.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatatu, 4 Aprili 2016

WAZIRI PROF. MBARAWA AKAGUA BARABARA YA TABORA-KOGA-MPANDA KM 356

1 
Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Katavi Eng. Abdon Maregesi akimuonesha athari za mvua Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kulia kwake) wakati akikagua daraja la Koga lililoathirika. Daraja hilo linaunganisha mkoa wa Katavi na Tabora.
2
Muonekano wa Daraja la Koga baada ya kufanyiwa ukarabati kufuatia kuathiriwa na mvua kubwa zilizonyesha katika mkoa wa Katavi. Daraja hilo kwa sasa linaruhusu magari kupita ya tani 1 hadi 3.
3
Muonekano wa barabara ya Tabora-Koga-Mpanda yenye urefu wa Km 356 inayojengwa kwa kiwango cha lami ikiwa katika hatua za awali za ujenzi wake.
4
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa mkandarasi wa kampuni ya CICO anayejenga barabara ya Tabora-Koga- Mpanda yenye urefu wa Km 356, sehemu ya Tabora-Sikonge kumaliza mradi huo kwa wakati.
5
Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Bi. Hanifa Sirengu akitoa taarifa kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa kuhusu hali ya miundombinu katika wilaya yake.
6
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) wakati alipotembelea kiwanja cha ndege cha Tabora.
7
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akisikiliza maelezo ya namna vifaa vya kuongozea ndege vinavyofanya kazi kutoka kwa mtaalamu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), mkoa wa Tabora.
8
Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto Uwanja wa ndege wa Tabora Bw. Yahya Nassoro akitoa maelezo ya namna gari la kuzimia moto linavyofanya kazi katika uwanja huo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho kuanza mradi wa ujenzi wa barabara ya Tabora-Koga-Mpanda yenye urefu wa Km. 356 kwa kiwango cha lami ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Awamu ya Tano aliyoitoa kwa wananchi wa Mikoa ya Katavi na Tabora.

Ametoa kauli hiyo wilayani Sikonge mkoani Tabora, mara baada ya kukagua barabara hiyo ambapo pamoja na mambo mengine amesema ujenzi huo unatarajia kuanza rasmi hivi karibuni.

‘Ujenzi wa barabara hii tumeugawa katika sehemu tatu ili kuharakisha utekelezaji wake, tutahakikisha ifikapo mwisho wa mwaka huu, makandarasi wote watatu watakuwa katika maeneo yao ya kazi’, amesema Prof. Mbarawa.

Amesisitiza kuwa wananchi wanaostahili kulipwa fidia watalipwa kwa wakati kwa kuwa takribani shilingi bilioni moja zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo.

Prof. Mbarawa pia amekagua daraja la Koga linalounganisha Mkoa wa Katavi na Tabora na kuwataka viongozi wa mikoa hiyo kuhakikisha kuwa magari yasiyozidi tani tatu ndio yanayopita katika daraja hilo ili kuepusha ajali hadi ukarabati mkubwa utakapofanyika.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Kanali Mstaafu Issa Nziku amemuomba Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupandisha hadhi baadhi ya barabara katika Wilaya hiyo ili zihudumiwe na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kutokana na uwezo mdogo wa Halmashauri hiyo kuzikarabati kila wakati.

Katika Hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua uwanja wa Ndege wa Tabora na kuwataka viongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania(TCAA) kuangalia namna bora ya ukarabati wa kiwanja hicho ili uruhusu ndege kubwa kutua na kuongeza biashara.

Prof. Mbarawa yuko katika ziara ya siku saba ya kukagua miundombinu ya taasisi zilizo chini ya Wizara yake katika mikoa ya Magharibi ili kuifungua kanda hiyo kimiundombinu na hivyo kufufua fursa za kiuchumi.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni