.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumapili, 21 Septemba 2014

WAZIRI MKUU MHE. MIZENGO PINDA ASEMA MCHAKATO WA BUNGE LA KATIBA NI HALALI

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema mchakato wa Bunge la Katiba unaoendelea hivi sasa ni halali na kwamba mchakato huo ni wa kisheria.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumapili, Septemba 21, 2014) wakati akizungumza na mamia ya waumini na viongozi mbalimbali waliohudhuria ibada ya uzinduzi wa dayosisi mpya ya Ziwa Tanganyika ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na kuwekwa wakfu Askofu Ambele Anyigulile Mwaipopo aliyeteuliwa kuongoza dayosisi hiyo. 
Dayosisi hiyo inakuwa ya 24 kwa kanisa hilo.

Waziri Mkuu alikuwa akitoa ufafanuzi wa hoja ya Askofu Mwaipopo aliyetaka maoni ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba yaheshimiwe na Bunge Maalum la Katiba lisitishwe kama ambavyo Jukwaa la Katiba limetaka na tamko la Jumuiya za Kikristo Tanzania (CCT) limetamka.

Waziri Mkuu alisema: “Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume hiyo siyo Katiba bali mawazo yaliyokusanywa ambayo yanapaswa kupitiwa na chombo kingine cha kisheria ambacho ni Bunge Maalum la Katiba. Mchakato huu halali na mchakato huo ni wa kisheria.”

Alisema muda ambao Tume hiyo ilipewa haukuwa mrefu sana kwa hiyo isingekuwa rahisi kwao kuzingatia kila eneo linalogusa maisha ya Watanzania. “Mfano suala la ardhi halikuelezwa vizuri katika rasimu lakini kwa sasa limeelezwa vizuri jinsi ardhi inavyoweza kumnufaisha Mtanzania kwenye kilimo, ufugaji, uvuvi na rasilmali misitu,” alisema.


Alisema kinachowachanganya Watanzania ni suala la Serikali mbili au tatu lakini katika makabrasha ya Tume ambayo wajumbe wote walipewa, suala la Muungano halikupewa kipaumbele na Watanzania wengi waliotoa maoni yao. “Kulikuwa na masuala makubwa sita. Suala la ukiukwaji wa haki za binadamu ndilo lilikuwa namba moja, suala lililopewa umuhimu wa pili lilikuwa ni la matatizo ya huduma za jamii na hilo la muungano lilichangiwa na kundi dogo sana,” alisema.



Alisema kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Jaji Warioba watu waliotaka Muungano wa Serikali tatu ni kati ya asilimia 12 na 13. “Haiwezekani kwa takwimu zile za asilimia 12 hadi 13 za kutaka Serikali tatu, iamuliwe jumla kwamba ni kwa niaba ya Watanzania wengi.”



Ili kukidhi shauku ya wengi, Waziri Mkuu alisema yuko radhi ifanyike kura mahsusi ya kuwaomba Watanzania waseme kama wanataka Muungano na tena uwe ni wa aina gani.



“Baba Askofu amesema tusitishe Bunge la Katiba, hivi sababu hasa ya kusitisha ni nini? Je sote tunajua hoja iliyowafanya wenzetu watoke nje na kususia ni ipi? Katika muda wa kuchangia kulikuwa na dakika 40 za wengi, dakika 20 za wachache na wakapewa dakika nyingine 30 za kuchangia. Muda ule ni mwingi mno kama hujaweka mchango wako kwenye maandishi. Badala yake, sote tulishuhudia kukashifiana, kejeli na kukashifiana.”



Aliwasihi Maaskofu, wachungaji na viongozi wengine wa dini waliohudhuria uzinduzi huo waendelee kuumboe mchakato huo ili uishe vizuri.



Katika hotuba yake, Waziri Mkuu alimuomba Askofu huyo mpya apokee jukumu hilo kwa mikono miwili na kumuahidi kuwa Serikali itasaidiana naye kuwaongoza Watanzania walioko kwenye dayosisi yake. Dayosisi hiyo mpya inahusisha mikoa ya Rukwa na Katavi eneo ambalo lina ukubwa wa kilometa za mraba 75,140. Kati ya hizo km. za mraba 27,713 ni za mkoa wa Rukwa na km. za mraba 47,527 ni za mkoa wa Katavi.



Alisema katika dayosisi hiyo mpya kuna changamoto nyingi kama vile za malezi ya vijana na watoto, tabia ya watu kutopenda kufanya kazi hasa vijana, kukosekana kwa injili kwenye maeneo wanayoishi wafugaji na suala la imani za ushirikina.



“Asilimia kubwa ya Watanzania ni vijana na wao ndiyo Taifa la leo. Ukiangalia mavazi ya vijana wa kike (vimini) na wa kiume (mlegezo) hutamani kuwaangalia mara ya pili. Msingi mkubwa wa kuwabadilisha hawa wote ni malezi ya kiroho. Una changamoto pia ya kufikisha neno la Mungu kwa wafugaji ambao ni wengi eneo hili lakini hawana muda wa kuabudu na wengi wao hawalijui neno la Mungu, wako bize na mifugo yao.”



“Lakini changamoto kubwa kuliko zote ni ya kubadili mtazamo wa jamii kuhusu Mkoa wa Rukwa hasa kwenye suala la ushirikina. Mtu hata kama hatoki huku bado ataweka bango akisema Mganga machachari kutoka Sumbawanga. Baba Askofu naomba tushirikiane kupiga sana vita imani hizi potofu kwa sababu zinachangia mauaji ya wazee na walemavu wa ngozi,” alisisitiza Waziri Mkuu.



Mapema, akitoa hotuba yake ya kwanza mara baada ya kusimikwa rasmi, Askofu Mwaipopo aliiomba Serikali isifumbie macho viashiria vyote vya upotevu wa amani kwani amani ni tunda la upendo na wala haipatikani kwa ncha ya upanga.



IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU

DAR ES SALAAM.

JUMAPILI, SEPTEMBA 21, 2014

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni