.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatatu, 22 Mei 2017

SERIKALI YATOLEA UFAFANUZI VIWANGO VYA RIBA KATIKA TAASISI ZA FEDHA

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango (MB), Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji,

                                                                                   Benny Mwaipaja, WFM-Dodoma

Serikali imesema kuwa mabadiliko ya sekta ya fedha ya mwaka 1991 yalipelekea Serikali kujitoa katika uendeshaji wa moja kwa moja wa shughuli za kibenki nchini ili kuruhusu mfumo wa Soko Huria, hususan nguvu ya soko kuamua viwango vya riba za mikopo, riba za amana na gharama zingine za huduma za kibenki.

Kauli hiyo imetolewa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango (MB), Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Jesca David Kishoa (CHADEMA), aliyehoji licha ya kuwa na benki nyingi zaidi kuliko nchi zote Kusini na Mashariki mwa Afrika, kwa nini wingi huo bado haujaleta unafuu katika tozo ya riba.

Akijibu swali hilo Mhe. Dkt. Kijaji alisema kuwa, viwango vya riba za mikopo hupangwa kwa kuzingatia gharama za upatikanaji wa fedha, uendashaji, bima, sifa za mkopaji na hatari ya mkopaji kutolipa mkopo, pamoja na kasi ya mfumuko wa bei.
 

“Dhana ya uhitaji na utoaji wa mikopo siyo kigezo pekee kinachoweza kupunguza viwango vya riba hapa nchini, hatari ya kutolipa mkopo ni kigezo kikubwa kinachotumiwa na benki kupanga viwango vya riba za mikopo, hususan kwa wajasiriamali wadogo”. Alisema Dkt. Kijaji

Dkt. Kijaji aliongeza kuwa, uzoefu uliopo unaonesha kuwa, benki zinapendelea kukopesha wajasiriamali waliojiunga katika vikundi kuliko mjasiriamali mmoja mmoja ili kupunguza kiwango cha mikopo isiyolipika.


Aidha, Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Jesca David Kishoa, alihoji ni kwa nini Serikali isiweke ukomo wa riba kisheria kwa benki hizo ili kumsaidia mjasiriamali wa sekta binafsi kama ilivyofanya nchi ya Kenya.
 

Dkt. Kijaji alifafanua kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Taasisi za Fedha ya Mwaka 1991, iliyotungwa kwa kuzingatia misingi ya mfumo wa soko huria, Benki Kuu imepewa jukumu na mamlaka ya kusimamia na kuzichukulia hatua taasisi za fedha zinazoendesha shughuli zao kwa hasara.
 

Aliongeza kuwa, kutoa maelekezo kwa benki kutumia viwango fulani vya riba, kutaifanya Benki Kuu kukosa nguvu na mamlaka ya kuzichukulia benki hatua endapo zitapata hasara kwa kutumia riba ambayo Benki Kuu imeelekeza.
 

Katika swali la nyongeza Mbunge huyo, alieleza kuwa mikopo isiyolipika imekua kwa kiwango kikubwa tangu mwaka 1991 huku akitaja sababu kubwa mbili ambazo ni mazingira magumu ya biashara pamoja na riba kubwa kwa wafanyabiashara hao.
 

‘’Je Serikali haioni umuhimu wa kuwasaidia kwa kuwapa riba nafuu ili iweze ‘Kustimulize’ (kuchochea) biashara zao’’. Alihoji Mhe. Kishoa.

Akijibu swali hilo la nyongeza Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji alisema kuwa kutokana na mabadiliko ya mfumo wa mwaka 1991 ya sheria ya Mabenki na Taasisi za fedha, Benki Kuu au Serikali haiwezi kutoa mweleko au ukomo wa Taasisi za fedha.


Hakuna maoni :

Chapisha Maoni