.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Alhamisi, 8 Juni 2017

HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA DKT. PHILIP I. MPANGO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI TAARIFA YA HALI YA UCHUMI 2016 NA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA KWA MWAKA 2017/18


             Tamaa yangu, na kwa kweli jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano, zitakuwa katika ujenzi wa uchumi wa kipato cha kati ambapo sura na maisha ya Watanzania walio wengi yafanane fanane na nchi ya kipato cha kati. Njia moja ya kutufikisha huko ni uendelezaji wa viwanda.

Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tarehe 20 Novemba 2015, BUNGENI, DODOMA.

 UTANGULIZI

1.          Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee na kujadili Taarifa ya Hali ya Uchumi kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/18. Pamoja na hotuba hii nawasilisha vitabu vya Taarifa ya Hali ya Uchumi kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/18, ambapo taarifa hizi ndio msingi wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/18 itakayowasilishwa Bungeni baadaye hivi leo.

2.          Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai na afya njema na kutuwezesha kukutana katika Mkutano wa 7 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tukiwa na dhamira ya kulinda na kuendeleza amani na maelewano hapa nchini, na pia ari ya kufikia malengo yetu ya maendeleo. Napenda kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika, Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa Bunge kwa kuendesha majadiliano ya Bajeti za Kisekta na shughuli nyingine za Bunge hili kwa umakini, utulivu na hekima kubwa. Ni matumaini yangu kuwa uzalendo uliojionesha katika kujadili hotuba za mipango na bajeti za kisekta utaendelea kudumishwa.

3.          Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kutoa pole kwako, Waheshimiwa Wabunge wote na wananchi kwa kuondokewa na wabunge wenzetu, Mheshimiwa Hafidh Ally Tahir aliyekuwa Mbunge wa Dimani (CCM) na Mheshimiwa Dkt. Elly Marko Macha, Mbunge wa Viti maalum (CHADEMA). Pia, nitumie fursa hii kuwapa pole wabunge wote waliopoteza wapendwa wao na wananchi wote waliopatwa na maafa mbalimbali katika mwaka huu, yakiwemo matukio ya kusikitisha ya kuondokewa na watoto wetu 32, walimu wawili na dereva wa shule ya Lucky Vincent katika ajali mkoani Arusha mwezi uliopita, wanafunzi watatu kule mkoani Geita, wanafunzi wawili na mzazi mmoja mkoani Kagera kwa kuzama majini na Askari wetu nane na wananchi wengine waliouawa kikatili katika matukio ya kupanga mkoani Pwani. Tunamwomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema, peponi.

4.          Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa, napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wasaidizi wake wakuu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais na Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi madhubuti kusimamia mabadiliko yanayoleta tija katika utendaji Serikalini, kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nakuendeleza misingi ya utawala bora. Uongozi wao umejipambanua katika kupambana na rushwa, ufisadi, ukwepaji kodi, uzembe na urasimu katika utumishi wa umma na ubadhirifu wa mali za umma lakini pia msisitizo wa umuhimu wa kila mwananchi kufanya kazi. Juhudi hizi zinapaswa kuungwa mkono kwa nguvu zote na viongozi na Wananchi wote.

5.          Mheshimiwa Spika, niruhusu pia niwapongeze kwa dhati wabunge wapya walioingia Bungeni katika mkutano huu wa 7 wa Bunge la 11 ambao ni: Mheshimiwa Salma R. Kikwete, Mheshimiwa Dkt. Gertrude Pangalile Rwakatare, wote wa CCM na Mheshimiwa Dkt. Catherine Ruge wa CHADEMA. Tunawakaribisha kuungana na Waheshimiwa Wabunge wengine kutekeleza wajibu wa msingi wa Bunge wa kuishauri na kuisimamia Serikali kwa hekima na weledi na kuweka mbele maslahi ya Taifa kwa manufaa ya Watanzania. Nawapongeza pia Waheshimiwa Wabunge kutoka vyama vyote waliochaguliwa na Bunge hili kuiwakilisha nchi yetu katika Bunge la Afrika Mashariki. Matarajio yetu ni kuwa watalinda na kusimamia na kutetea vema maslahi ya nchi yetu katika Bunge hilo la Afrika Mashariki.

 6.          Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuishukuru sana Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, inayoongozwa na Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini; na Makamu wake, Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kwa maelekezo na ushauri wa kizalendo waliotupatia, ambao umesaidia kuboresha taarifa za mwenendo wa uchumi wa Taifa kwa mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2017/18, ninazoziwasilisha.

7.          Mheshimiwa Spika, hotuba ninayoiwasilisha imegawanyika katika maeneo makuu matano (5): eneo la kwanza ni utangulizi, la pili ni taarifa ya mapitio ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2016 na robo ya kwanza ya 2017; eneo la tatu, ni Muhtasari wa Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2016/17; nne, ni Maeneo ya Kipaumbele ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo kwa mwaka 2017/18; na mwisho, ni Majumuisho.

MWENENDO WA HALI YA UCHUMI 2016

Uchumi wa Dunia

8.          Mheshimiwa Spika, Kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia kwa mwaka 2016, ilikuwa asilimia 3.1 ikilinganishwa na asilimia 3.2 mwaka 2015. Kupungua huku ni matokeo ya kupungua kwa ukuaji wa uchumi katika nchi zilizoendelea, ambapo ukuaji wa uchumi kwa nchi zilizoendelea kilikuwa asilimia 1.7 mwaka 2016 ikilinganishwa na asilimia 1.9 mwaka 2015, ukichangiwa na kushuka kwa mahitaji ya bidhaa na huduma katika masoko mengi duniani na kupungua kwa tija ya uzalishaji na kasi ya uwekezaji. Kasi ya ukuaji wa uchumi kwa nchi zinazoendelea ilikuwa asilimia 4.1 sawa na ilivyokuwa mwaka 2015. Ukuaji huu kwa nchi zinazoendelea ulichangiwa zaidi na kupungua kwa ukuaji wa uchumi kwa nchi za China na Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kufuatia kuporomoka kwa bei za bidhaa hasa bidhaa ghafi katika soko la dunia, kupungua kwa uwekezaji wa moja kwa moja wa sekta binafsi na kushuka kwa mahitaji ya bidhaa zinazozalishwa katika masoko mengi duniani.

9.          Mheshimiwa Spika, mfumuko wa bei duniani uliongezeka kufikia wastani wa asilimia 2.9 mwaka 2016 ikilinganishwa na asilimia 2.8 mwaka 2015. Kwa kiasi kikubwa mfumuko wa bei uliongezeka kutokana na kulegezwa kwa sera za bajeti na fedha kwa baadhi ya nchi na ukame uliochangiwa na mabadiliko ya hali ya hewa (yanayojulikana kama La Nina). Mfumuko wa bei kwa nchi zilizoendelea uliongezeka kufikia asilimia 0.8 kwa mwaka 2016 ikilinganishwa na asilimia 0.3 mwaka 2015, ambapo kwa nchi zinazoendelea za Asia, uliongezeka hadi asilimia 3.1 kutoka asilimia 2.7 mwaka 2015. Kwa nchi za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, ulifikia asilimia 11.4 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2015.

Uchumi wa Afrika na Kikanda

10.     Mheshimiwa Spika, kwa upande wa nchi za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, wastani wa kasi ya ukuaji wa uchumi ilipungua kutoka asilimia 3.4 mwaka 2015 hadi asilimia 1.4 mwaka 2016. Hii ni kutokana na kupungua kwa upatikanaji wa mikopo kutoka kwenye masoko ya kimataifa uliosababisha miradi iliyopangwa katika kipindi hicho kushindwa kukamilika, kuendelea kwa migogoro ya kisiasa  kwa baadhi ya nchi (Burundi, Libya, Chad, Sudan Kusini na DRC), na kuporomoka kwa bei za baadhi ya mazao ghafi, hususan, dhahabu na mafuta ya petroli.

11.     Mheshimiwa Spika, kasi ya ukuaji wa uchumi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ilishuka kutoka wastani wa asilimia 6.5 mwaka 2015 hadi asilimia 5.3 mwaka 2016 ijapokuwa Jumuiya hii iliendelea kuongoza kwa ukuaji miongoni mwa Jumuiya mbalimbali za Afrika. Kasi ndogo ya ukuaji wa uchumi katika Jumuiya hii ilichangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo kushuka kwa bei za bidhaa na kudorora kwa uchumi wa dunia. Maoteo ya mwenendo wa uchumi katika ukanda huu yanaonesha utakua kwa wastani wa asilimia 5.7 mwaka 2017 na asilimia 6.0 mwaka 2018. Matarajio haya yanazingatia hatua zinazochukuliwa na nchi za ukanda huu katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na uendeshaji biashara kama vile kuwa na maeneo tengefu ya ujenzi wa viwanda (industrial parks), hususan, vya nguo, bidhaa za ngozi, kilimo, madawa na vifaa tiba.

12.     Mheshimiwa Spika, Mfumuko wa bei katika nchi za Afrika Mashariki kwa mwaka 2016 uliendelea kuwa wa kiwango cha tarakimu moja, ambapo Rwanda ilikuwa na asilimia 7.1, Uganda asilimia 5.4, Tanzania asilimia 5.2, Kenya asilimia 6.3 na Burundi asilimia 5.6. Aidha, kufikia Machi 2017, mfumuko wa bei kwa nchi hizi ulipanda, ambapo kwa Burundi ulifikia asilimia 21.10, Rwanda asilimia 13.0; Kenya asilimia 10.28; Uganda asilimia 6.4 na Tanzania asilimia 6.4. Hali hii ilichangiwa na ukame katika maeneo mengi ya ukanda huu kutokana na kuchelewa kwa msimu wa mvua.

13.     Mheshimiwa Spika, kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, yaani SADC, kasi ya ukuaji wa uchumi ilishuka kutoka wastani wa asilimia 1.9 mwaka 2015 hadi asilimia 1.1 mwaka 2016. Kasi ndogo ya ukuaji wa uchumi katika Jumuiya hii ilichangiwa na uhaba wa nishati ya umeme pamoja na ukame uliochangiwa na mabadiliko ya hali ya hewa ya La Nina. Licha ya kasi ndogo ya ukuaji, Jumuiya hii iliendelea kuwa ya tatu kwa ukuaji miongoni mwa Jumuiya za barani Afrika na unatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 1.4 mwaka 2017. Mfumuko wa bei ulifikia asilimia 10.5 mwaka 2016 ikilinganishwa na asilimia 5.7 mwaka 2015, ukichangiwa na ukame na kuyumba kwa utekelezaji wa sera za mapato na matumizi kwa baadhi ya nchi wanachama. Matarajio ni kuwa kwa mwaka 2017 mfumuko wa bei utapungua hadi kufikia asilimia 8.7 kutokana na kushuka kwa gharama za bidhaa, kuimarika kwa upatikanaji wa nishati ya umeme, na uthabiti wa bei ya mafuta; na kuimarika kwa hali ya hewa.


Uchumi wa Taifa

Ukuaji wa Uchumi na Pato la Taifa 

14.     Mheshimiwa Spika, Pato la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 7.0 kwa mwaka 2016, kama ilivyokuwa mwaka 2015. Kiwango hiki hata hivyo ni chini ya maoteo ya kufikia asilimia 7.2 kutokana na ukuaji wa baadhi ya shughuli kushindwa kufikia maoteo ya viwango vya ukuaji. Baadhi ya shughuli za kiuchumi ambazo zilishindwa kufikia maoteo ya viwango vya ukuaji ni pamoja na: sekta ya kilimo iliyokua kwa asilimia 2.1 ikilinganishwa na maoteo ya asilimia 2.9; biashara na matengenezo asilimia 6.7 dhidi ya asilimia 7.8; huduma za malazi na chakula asilimia 3.7 kinyume na maoteo ya asilimia 8.0; na huduma za utawala asilimia 2.1 ikilinganishwa na maoteo ya asilimia 6.3. Aidha, zipo shughuli za kiuchumi zilizokua na hata kuzidi maoteo. Shughuli za uchumi zilizokuwa na viwango vikubwa vya ukuaji ni pamoja na: habari na mawasiliano asilimia 13.0 dhidi ya maoteo ya asilimia 12.1; usafirishaji na uhifadhi mizigo asilimia 11.8 dhidi ya maoteo ya asilimia 8.0; uchimbaji madini na mawe asilimia 11.5 dhidi ya maoteo ya asilimia 9.2; na uzalishaji viwandani asilimia 7.8 ikilinganishwa na maoteo ya asilimia 6.7.

Mchango wa Kisekta katika Pato la Taifa

15.     Mheshimiwa Spika, mchango wa shughuli za kilimo (mazao, ufugaji, misitu na uvuvi) katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 29.1 mwaka 2016 ikilinganishwa na asilimia 29.0 mwaka 2015. Shughuli za viwanda na ujenzi zilichangia asilimia 25.2 ya Pato la Taifa mwaka 2016 ikilinganishwa na asilimia 24.3 mwaka 2015, ambapo mchango wa sekta za huduma (ikijumuisha biashara na matengenezo, usafirishaji na uhifadhi mizigo, malazi, habari na mawasiliano, fedha na bima, upangishaji majumba, elimu na afya) ulikuwa asilimia 39.1 mwaka 2016 ikilinganishwa na asilimia 40.0 mwaka 2015. Kuongezeka kwa mchango wa shughuli za viwanda, ni dalili kuwa azma ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda imeanza kuleta matokeo chanya, ambapo tija na uzalishaji viwandani unaimarika. Pamoja na mambo mengine, hii inatokana na kuimarika kwa upatikanaji wa miundombinu, hususan, nishati na usafiri.

Wastani wa Pato la Kila Mtu

16.     Mheshimiwa Spika, Pato la Taifa kwa mwaka 2016 lilifikia Shilingi milioni 103,744,606 (kwa bei za mwaka husika). Kiasi hiki cha Pato kikigawiwa kwa idadi ya watu wanaokadiriwa kuwepo Tanzania Bara, ya watu 48,676,698, inafanya wastani wa Pato la kila mtu kufikia Shilingi 2,131,299 ikilinganishwa na wastani wa Shilingi 1,918,897 mwaka 2015, sawa na ongezeko la asilimia 11.1. Hata hivyo, katika thamani ya Dola za Marekani, wastani wa Pato la kila mtu liliongezeka kidogo kutoka Dola 967.5 mwaka 2015 hadi Dola 979.1 mwaka 2016, ikimaanisha kuwa bado kuna hatua ili kuingia katika kundi la uchumi wa kati. Kiwango cha chini cha uchumi wa kati ni kufikia Dola 1,043. Hivyo basi, kasi ya ongezeko la Pato la mwananchi katika thamani ya Dola haina budi kuongezeka. Hii itawezekana kwa kutanzua changamoto zilizopo hususan, uzalishaji na tija katika sekta zinazoajiri wananchi wengi hasa kilimo cha mazao, ufugaji na uvuvi.

Mwenendo wa Bei

17.     Mheshimiwa Spika, Kwa miaka minne mfululizo, wastani wa mfumuko wa bei nchini umeendelea kupungua, ukibaki katika kiwango cha tarakimu moja. Kwa mwaka 2016, mfumuko wa bei ulifikia wastani wa asilimia 5.2 ikilinganishwa na asilimia 5.6 mwaka 2015. Kupungua kwa wastani wa mfumuko wa bei nchini kulichangiwa kwa kiasi kikubwa na: mwenendo wa kushuka wa bei za mafuta ya petroli katika soko la dunia na nchini; kuimarika kwa upatikanaji wa vyakula nchini na hivyo wastani wa bei; na kuwepo kwa sera madhubuti za usimamizi wa bajeti na fedha. Mfumuko wa bei uliongezeka kidogo, ambapo ulifikia asilimia 6.4 mwezi Aprili 2017 lakini ukiwa ndani ya maoteo ya wastani wa tarakimu moja (asilimia 5 – 8) kwa mwaka 2017. Hali ya kuongezeka kwa mfumuko wa bei nchini ilichangiwa na hofu iliyotokana na kuchelewa kwa msimu wa mvua katika maeneo mengi nchini na hivyo kuwepo kwa taharuki ya kutokea upungufu wa chakula. Hata hivyo, maeneo mengi yamepata mvua ya kutosha na hivyo bei  ya chakula nchini inatarajiwa kuimarika.

18.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016 viwango vya riba za amana na mikopo vilipungua ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. Riba za amana za muda maalum zilipungua kutoka wastani wa asilimia 9.30 hadi asilimia 8.78. Viwango vya riba za amana za mwaka mmoja vilipungua kutoka wastani wa asilimia 11.16 mwaka 2015 hadi asilimia 11.03 mwaka 2016. Vile vile, viwango vya riba za mikopo ya hadi mwaka mmoja vilipungua kutoka wastani wa asilimia 14.22 kufikia asilimia 12.87 mwaka 2016. Mwenendo huu ulichangiwa na kuongezeka kwa ushindani wa kibenki. Kufuatia hali hiyo, tofauti kati ya riba za amana na mikopo ya mwaka mmoja ilipungua kufikia asilimia 1.83 mwaka 2016 ikilinganishwa na asilimia 3.06 mwaka 2015. Hata hivyo, riba ya mikopo baina ya benki iliongezeka kufikia wastani wa asilimia 13.49 mwezi Desemba 2016 kutoka asilimia 7.29 kwa muda kama huo mwaka 2015. Riba kwa dhamana za Serikali ilipungua kutoka asilimia 18.25 mwezi Desemba 2015 kufikia wastani wa asilimia 15.12 mwezi Desemba 2016.

19.     Mheshimiwa Spika, kufikia Machi 2017, riba za amana za muda maalum ziliongezeka kidogo kuwa asilimia 10.89; na riba za amana za mwaka mmoja kufikia asilimia 12.03. Wakati huo huo, riba za mikopo ya hadi mwaka mmoja ziliongezeka kufikia asilimia 18.07. Ongezeko hili la riba za mikopo katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2017 kunatokana na mabenki kuchukua tahadhari dhidi ya kuongezeka kwa makadirio ya mikopo chechefu na kupunguza maoteo ya faida. Kuongezeka kwa riba za amana kulichangiwa na kuongezeka kwa ushindani wa kibenki katika kuvutia amana. Kwa upande mwingine, riba za mikopo baina ya benki zilipungua kufikia wastani wa asilimia 8.16 na kwa dhamana za Serikali asilimia 14.52.

Amana katika Benki za Biashara
20.     Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2016, amana katika benki za biashara ziliongezeka kwa asilimia 2.3 kufikia shilingi bilioni 19,729.5 kutoka shilingi bilioni 19,293.7 mwaka 2015. Kati ya amana hizo, sekta binafsi ilichangia asilimia 97.1 ikilinganishwa na asilimia 95.6 mwaka 2015. Aidha, uwiano wa amana za fedha za kigeni katika amana zote ulipungua kufikia asilimia 31.6 mwaka 2016 kutoka asilimia 32.8 mwaka 2015. Katika kipindi cha Januari hadi Machi 2017, amana katika benki za biashara ziliongezeka kufikia shilingi bilioni 19,853.40, ambapo sekta binafsi ilichangia asilimia 96.4.

Mwenendo wa Mikopo kwa Sekta Binafsi
21.     Mheshimiwa Spika, mikopo ya mabenki kwa sekta binafsi kwa mwaka 2016 iliongezeka kwa asilimia 7.2 kufikia Shilingi bilioni 16,608.9 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 15,492.7 mwaka 2015. Ukuaji huu ulikuwa chini ya kiwango cha mwaka 2015 cha asilimia 24.8. Kiasi cha mikopo kilichotolewa kwa sekta binafsi mwaka 2016 kilifikia asilimia 16.2 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 17.1 mwaka 2015. Kiwango cha mikopo kilichotolewa kwa shughuli za uzalishaji; kilimo, uchukuzi na mawasiliano, viwanda, huduma za kifedha, umeme, majengo na ujenzi, kilipungua mwaka 2016 ikilinganishwa na mwaka 2015. Wakati huo huo, mikopo ya shughuli za madini na uchimbaji mawe, biashara, utalii, hoteli na migahawa na shughuli binafsi iliimarika, japo kwa kasi ndogo. Mikopo iliyoelekezwa katika shughuli za biashara, ilikuwa asilimia 21 ya mikopo yote na shughuli binafsi asilimia 18.6. Mwenendo huu ulichangiwa, kwa kiasi kikubwa, na kupungua kwa ukwasi katika mabenki kutokana na tahadhari zilizochukuliwa na mabenki kufuatia kuongezeka kwa makisio ya viwango vya mikopo chechefu na kupungua kwa maoteo ya faida.

22.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Januari hadi Machi 2017, mikopo ya benki za biashara kwa sekta binafsi iliendelea kuimarika, ikiongezeka kwa shilingi bilioni 77.4 kufikia shilingi bilioni 16,686.30. Hizi ni ishara njema za kuanza kuimarika kwa uchumi na shughuli za sekta binafsi hususan, za uzalishaji viwandani, majengo na mahoteli na mighahawa.

Ukuzaji Rasilimali
23.     Mheshimiwa Spika, Tanzania ni mojawapo wa nchi chache za Afrika zilizojipambanua kwa kuwa na utulivu wa uchumi jumla kwa muda mrefu sasa. Hii ikiwa ni pamoja na kuwa na kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi, mfumuko wa bei wa wastani na mwenendo wa thamani ya shilingi umekuwa thabiti. Hali hii imekuwa kishawishi kikubwa cha mitaji kutoka nje kuja nchini. Kwa mwaka 2016, ukuzaji rasilimali, kwa bei za miaka husika, uliongezeka kwa asilimia 3.4 kutoka shilingi milioni 24,717,206 mwaka 2015 hadi Shilingi milioni 25,558,140. Hata hivyo, uwiano wa ukuzaji rasilimali na Pato la Taifa, kwa bei za miaka husika, ulipungua kufikia asilimia 24.6 mwaka 2016 ikilinganishwa na asilimia 27.2 mwaka 2015. Kiwango cha ukuzaji rasilimali kwa bei za mwaka 2007, kilipungua kwa asilimia 4.3 kutoka Shilingi milioni 13,733,585 mwaka 2015 kufikia Shilingi milioni 13,140,451 mwaka 2016.

Sekta ya Nje

24.     Mheshimiwa Spika, Mwaka 2016, mwenendo wa biashara ya bidhaa na huduma kati ya Tanzania na nchi mbalimbali uliendelea vizuri. Thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nje iliongezeka kwa asilimia 4.1 kufikia dola za Marekani milioni 9,285.6 mwaka 2016 ikilinganishwa na Dola milioni 8,918.1 mwaka 2015. Aidha, uagizaji wa bidhaa na huduma nje ilipungua kwa asilimia 14.0 kwa mwaka 2016 kutoka Dola milioni 12,528.2 mwaka 2015 kufikia dola za Marekani milioni 10,772.3. Mwenendo huo ulitokana na kupungua kwa thamani ya bidhaa nyingi zilizoagizwa kutoka nje isipokuwa kwa malighafi za viwandani zilizoongezeka ikichangiwa pia na kupungua kwa gharama za usafirishaji, huduma zitolewazo na  Serikali, na huduma nyingine za kibiashara.

25.     Mheshimiwa Spika, Biashara kati ya Tanzania na nchi mbalimbali duniani ziliendelea kuimarika na masoko kubadilika, ambapo kwa mwaka 2016 sehemu kubwa ya mauzo yote nje ya nchi yalikwenda katika nchi za Uswisi (asilimia 16.2), India (asilimia 12.4), Afrika ya kusini (asilimia 12.2), China (asilimia 6.2), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (asilimia 5.6) na Kenya (asilimia 5.5). Hii inaonesha kuwa kumekuwa na mabadiliko kutoka masoko asilia, kama vile, Uingereza, Ujerumani na Canada. Bidhaa zilizouzwa kwa wingi nchini Uswisi na India ni pamoja na dhahabu, mbegu za mafuta, vito vya thamani na mbogamboga. Bidhaa zilizouzwa Kenya zilikuwa chai, mahindi, vifaa vya ushonaji, mbogamboga na nafaka. Vile vile, bidhaa zilizouzwa Afrika ya Kusini zilikuwa dhahabu, madini ya shaba na chai. Pamoja na maendeleo haya, mauzo mengi nje ya nchi yaliendelea kuwa ya mazao ghafi yasiyoongezwa thamani na hivyo kupata thamani ndogo.

26.     Mheshimiwa Spika, kwa upande wa bidhaa zilizoagizwa kutoka nje, kiasi kikubwa kilitoka katika nchi za China, India, Ufalme wa nchi za Kiarabu, Afrika ya Kusini, Japani na Kenya, nchi ambazo kwa pamoja zilichangia asilimia 60.6 ya bidhaa zote zilizoagizwa. Bidhaa zilizoagizwa kutoka China ni pamoja na mitambo na bidhaa za marumaru, kwa Ufalme wa nchi za Kiarabu ni mafuta ya petroli na sukari na kwa upande wa Japani na Afrika ya Kusini ni magari na bidhaa za chuma, kuonesha kuwa uzalishaji nchini bado unategemea vipuri, malighafi na mitambo kutoka nje.

27.     Mheshimiwa Spika, kufuatia mwenendo wa biashara kwa mwaka 2016, urari wa biashara ya bidhaa na huduma ulikuwa na nakisi ya Dola za Marekani milioni 1,489.5, ikipungua kwa asilimia 58.6 kutoka nakisi ya Dola za Marekani milioni 3,594.7 mwaka 2015. Hali hii kwa kiasi kikubwa, ilichangiwa na kuongezeka kwa mapato ya mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi na kupungua kwa uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi. Hivyo, urari wa malipo yote, kwa mwaka 2016, ukijumuisha urari wa biashara ya bidhaa na huduma, mapato ya vitega uchumi, uhamisho wa mali, malipo ya kawaida, uhamisho wa mitaji na malipo ya fedha katika uwekezaji, ulikuwa na ziada ya dola  za Marekani milioni 305.5 ikilinganishwa na nakisi ya dola za Marekani  milioni 199.1 mwaka 2015. Katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka 2017, thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nje ilifikia Dola za Marekani milioni 2,224.8, ikichangiwa, kwa kiasi kikubwa, na mauzo ya bidhaa asilia na zisizo asilia hasa huduma za utalii, dhahabu, bidhaa za mboga mboga na matunda. Aidha, katika kipindi hicho, uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ulikuwa Dola za Marekani milioni 2,203.6 na hivyo kuendelea kuwa na ziada katika urari wa akaunti ya biashara ya bidhaa na huduma.

Akiba ya Fedha za Kigeni na Thamani ya Shilingi
28.     Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Desemba 2016, akiba ya fedha za kigeni ilifikia Dola za Marekani milioni 4,325.6 ikilinganishwa na Dola milioni 4,093.7 Desemba 2015. Kiasi hicho kilikuwa kinaweza kulipia gharama za kununua bidhaa na huduma kutoka nje kwa miezi 4.2. Kufikia Machi 2017, akiba ya fedha za kigeni ilifikia Dola za Kimarekani milioni 4,482.6, kiasi kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa miezi 4.3. Kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni kumesaidia kurejesha utengamavu wa thamani ya shilingi. Katika kipindi cha mwaka 2016, mwenendo wa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani ulikuwa wa kuridhisha ukipungua kwa asilimia 8.8 tu ambapo dola moja ya Marekani ilinunuliwa kwa wastani wa Shilingi 2,177.07 ikilinganishwa na shilingi 1,991.4 mwaka 2015.. Hadi kufikia Machi 2017, dola moja ya Marekani ilinunuliwa kwa wastani wa shilingi 2,223.9 kutoka Shilingi 2,172.6 ilivyokuwa ikinunuliwa mwishoni mwa mwaka 2016.

Mabadiliko ya Maisha ya Watu
29.     Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Tanzania ina wastani wa ongezeko la watu la asilimia 2.7 kwa mwaka, ambapo kufikia mwaka 2016 ilikadiriwa kuwa na watu 48,676,698. Kwa makadirio haya, Tanzania inakuwa ni nchi ya tano kwa idadi ya watu Barani Afrika, ikitanguliwa na nchi nne (4) ambazo ni Nigeria, Ethiopia, Misri na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Idadi kubwa ya watu na kasi ya ongezeko imekuwa ni changamoto kubwa katika harakati za kupunguza umaskini na kuimarisha utoaji wa huduma. Kwa kuzingatia hali hii, Serikali imeendelea kuongeza na kuboresha upatikanaji wa elimu msingi hususan kwa wasichana. Kwa upande mwingine, idadi kubwa ya watu ni fursa pia kwa maana ya soko la bidhaa na huduma, ikiwa itaendana na maendeleo ya stadi, teknolojia, ujasiriamali na pato la kila mwananchi.

30.     Mheshimiwa Spika, licha ya hatua hizi, bado kumekuwa na changamoto nyingine kufuatia kasi kubwa ya uhamiaji mijini, ambapo kwa sasa, takribani asilimia 30 ya watu nchini wanaishi mijini. Kasi hii ya mabadiliko ya idadi ya watu na uhamiaji mijini inadunisha kasi ya  kuboresha upatikanaji wa nyumba na makazi yaliyopangwa  na pia utoaji wa huduma zinazoendana na idadi ya wakazi wa mijini. Katika kukabiliana na changamoto hizi, Serikali imeendelea kuimarisha upimaji wa maeneo ya makazi, ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na kuchukuwa hatua zinazolenga kuinua tija na faida katika shughuli za kilimo. Hatua hizo ni pamoja na kuimarisha upatikanaji wa huduma za ugani, pembejeo, zana za kilimo, masoko, miundombinu ya umwagiliaji, na kuondoa utitiri wa kodi katika shughuli za kilimo. Hatua pia zimeendelea kuchukuliwa kwa lengo la kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na uendeshaji wa shughuli za viwanda na biashara hasa vijijini. Lengo ni kupanua fursa za ajira mbadala kwa wakazi wa vijijini, ikiwa ndiyo njia ya kuaminika zaidi katika kudhibiti kasi ya watu kuhamia mijini. Huduma za mafunzo ya ufundi stadi zimezidi kuimarishwa ili wale wanaohamia mijini waweze kuajirika na kujiajiri kwa urahisi.

31.     Mheshimiwa Spika, kwa upande  wa ustawi wa jamii, maisha ya watu yameendelea kuboreka kama inavyothibitishwa na taarifa ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo ya Watu kwa mwaka 2016, ambapo kwa kigezo cha fahirisi ya maendeleo ya watu (HDI) ustawi wa watanzania umeendelea kuimarika kutoka alama 0.521 mwaka 2014 hadi alama 0.531 mwaka 2015. Kigezo hiki huzingatia viashiria kadhaa vya maendeleo na ustawi, hususan, muda wa kuishi baada ya kuzaliwa, elimu, na wastani wa kipato cha mwananchi. Kwa kutumia kigezo hiki Tanzania ni nchi ya pili kwa ustawi wa maisha ya wananchi katika Ukanda wa Afrika Mashariki baada ya Kenya iliyofikia alama 0.555 katika kipindi hiki.

32.     Mheshimiwa Spika, mafanikio ya Tanzania ni matokeo ya jitihada zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha upatikanaji wa huduma za jamii kama vile elimu, afya, maji safi na salama, na umeme katika maeneo ya vijijini na  mijini.  Mfano, idadi ya wananchi waliofikiwa na huduma ya umeme hadi Machi 2017 ilifikia asilimia 67.5 ikilinganishwa na asilimia 40 iliyokuwa imefikiwa Aprili, 2016. Kwa maeneo ya mijini, idadi ya wananchi waliopata umeme ilifikia asilimia 97.3 Machi 2017 ikilinganishwa na asilimia 63.4 mwaka 2014/15, na upande wa maeneo ya vijijini ilifikia asilimia 49.5 Machi 2017 ikilinganishwa na asilimia 21.0 mwaka 2014/15. Kwa upande wa upatikanaji wa maji, idadi iliongezeka kutoka watu 21,900,000 Juni 2016 hadi 22,951,371 Machi 2017. Kumekuwa na mafanikio pia kwa upande wa elimu, ambapo uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza uliongezeka kutoka milioni 1.5 mwaka 2014 hadi milioni 2.1 mwaka 2016. Vile vile, idadi ya wananchi wanaonufaika na huduma ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) imeongezeka kutoka 3,377,023 mwaka 2015/16 hadi 3,880,088 Machi 2017. Wanufaika wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) wameongezeka kutoka 8,717,130 mwaka 2015/16 hadi kufikia wanufaika 9,573,906 Machi 2017.

33.     Mheshimiwa Spika, pamoja na kupunguza umasikini wa mahitaji ya msingi, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kuwa idadi ya Watanzania wanaokosa mlo kwa siku au kuishi kwa mlo mmoja inapungua kutoka kiwango cha asilimia 9.7 kwa sasa kufikia asilimia 5.7 na 4.4 ifikapo mwaka 2020 na 2025, kwa mtiririko huo. Hatua zinazochukuliwa kufikia lengo hili ni pamoja na kuimarisha uzalishaji na hivyo upatikanaji wa chakula katika kaya; kuongeza fursa za ajira mijini na vijijini; kuendelea na mpango wa kusaidia kaya masikini; na kuwezesha upatikanaji wa mikopo nafuu kwa wajasiriamali kupitia mifuko ya maendeleo ya vijana, wanawake na wajasiriamali wadogo.

34.     Mheshimiwa Spika, licha ya mafanikio yaliyofikiwa, kiwango cha umaskini kwa maeneo ya vijijini bado ni kikubwa ikilinganishwa na maeneo ya mijini. Umaskini vijijini umepungua kutoka asilimia 39.4 mwaka 2007 hadi asilimia 33.3 mwaka 2012 ikimaanisha kuwa japo vijijini umaskini unapungua lakini bado ni chini ya wastani wa kitaifa. Mantiki yake ni kuwa kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi haijaligusa kundi kubwa la wananchi wa vijijini, ambao wengi wao hutegemea shughuli za kilimo, ufugaji na uvuvi. Sekta hizi, ambazo ndizo msingi wa ustawi wa maisha ya watu wa vijijini, zimekuwa na tija na kasi ndogo ya ukuaji kwa kipindi chote. Shabaha ya Serikali ni kupunguza wastani wa umaskini vijijini kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 33.3 hadi kufikia asilimia 19.7 na 15 mwaka 2020 na mwaka 2025, kwa mtiririko huo.

35.     Mheshimiwa Spika, kipimo cha mgawanyo wa kipato miongoni mwa wananchi (Gini coefficient) kwa upande wa Tanzania Bara kinaonesha kuwa tofauti ya kipato imepungua kutoka 0.37 mwaka 2006/7 hadi 0.34 mwaka 2011/12. Hata hivyo, tofauti ya kipato kati ya jiji la Dar es Salaam na maeneo ya miji mingine na ile ya maeneo ya vijijini ni kubwa zaidi. Hali hii imechangiwa na tofauti ya upatikanaji wa huduma, miundombinu, fursa za ajira, athari za mazingira na mabadiliko ya tabia nchi katika shughuli msingi za jamii husika.

36.     Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania 2015/16, vifo vya watoto wachanga chini ya mwaka mmoja vimepungua kutoka 51 kwa vizazi hai 1,000 mwaka 2010 hadi 43 kwa vizazi hai 1,000 mwaka 2015/16, vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kutoka 81 kwa vizazi hai 1,000 mwaka 2010 hadi vifo 67 kwa vizazi hai 1,000 mwaka 2015/16. Kushuka kwa viashiria hivi kunatokana na kuimarika kwa upatikanaji wa huduma za msingi za kijamii ikiwemo afya ya uzazi na mama na mtoto nchini.

37.     Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu hali ya uchumi yapo katika kitabu cha Hali ya Uchumi kwa mwaka 2016.

UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2016/17

Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo 2016/17
38.     Mheshimiwa Spika, mwaka 2016/17 ulikuwa mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Mpango huu utatekelezwa hadi 2020/21, ambapo msukumo ni kuchochea mageuzi ya uchumi kupitia ujenzi wa uchumi wa viwanda na kufungamanisha maendeleo ya uchumi na maendeleo ya watu. Kwa kuzingatia hili, Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2016/17 ulijielekeza katika maeneo makuu manne ya kipaumbele, ikiwa ni:-
     (i)    Kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda;
    (ii)    Kufungamanisha uchumi na maendeleo ya watu;
  (iii)    Kujenga mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji; na
  (iv)    Kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa Mpango.

39.     Mheshimiwa Spika, mapitio ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa 2016/17 yamefafanuliwa kwa kina katika hotuba za mipango na bajeti za Mawaziri wa sekta husika. Kwa maana hiyo nitajikita kuelezea hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa baadhi tu ya miradi ya maendeleo kwa mwaka 2016/17.

Miradi Iliyopewa Msukumo wa Kipekee:
40.     Mheshimiwa Spika, Hii ni miongoni mwa miradi ya kimkakati iliyobainishwa kwa utekelezaji katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano, 2016/17 – 2020/21. Utekelezaji wa miradi hiyo ni kama ifuatavyo:
(i)        Ujenzi wa Reli ya Kati: kusainiwa kwa mkataba wa kusanifu na kujenga awamu ya kwanza ya mradi kutoka Dar es Salaam – Morogoro (Km 205) ambapo mkandarasi ameanza maandalizi ya ujenzi ikiwemo ujenzi wa kambi, ofisi pamoja na kiwanda cha kukarabati mataruma. Mkandarasi amelipwa Shilingi bilioni 300 malipo ya awali (advance payment) na Mheshimiwa Rais alizindua kazi ya ujenzi tarehe 12 Aprili 2017. Taratibu zinazoendelea ni kupata fedha na kuendelea na ujenzi sehemu za reli zilizobakia. Kwa sehemu ya Morogoro hadi Makutupora (Km 336), Serikali inaendelea na mazungumzo na Mkandarasi aliyepatikana; na kwa sehemu za Makutupora hadi Tabora (Km 294), Tabora hadi Isaka (Km 133) na Isaka hadi Mwanza (Km 249), Serikali ipo kwenye mazungumzo na baadhi ya mabenki ambayo yameonesha nia ya kutoa mkopo nafuu wa benki kwa ajili ya ujenzi.

(ii)      Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania: Ndege mbili (2) zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja zilinunuliwa na zilianza kutoa huduma tangu Oktoba 2016. Vile vile, maandalizi ya ununuzi wa ndege nyingine 4 yamekamilika na mikataba imesainiwa, ambapo malipo ya awali ya kiasi cha Dola za Marekani milioni 56.89 tayari yamefanyika. Kati ya ndege hizo, moja inategemewa kuwasili Julai 2017; mbili zinategemewa kuwasili Juni 2018, na ya mwisho, ambayo itakuwa ya masafa marefu yenye uwezo wa kubeba abiria 262 inategemewa kuwasili Julai 2018.

(iii)    Makaa ya Mawe Mchuchuma na Chuma Liganga: maandalizi yote ya ujenzi wa miradi hii yamekamilika, ikiwa ni pamoja na kutenga fedha kwa ajili ya malipo ya fidia kwa wananchi watakaopisha mradi. Vile vile, kampuni ya Sichuan Hongda (Group) Corporation Ltd, ambayo ndio mbia katika miradi hii, wametenga jumla ya Dola za Kimarekani milioni 300 kwa ajili ya kulipia sehemu ya mtaji (equity) wao katika miradi. Mfumo uliokubalika na pande zote mbili ni mwekezaji kujenga mtambo wa kufua umeme, kumiliki na kuuendesha (Build Own and Operate, BOO). Mauziano ya umeme kwa TANESCO hayatajumuisha gharama za uwekezaji.

