.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Ijumaa, 26 Mei 2017

NI FAINALI ZA AZAM SPORTS FEDERATION CUP 2016/17

Kesho Jumamosi, Mei 27 mwaka huu Simba SC ya Dar es Salaam na Mbao FC ya Mwanza zitakutana Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma kwenye fainali za kuwania Kombe la Shirikisho la Azam yaani Azam Sports Federation Cup - ASFC 2016/17 katika mchezo utakaoanza saa 10.00 jioni.
 

Kwa mujibu wa kanuni ya 7 (2) za michuano ya ASFC, ratiba ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports HD itatolewa na TFF na ndiyo kesho itachezwa.
 

Kadhalika kwa mujibu wa Kanuni ya 6 (2), Mshindi wa mchezo wa fainali (Kwa msimu huu kati ya Simba na Mbao), ndiye akayekuwa Bingwa wa Kombe la ASFC, atapewa Kombe la Ubingwa na zawadi ya fedha kiasi cha shilingi milioni hamisini (50,000,000/-) kama zilivyoainishwa kwenye waraka wa zawadi wa michuano.
 

PONGEZI ZA INFANTINO KWA YOUNG AFRICANS
 

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino, Mei 24, mwaka huu alituma ujumbe Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuipongeza Young Africans ya Dar es Salaam kwa kutwaa ubingwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2016/17.
 

Young Africans imetwaa Kombe hilo ikiwa ni mara tatu mfululizo na katika salamu za pongezi, Rais Gianni Infantino amesema ubingwa huo wa Young Africans ni kielelezo cha ushirikiano baina ya wachezaji, kocha, utawala, matabibu pamoja na mashabiki.
 

Katika pongezi zake Rais Infantino ameishukuru Young Africans na shirikisho la mpira wa miguu la nchi kwa kusadia kupeleka ujumbe chanya kwa jamii kuhusiana na mpira wa miguu.

UAMUZI WA ADHABU MBALIMBALI KUTOKA KAMATI YA SAA 72

Mechi namba 206 (Yanga 1 Vs Toto Africans 0).
 

Klabu ya Yanga imepigwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kutokana na timu yake kutoingia vyumbani wakati wa mechi hiyo iliyochezwa Mei 9, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu. Uamuzi huo umezingatia pia kuwa Yanga imekuwa ikirudia kosa hilo mara kwa mara.

Mechi namba 225 (JKT Ruvu 0 Vs Majimaji 1).

Timu ya Majimaji haikuingia vyumbani wakati wa mapumziko katika mechi hiyo iliyofanyika Mei 13, 2017 katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Kutokana na timu hiyo kurudia kufanya kosa hilo, klabu ya Majimaji imepigwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja). Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu.

Mechi namba 230 (Kagera Sugar 2 Vs Mbao FC 0).

Klabu ya Mbao imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na timu yake kutoingia vyumbani wakati wa mechi hiyo iliyochezwa Mei 13, 2017 katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu.

Mechi namba 231 (Yanga 2 Vs Mbeya City 1).

Timu zote mbili hazikupita kwenye mlango rasmi wakati wa kuingia uwanjani katika mechi hiyo iliyochezwa Mei 13, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Hivyo, kila klabu imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na kitendo hicho, uamuzi ambao umezingatia Kanuni ya 14(48).

Pia klabu ya Yanga imepigwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kutoingia vyumbani kwenye mechi hiyo. Adhabu hiyo pia imezingatia Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu.

Mechi namba 236 (Mbao FC 1 Vs Yanga 0).

Klabu ya Yanga imepigwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kupita mlango usio rasmi katika mechi hiyo iliyofanyika Mei 20, 2017 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu.

Pia Yanga imepigwa faini ya sh. 1,500,000 (milioni moja na laki tano) kwa kutoingia vyumbani. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(8) ya Ligi Kuu. Vilevile klabu hiyo imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na kuonyesha vitendo vinavyoashiria ushirikiana. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu.

Washabiki wa Yanga walivunja uzio wa ndani (fence) wa upande wa Magharibi wakati wakiingia uwanjani kusherehekea ubingwa wa timu hiyo. Hivyo, klabu ya Yanga imeagizwa kulipa gharama za uharibifu huo uliofanywa na washabiki wake, uamuzi ambao umezingatia Kanuni ya 42(3) ya Ligi Kuu.
 

Nayo klabu ya Mbao FC imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na washabiki wake kuingia uwanjani kushangilia baada ya timu yao kupata ushindi.

Wachezaji Deus Kaseke, Simon Msuva na Obrey Chirwa wa Yanga wamesimamishwa kucheza mechi za Ligi Kuu wakati wakisubiri suala lao la kumsukuma na kumwangusha Mwamuzi Ludovic Charles kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Walifanya kitendo hicho katika mechi hiyo dhidi ya Mbao FC iliyofanyika Mei 20, 2017 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijni Mwanza. Uamuzi wa Kamati umezingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu.

Mwamuzi Ludovic Charles amepewa onyo kali kwa kutodhibiti vizuri mchezo. Uamuzi dhidi yake ni kwa mujibu w Kanuni ya 38(5) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.


IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni