.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Alhamisi, 8 Juni 2017

BALOZI SEIF ASHIRIKI MAZIKO YA MZEE KHAMIS JUMA MKADARA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wa Tatu kutoka Kulia akijumuika pamoja na Viongozi na Wananchi katika kumsalia Mwanasiasa Mkongwe wa Kisiwani Pemba Mzee Khamis Juma Mkadara kwenye Msikiti wa Ijumaa Wawi Chake chake Pemba.
Kushoto ya Balozi Seif ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dr. Juma Abdulla Juma {Mabodi } na kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Kilimo, Mali Asili, Mifugo na Uvuvi Mh. Hamad Rashid Mohamed.
Baadhi ya Waumini wa Dini ya Kiislamu wa Mtaa wa Wawi Chake chake wakiwa miongoni mwa wananchi waliomsalia Kiongozi huyo nguli wa Kisiasa Kisiwani Pemba Mzee Mkadara.
Balozi Seif akimimina mchanga katika Kaburi la Mzee Khamis Juma Mkadara aliyezikwa katika Mavani ya Familia yake yaliyopo Mashariki ya Msiku wa Ijumaa wa Wawi Chake chake.
Balozi Seif wa Pili kutoka Kulia akiwa sambamba na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dr. Juma Abdulla Juma { Mabodi } wakiwafariji wanafamilia ya Mwanasiasa Mkadara Nyumbani kwake Wawi Chake chake.
Baadhi ya Wanafamilia ya Mzee Khamis Juma Mkadara wakionyesha sura za majonzi na huzuni kufuatia kuondokewa na mpendwa wao aliyekuwa kiungo katika familia hiyo.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dr. Juma Abdulla Mabodi wa Pili kutoka Kulia akiwataka kuwa na moyo wa subra Wajukuu wa Mzee Mkadara.

                                                                                                    Picha na – OMPR – ZNZ.
 

Mwanasiasa Mkongwe wa Zanzibar Mzee Khamis Mkadara aliyefariki Dunia mapemba jana asubuhi amezikwa Kijijini kwake Wawi Mkoa wa Kusini Pemba maziko yaliyohudhuriwa na Mamia ya Waumini wa Dini ya Kiislamu, Wananchi pamoja na Viongozi wa Kiserikali na Kisiasa.

Mzee Khamis Mkadara alikuwa akisumbuliwa na Maradhi ya kawaida pamoja na uzee alifariki nyumbani kwake Mtaa wa Wawi Wilaya ya Chake chake Mkoa wa Kusini Pemba.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika mazishi hayo aliiwakilisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Chama cha Mapinduzi akijumuika na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dr. Juma Abdulla Mabodi na baadhi ya watendaji wa Serikali.

Marehemu Mzee Khamis Juma Mkadara alizaliwa Mwaka 1927 na kuanza elimu ya Quran katika Madrasa mbali mbali za Wilaya ya Chake chake ambapo baadaye katika ujana wake akajishughulisha na masuala ya Kisiasa katika dhana nzima ya kudai Uhuru wa Visiwa vya Zanzibar.

Katika kipindi hicho ya kutaka kujikomboa Mzee Mkadara alikuwa muanzilishi wa Chama cha Shirazy Association na baadaye kukiunganisha na chama cha African Association na Kuzaliwa kwa Chama cha Afro Shirazy Party.

Katika utumishi wa Chama Mzee Khamis Juma Mkadara aliwahi kuwa Mwenyekiti wa ASP wa Wilaya ya Chake chake mwaka 1973 na baada ya kuzaliwa Chama cha Mapinduzi mwaka 1977 aliendelea na wadhifa huo hadi mwaka 1997.

Mbali ya wadhifa huo wa Kichama Mzee Mkadara pia aliwahi kuwa Diwani wa Wadi ya Wawi mwaka 1995.

Mwanasiasa huyo mkongwe Kisiwani Pemba alikuwa mstawi wa mbele katika utetezi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar akiwa miongoni mwa Wazee waliotumikia kwa kiindi kirefu Taifa hili la Tanzania.

Utumishi huo uliweza kumpatia fifa na ushujaa uliopelekea kutunukiwa nishani na Rais Mstaafu wa Tanzania Awamu ya Nne Dr. Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na Rais wa Zanzibar wa Awamu ya Sita Dr. Aman Abeid Karume.

Mzee Khamis Juma Mkadara aliyefikisha umri wa Miaka 90 ameacha Kizuka Mmoja, Watoto Wanane na Wajukuu 33.

Mwenyezi Muungu ailaze roho ya Mwanasiasa huyo Mkongwe Mzee Khamis Juma Mkadara mahali pema peponi. Amin.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
8/6/2017.


Hakuna maoni :

Chapisha Maoni