.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumapili, 20 Aprili 2014

MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR BALOZI SEIF AFUNGA KONGAMANO LA MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA MUUNGANO


Wazanzibari na Watanzania wametanabahishwa kwamba baadhi ya mambo yaliyokuwa yakilalamikiwa kwa muda mrefu na Zanzibar yatokanayo na kero za Muungano yanaweza kushindikana kurekebishwa kisheria endapo mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya ya Muungano hautafikia lengo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alitanabahisha hilo wakati akilifunga Kongamano la siku moja la Maadhimisho ya Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar lililofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort iliyopo Mazizini Nje kidogo ya Mjini Zanzibar.

Balozi Seif alilitolea mfano Suala la Mafuta na Gesi ambalo Zanzibar inataka litolewe kabisa katika mambo yaliyomo ndani ya Muungano linaweza lisifikie usuluhishi kwa vile ni suala linalohitaji marekebisho ya kina ya Kisheria.



Alisema masuala yaliyojitokeza ndani ya mjadala wa Bunge Maalum la Katiba Tanzania na kupelekea baadhi ya Wajumbe wa Bunge hilo kuamua kususia mjadala huo yanaweza yakaikosesha fursa Zanzibar katika mchakato mzima wa kujiimarisha kiuchumi.

Alisema Taifa tayari limeshatumia gharama kubwa katika kuandaa mchakato huo wa Kupata Katiba Mpya ya Tanzania lakini baadhi ya Watu zaidi wakiwa wanasiasa wanajaribu kutafuta mbinu za makusudi za kukwamisha mchakato huo muhimu katika Historia ya Taila la Tanzanai ndani ya Kipindi cha Miaka 50 tokea kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar Tarehe 26 Aprili Mwaka 1964.

“ Yale mambo ambayo yamelalamikiwa na Zanzibar kwa muda mrefu kuhusu kero za Muungano hasa lile suala la Mafuta na Gesi yatashindwa kurekebishwa kisheria kupitia mchakato huo kama utakwama “. Alifafanua Balozi Seif.

Akizungumzia Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema suala la Elimu ya Muungano na umuhimu wake bado lina uzito mkubwa katika Jamii hasa Kizazi kilicho hivi sasa.

Alisema inashangaza kuona baadhi ya Watu hasa wanasiasa wamebeba bango la kuhoji uhalali na faida za Muungano huo visingizo vinavyoleta hofu kiasi kwamba umuhimu huo wa Elimu ya Muungano inastahiki ili jamii iepuke kupotoshwa na watu wa aina hiyo.

Alifahamisha kwamba Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na hasa Zanzibar imefaidia vilivyo na Muungano uliopo kwa vile tayari umeshalitangaza Taifa hili kwa upana zaidi ulimwenguni.

Alieleza kwamba Wananchi wengi wa Zanzibar zaidi ya Laki Nane sawa na asilimia 62% ya Wazanzibari wote wanaendelea kufaidika Kijamii na Kiuchumi upande mwengine wa Jamuhuri hiyo huko Tanzania Bara.

Balozi Seif alisema kuwa Uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla umeimarika kutokana na Mataifa, mashirika na Taasisi za Kimataifa kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika harakati zake za kujiletea maendeleo.

“ Mataifa mbali mbali Duniani yanaiona Tanzania watu wake ni wenye msimamo katika kuimarisha Umoja na kudumisha amani, msimamo ambao umewavutia wawekezaji wengi na kutamani kuwekeza miradi tofauti ya kiuchumi Nchini “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kwamba ni wajibu wa Jamii Nzima ya Wanzania kuendelea kuwakumbuka waasisi wa Muungano huo Marehemu Mzee Abeid Amani Karume na Marehemu Mwalimu Julius K ambarage Nyerere kwa mchango wao mkubwa uliofanikisha maendeleo yaliyopo hivi sasa.

Alisema fikra sahihi za waasisi hao zinapaswa kudumishwa na kuimarishwa ndani ya Muungano unaoendelea hivi sasa ili kuijenga Tanzania iliyostawi kwa maslahi ya wananchi wote,vizazi vya sasa ni vile vijavyo.

Balozi Seif aliwanasihi wnanchi wote kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali zote mbili ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar katika dhana nzima ya kudumisha na kuimarisha Muungano huo.

Akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kulifunga Kongano hilo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan alisema kwamba utekelezaji wa kero za Muungano uliohusisha pande zote mbili umefikia hatua nzuri.

Waziri Samia alisema Kamati ya pamoja na Viongozi waandamizi wa pande hizo mbili Chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imemaliza kazi ya kutanzua kero kumi kati ya 13 zilizowasilishwa kwenye Kamati hiyo.

“ Utekelezaji wa Kero za Muungano zilikuwa 13 zilizowasilishwa kwenye Kamati yetu na tayari tumeshazifanyia kazi. Hivi sasa zimebakia Tatu lakini ni sawa na kusema imebakia moja ile kubwa ya Kiuchumi “. Alifafanu Waziri Samia Suluhu Hassan.

Kauli mbiu ya Maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 50 ya Muungano wa Tannganyika na Zanzibar inasema “ Utanzania wetu ni Muungano wetu, Tuulinde, Tuuimarishe na Kuudumisha “.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

20/4/2014.


Hakuna maoni :

Chapisha Maoni