.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumamosi, 24 Juni 2017

BALOZI SEIF AKAGUA UJENZI WA MSIKITI MITONDOONI WILAYA YA MAGAHARIBI B

Jengo la Msikiti Mitondooni linalojengwa katika Mtaa wa Kisauni Wilaya ya Magharibi “B” Mkoa wa Mjini Magharibi linalotarajiwa pia kuwa Kitengo cha Elimu ya Dini itakayofundishwa kwa Lugha Nne za Kimataifa.
Ramani ya Jengo la Msikiti Mitondooni itakavyokuwa baada ya kukamilika litakalofanana na Msikiti Mabuluu uliopo Kinazini Kusini mwa Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar.
Muonekano wa uendelezaji wa Jengo la Msikiti wa Mitondooni liliopo katika Mtaa wa Kisauni Wilaya ya Magharibi “B”.  Picha na – OMPR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameziagiza Taasisi zinazosimamia Mipango Miji, Mazingira, Ardhi na Halmashauri kukaa pamoja na Mjenzi wa Jengo la Msikiti wa Mitondooni Kisauni ili kuzitafutia ufumbuzi hitilafu zilizojitokeza katika uendelezaji wa ujenzi huo.

Alisema Taasisi zinayohusika na Mipango Miji lazima zihusike kikamilifu katika utafiti wa kina wa michoro ya ujenzi huo na kuridhina nayo kulingana na mazingira ya eneo lenyewe ili hatua za ujenzi ziende bila ya kuibuka kasoro nyengine hapo baadae.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo alipofanya ziara fupi ya kukagua jengo la Msikiti linalojengwa katika Mtaa wa Mitondooni Kisauni Wilaya ya Magharibi “ B”linalotarajiwa kuwa na Kitengo cha madarasa ya Elimu ya Dini itakayofundishwa kwa lugha Nne za Kimataifa.

Alisema ujenzi wa majengo ya Taaluma na Ibada yanayozunguuka Makazi ya Watu ambayo yako katika maeneo yasiyo ya kawaida kama vile sehemu zinazotuwama maji yanahitaji kufanyiwa utafiti mkubwa ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza wakati wa kuanza kwa matmizi ya majengo hayo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar isingepelea kushuhudia mizozo na migongano inayojichomoza kati ya Wananchi na Wafadhili au wadau wanaoamua kusaidia miradi inayotekelezwa kwa faida ya kuinufaisha Jamii.

Balozi Seif aliziasa Taasisi zinazosimamia masuala mbali mbali Nchini kuhakikisha kwamba zinawajibika ipasavyo kwa Watendaji wake kufuatilia au kukagua miradi wanayoisimamia ili kuwepuka mapema athari inayoweza kujitokeza hapo baadae.

Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Idara ya Mipango Miji na Vijiji Zanzibar Nd. Muhammad Juma alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Taasisi yake itakuwa tayari kumsaidia Mjenzi wa Jengo hilo la Msikiti katika azma yake ya kuweka vitenga uchumi vinavyolenga kuuendesha Msikiti huo.

Nd. Muhammad alisema hatua hiyo itachukuliwa kutokana na hali halisi ya eneo linalojengwa Msikiti huo kuwa na kawaida ya uhifadhi wa maji yanayotokea milimani wakati wa msimu wa mvua za Masika unapofikia.

Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Idara ya Mipango Miji na Vijiji alikiri kwamba Taasisi yake bado ina ipungufu wa Maafisa wanaohusika na Ukaguzi na ufuatiliaji wa masuala yanayohusu ujenzi katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba.

Ujenzi wa Msikiti Mitondooni uliopo katika Mtaa wa Kisauni kwa mujibu wa Michoro, Ramani na maazingira ya eneo lake unatarajiwa ujenzi wake kulingana na Msikti Mabuluu uliopo Kinazini Mjini Zanzibar.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
24/6/2017.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni