.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumanne, 1 Desemba 2015

BALOZI SEIF ATEMBELEA MRADI MKUBWA WA UJENZI WA KISIWA CHA KITALII, ZANZIBAR



Mradi mkubwa wa Kimataifa wa ujenzi wa kisiwa cha Kitalii ambacho kitatengezezwa kwa mfumo wa ufukiaji Bahari umeanza rasmi katika eneo la Hoteli ya Utalii iliyopo Mtoni Marine kaskazini Magharibi ya Mji wa Zanzibar.

Hata hivyo gharama kamili za Mradi huo bado hazijafahamika wakati utakapokamilika rasmi ujenzi wake hapo baadaye.

Mradi huo unaoendeshwa na Kampuni ya Kizalendo ya Baghresa Group utahusisha ujenzi wa Hoteli ya Kimataifa ya Ghorofa Tano ya Daraja la Tano { Five Star + }, utengenezaji wa eneo la wazi la mapumziko { Public Beach } pamoja na kutengeneza Kisiwa cha Mji mpya .

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alishuhudia harakati za ujazaji wa mchanga katika eneo linalofukiwa ambazo hufanywa kwa utaalamu wa hali ya juu.

Mhandisi wa Mradi huo Bwana Ahmed Shamsi alimueleza Balozi Seif kwamba chombo maalum kinachotumika kwa kazi ya uchimbaji wa mchanga Baharini kina uwezo wa kunyonya na kusafirisha mchanga kutoka ndani ya Bahari sambamba na kukata Majabali.

Mhandisi Shamsi alisema kazi hiyo inafanyika kwa saa 12 kila siku ambapo takwimu zinaonyesha wazi kwamba uchimbaji huo wa mchanga unaokwenda zaidi ya mita 15 chini ya Bahari unafikia Tani 600 za mchanga kwa saa Moja.

Alifahamisha kwamba harakati za uchimbaji na kufukia mchanga katika eneo hilo zilizoanza Mwezi uliopita wa Novemba zinatarajiwa kukamilika mwezi Januari mwaka ujao.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Baghresa Group Bwana Said Salim Baghresa alisema kwamba ujenzi wa mradi huo muhimu kwa uchumi wa Nchi utasaidia mapato ya Taifa pamoja na kutoa ajira kubwa kwa vijana Wazalendo hapa Nchini.

Bwana Baghresa alisema mfumo wa ufukiaji Bahari kwa ajili ya kuanzisha miradi ya Kiuchumi ni mfumo unaotumiwa na Mataifa mbali mbali Duniani ambapo kwa Afrika mradi kama tayari umeanza kutumiwa katika Kisiwa cha Seycheles.

Akitoa nasaha zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameupongeza Uongozi wa Baghresa Group kwa uamuzi uliochukuwa wa kuanzisha mradi huo mkubwa wa Kimataifa.

Balozi Seif alieleza kwamba kukamilika kwa mradi huo mkubwa ambao umeshazoeleka katika Mataifa yaliyoendelea utasaidia kuitangaza Zanzibar na Tanzania kwa ujumla Kiutalii Kimataifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhakikishia Uongozi huo wa Baghresa Group kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa kila msaada unaohitajika katika kuona mradi huo unafikia malengo uliojipangia.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamui wa Pili wa Rais wa Zanzibar


Hakuna maoni :

Chapisha Maoni