharibu kazi na sifa ya chuo hicho kwa kuwa baadhi ya makampuni wanayoyapa kazi hayakidhi vigezo.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Novemba 23, 2017) kwenye ufunguzi wa sherehe za maadhimisho ya miaka 10 ya Chuo Kikuu Ardhi.

“Kama kuna umuhimu wa kufanya kazi na kampuni ni bora muanzishe kampuni ya kwenu itakayofanya kazi vizuri ili kujiepusha na matatizo.”

Pia Waziri Mkuu amekiagiza chuo hicho kufanya tafiti zenye kuleta majibu ya maswali na changamoto mbalimbali zinazolikabili Taifa na Dunia.

Ametaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni mabadiliko ya tabia nchi, ujenzi holela, uharibifu wa mazingira na majanga ya asili kama mafuriko.

Amesema Serikali inaamini kuwa matokeo ya kazi zinazofanywa na chuo hicho zikiwemo tafiti ni chachu ya maendeleo ya taasisi za elimu ya juu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Dira ya Maendeleo ya Taifa imeweka mkazo wa kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa kupato cha kati ifikapo 2025, hivyo wanahitajika wataalamu wa kutosha na wenye weledi.

“Hivyo Chuo Kikuu cha Ardhi kama taasisi ya Serikali inawajibu mkubwa wa kutayarisha wataalamu mbalimbali wa sekta za ujenzi, ukadiriaji majenzi na uhandisi wa mazingira.

Pia Waziri Mkuu amewataka watumie fursa hiyo ya kuadhimisha miaka 10 ya chuo hicho kujitafakari na kuona ni kwa namna gani wanaweza kuwekeza zaidi ili kuongeza tija ya uwepo wa taasisi hiyo kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

“Wekeni mikakati madhibuti itakayowezesha chuo kupiga hatua kubwa zaidi katika kipindi cha miaka 10 ijayo. Siku zote mjikite katika kutafuta kuwa na ubora zaidi ya wakati uliopita.”

Awali, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema Serikali inakkitegemea chuo hicho katika kufanikisha ajenda yake ya uchumi wa viwanda kwa kuwa kinatoa wataalamu wengi.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na Mkuu wa chuo hicho ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa David Msuya, Mwenyekiti wa Baraza la chuo Bibi Tabitha Siwale, Makamu Mkuu wa chuo Profesa Evaristo Liwa pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, wanafunzi na watumishi wa chuo hicho.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, NOVEMBA 23, 2017.

WAZIRI HARRISON MWAKYEMBE AZINDUA MICHUANO YA SHIMUTA IRINGA

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe akiwa pamoja na mkuu wa mkoa wa Iringa bi Amina Masenza jukwaa kuu akiwahutubia wanamichezo waliojitokeza kushiriki michuano ya SHIMUTA

Baadhi ya wanamichezo walikuwa wakifurahia jambo baada ya waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe kuzindua rasmi mashindano hayo

Michuano ya SHIMUTA inayohusisha wafanyakazi wa mashirika ya umma, kampuni za watu binafsi na taasisi zilizopo hapa nchini imezinduliwa rasmi mkoani Iringa huku washiriki wakiwataka waajiri kuwaruhusu wafanyakazi kushiriki katika michezo huku waziri mwenye dhamana ya michezo akitoa onyo kwa mamluki.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amezionya timu ambazo zinashiriki kwenye michuano ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma na Kampuni Binafsi Nchini (SHIMUTA) kuacha kuchukua wachezaji ambao sio wafanyakazi kwani kufanya hivyo kunapunguza ladha ya mashindano hayo.

Mwakyembe alisema kuwa michezo hujenga undugu na furaha baina ya wanamichezo hivyo kuwaingiza wachezaji ambao sio wafanyakazi kwenye mashindano hayo wataondoa maana halisi ya mashindano hayo jambo ambalo linaweza kuwafanya kushindwa kufikia malengo yao waliojiwekea.

“Mashindano haya ni ya wanamichezo wafanyakazi…kuna wale wanamichezo ambao sio wafanyakazi ambao wanajulikana kama mamluki au wavamizi kwamba hapa sio mahala pao nawasihi tuchezeshe wafanyakazi halisi ili mshindi apatikane kihalali na sio vyenginevyo….. kwa sababu ni hatari sana kumleta mwanamichezo ambaye sio mfanyakazi kwenye michezo hii anaweza kuvunjika mguu au akifa kwa mfano hatuombei itokee hiyo itakuwaje “Alisema Mwakyembe

Aidha Mwakyembe alizitaka timu hizo kuacha kuwatumia wachezaji wa aina hiyo kwani wana madhara makubwa hasa pale yanapokuwa yakijitokeza kwa kuzitaka timu zenye utamaduni huo kuhakikisha wanaondokana nao.
Hata hivyo waziri Mwakyembe alionekana kukerekwa na baadhi ya menejimenti za Taasisi,Mashirika na makampuni mbalimbali kuwa na utashi wa kutokupenda michezo na wengine kwa kisingizio cha ukosefu wa fedha kuacha kufanya hivyo badala yake wamuunge mkono Rais Jakaya Kikwete katika jitihada zake za kuinua na kuendeleza michezo hapa nchini.

Akizungumzia waamuzi wanaochezesha mashindano hayo, Mwakyembe aliwataka kuchezesha kwa haki bila upendeleo kwa kufuata sheria za mchezo husika ili mshindi aweze kupatikana kihalali kwa sababu wakienda kunyume chake wanaweza kusababisha tafrani na manung’uniko kwa baadhi ya timu shiriki.

Hali kadhalika aliwataka kuhakikisha wanakuwa na nidhamu ya hali ya juu wakati wote wa mashindano ikiwemo kukubaliana na matokeo pindi watakapojikuta wamefungwa wakati wa mashindano hayo.
Naye Mwenyekiti wa Shimuta, Khamis Mkanachi alisema kuwa kupungua kwa idadi ya timu shiriki kunatokana na baadhi ya mashirika kubinafsishwa hali ambayo imepelekea timu nyingi kushindwa kupata nafasi ya kupeleka washiriki wake lakini pamoja na kuwepo hali hiyo shirikisho hilo limendelea na jitihada za ziada kuhakikisha idadi ya timu hizo haipungui bali kuongezeka.

Nao baadhi ya washiriki wameeleza sababu ya baadhi ya waajiri wasio na mapenzi na michezo kushindwa kutoa hamasa sehemu za kazi kwa kutokujua faida zitokanazo na michezo.

Ni wajibu wa viongozi kuinua na kuendeleza michezo mahala pa kazi “ni kauli mbiu yenye lengo la kuhamasisha ushiriki wa michezo kwa watumishi kwa lengo la kukutanisha wafanyakazi wa idara tofauti na kubadilishana uzoefu wa kikazi lakini kubwa zaidi ni kujenga afya kwa kupitia michezo.

SHIMUTA ni Shirikisho la Michezo la mashirika ya Umma Taasisi, na kampuni binafsi hapa nchini, lililoanzishwa na serikali ili kuhimiza michezo mahala pa kazi.

TAARIFA KUTOKA KAMATI YA BODI YA LIGI KUU TANZANIA BARA

KAMATI ya Bodi ya Ligi Kuu ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi katika kikao chake cha Novemba 22, 2017 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi kwa msimu wa 2017/2018 inayoendelea hivi sasa.

Klabu ya Tanzania Prisons imepewa Onyo Kali kwa kuwakilishwa kwenye benchi na ofisa tofauti na yule aliyeudhuria kikao cha maandalizi (pre match meeting) cha mchezo kati yake na Kagera Sugar uliofanyika Novemba 4, 2017 kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Katika kikao hicho, Prisons iliwakilishwa na Meneja wake Erasto J. Ntabah lakini kwenye benchi alikaa Hassan Mtege. Adhabu ya Onyo Kali kwa klabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Pia Erasto J. Ntabah amesimamishwa hadi suala lake la kutoka jukwaani na kwenda kumfokea Mwamuzi wa Akiba litakaposikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF. Amesimamishwa kwa mujibu wa Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu kuhusu Usimamizi wa Ligi.

Mchezaji Benjamin Asukile wa Tanzania Prisons amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu na Mwamuzi kwa kosa la kumpiga kiwiko kwenye paji la uso mchezaji wa Kagera Sugar.

Kocha wa Azam FC, Aristica Cioaba amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kuwafuata waamuzi na kuwalalamikia kwa kurusha mikono akionyesha kutoridhika na maamuzi yao. Alifanya hivyo kwenye mechi namba 69 ya Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya Ruvu Shooting iliyofanyika Novemba 4, 2017 kwenye Uwanja wa Azam Complex na adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 40(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Makocha.

Kwa upande wa Ligi Daraja la Kwanza, Klabu ya Mvuvumwa imepigwa faini ya sh. 100,000 (laki moja) kwa timu yake kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi dhidi ya African Lyon ikiwa na maofisa pungufu, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Kwanza. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Kwanza. Mechi hiyo ilifanyika Novemba 7, 2017 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Mtunza Vifaa wa timu ya JKT Mlale, Noel Murish amesimamishwa hadi suala lake la kuwamwagia maji washabiki wa Polisi Tanzania litakaposikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF. Uamuzi wa kumsimamisha ni kwa mujibu wa Kanuni ya 9(5) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Usimamizi wa Ligi. Alifanya kitendo hicho katika mechi hiyo iliyochezwa Novemba 4, 2017 kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.

Klabu ya Coastal Union imepewa Onyo Kali kutokana na timu yake kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi ikiwa na maofisa pungufu, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Kwanza. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Kwanza. Ilifanya hivyo katika mechi dhidi ya JKT Mlale iliyofanyika Novemba 12, 2017 katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Nayo Klabu ya JKT Mlale imepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa kutoingia vyumbani wakati wa mapumziko katika mechi hiyo. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Daraja la Kwanza.

JKT Mlale imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya KMC kumchezesha nahodha wake Stephano Mwasika katika mechi namba 28 iliyofanyika Oktoba 30, 2017 kwenye Uwanja wa Azam Complex wakati akiwa anatumikia adhabu ya kadi nyekundu.

Mwasika alitolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga kiwiko mpinzani wake kwenye mechi namba 15 kati ya KMC na Mbeya kwanza iliyochezwa Oktoba 5, 2017 katika Uwanja wa Azam Complex.

Baada ya kupata kadi hiyo, Mwasika alitakiwa kukosa mechi tatu na kulipa faini ya sh. 300,000 (laki tatu). Mechi alizotakiwa kukosa ni dhidi ya Mufindi United (Oktoba 15), Polisi Tanzania (Oktoba 23) na JKT Mlale (Oktoba 30). Alikosa mechi mbili tu za kwanza, lakini akacheza mechi ya tatu dhidi ya JKT Mlale iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Klabu ya Toto Africans imepewa Onyo Kali kutokana na timu yake kuchelewa kikao cha maandalizi (pre match meeting) katika mechi dhidi ya Biashara United Mara iliyofanyika Novemba 5, 2017 kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza. Adhabu hiyo ni utekelezaji wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.

Meneja wa Toto Africans, Yusufu Jumaa amefungiwa miezi miwili na kupigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) baada ya kuondolewa na Mwamuzi kwenye benchi la ufundi kwa kupinga maamuzi yake na kumshambulia kwa maneno.

Ofisa Habari wa Toto Africans, Cuthbert Japhet amesimamishwa hadi suala lake la kummwagia maji Mwamuzi na kumjeruhi kwa kitu chenye ncha kali wakati wa mapumziko katika mechi hiyo litakaposilikizwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF.

Waamuzi Wasaidizi Jumanne Njige wa Mwanza na Bam Bilasho wa Dodoma wamepewa Onyo Kali kwa kuchezesha chini ya kiwango mechi namba 36 ya Kundi C kati ya Transit Camp na Rhino Rangers iliyofanyika Novemba 11, 2017 katika Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 38(5) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.

Simba, Lipuli sasa kucheza Uhuru

Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Lipuli iliyopangwa kuchezwa Jumapili, Novemba 26, 2017 kwenye Uwanja wa Azam Complex sasa itafanyika kwenye Uwanja wa Uhuru.

Awali mechi hiyo ilihamishiwa Azam Complex baada ya wamiliki wa Uwanja wa Uhuru kueleza kuwa utakuwa na matumizi mengine Novemba 26, 2017. Hata hivyo, Novemba 22, 2017 Bodi ya Ligi Kuu ilipokea barua kutoka kwa Mmiliki wa Uwanja wa Uhuru ikieleza kuwa uwanja wake sasa uko wazi kuwa mwenyeji wa mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 10 jioni.

IMETOLEWA NA BODI YA LIGI KUU TANZANIA