(iv)    Mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima Uganda – Bandari ya Tanga
Hatua iliyofikiwa ni pamoja na: kusainiwa kwa mkataba wa makubaliano ya awali; kutolewa kwa vivutio vya kodi; kusainiwa kwa Inter- Govermental Agreement; kufanyika kwa tathmini ya njia ya bomba; kufanyika kwa tathmini ya  mahitaji ya njia ya bomba; kufanyika tathmini ya masuala ya kijamii na mazingira; kufanyika kwa upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa gati ya kupokelea mafuta – Chongoleani katika bandari ya Tanga; na kutangazwa kwa zabuni za kuwapata wataalam elekezi kwa ajili ya uchunguzi wa udongo.
(v)      Ununuzi na Ukarabati wa Meli kwenye Maziwa Makuu: Hatua iliyofikiwa ni kuendelea na taratibu za ununuzi kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya kwa ajili ya usafirishaji wa abiria na mizigo katika ziwa Victoria na ukarabati mkubwa wa Mv. Victoria na Mv. Butiama. Kwa upande wa Mv. Liemba katika ziwa Tanganyika, mjenzi amepatikana ambaye ni M/S LEDA SHIPYARD. Ujenzi wa meli mbili za mizigo ziwa Nyasa umekamilika.

(vi)    Uanzishwaji wa Shamba la Miwa na Kiwanda cha Sukari Mkulazi: Shilingi Billioni 2 tayari zimewekezwa katika mradi huu. Kazi zilizofanyika ni: kupima ubora wa udongo; vitalu vya mbegu za miwa vimeandaliwa; na taratibu za kupata huduma ya wataalam wa kufanya upembuzi yakinifu, uchunguzi wa mbegu za miwa, tathmini ya athari za mazingira na ujenzi wa barabara za kuingia katika eneo la mradi zinaendelea.

(vii)  Ujenzi wa Mitambo ya Kusindika Gesi Kimiminika: Hatua iliyofikiwa ni pamoja na: kupatikana kwa eneo la mradi Likong’o mkoani Lindi; kuundwa kwa timu ya majadiliano na kuandaliwa kwa hadidu za rejea, kupitia nyaraka muhimu zinazohusu mradi (sera, sheria, mikataba, kanuni na mikakati ya Serikali); na kuanza kwa majadiliano na kampuni zinazoshiriki katika mradi juu ya masuala yatakayozingatiwa katika kuandaa mkataba kati ya kampuni husika na Serikali (Host Government Agreement – HGA).

(viii)                Uendelezaji wa Maeneo Maalum ya Kiuchumi
a.  Kituo cha Biashara cha Kurasini: kiasi cha fidia kilicholipwa kwa ajili ya kupata eneo la mradi ni Shilingi bilioni 101.04 na wananchi 1,019 tayari wamelipwa fidia. Eneo hili kwa sasa lipo chini ya umiliki wa Serikali kwa asilimia 100 na hivyo maandalizi ya mpango mahsusi wa uwekezaji katika eneo hilo yanaendelea.
b.  Eneo Maalum la Uwekezaji la Bagamoyo: Shilingi bilioni 26.66 zimetumika kulipa fidia kwa wananchi 1,155 kati ya 2,273 wanaopaswa kupisha mradi kwenye eneo la hekta 2,339.6.
c.  Eneo Maalum la Uwekezaji la Mtwara: Tayari eneo la hekta 10 kati ya hekta 110 za eneo lililotengwa kwa ajili ya Mtwara SEZ limetangazwa kwa ajili ya matumizi ya bandari huru (Freeport Zone) na maandalizi ya kuweka miundombinu, hususan barabara, kwa eneo hilo yanaendelea.

Kujenga Msingi wa Uchumi wa Viwanda
41.     Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma ya kujenga uchumi wa viwanda, mwelekeo umeanza kuwa vizuri. Miradi ya viwanda mbalimbali imeanzishwa kutokana na mchango wa sekta binafsi katika mikoa mbalimbali nchini, kwa mfano kwa mkoa wa Pwani una jumla ya miradi mipya ya viwanda 82. Aidha, baadhi ya miradi mikubwa ya viwanda iliyozinduliwa na kuwekwa mawe ya msingi kwa mkoa wa Pwani pekee ni pamoja na:- viwanda viwili vya Tywford Tiles (Chalinze) na Goodwill Ceramic (Mkuranga) vya kutengeza marumaru (tiles); kiwanda cha nondo cha Kiluwa Steel Industries Ltd (Mlandizi Pwani) ambacho kimeanza uzalishaji; kiwanda cha Global Packaging (Mailimoja Pwani) ambacho kinafanya kazi; kiwanda cha kutengeneza juisi ya matunda cha Bakhresa Food Product Ltd (Mkuranga) ambacho kimezinduliwa na kinafanya kazi; kiwanda cha Elyven Agric Co. Ltd (Bagamoyo); kiwanda cha Juisi cha Sayona Fruits Ltd (Mboga Pwani); na kiwanda cha KEDS Tanzania Co. Ltd (Kibaha Pwani).

42.     Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa na mchango mkubwa kuwezesha sekta binafsi kuwekeza katika viwanda hivi, ikiwa ni pamoja na kusaidia upatikanaji wa ardhi, kuweka miundombinu inayohitajika, na kutoa vibali vya ujenzi na pia vivutio. Halmashauri na Serikali za Mitaa katika maeneo haya zimekuwa na msaada na ushirikiano mkubwa kwa wawekezaji ikiwemo kutoa maeneo ya viwanda ili kuhamasisha uwekezaji. Mathalan, Maswa wameanzisha kiwanda cha kuzalisha Chaki cha Maswa Youth Enterprises Ltd kwa utaratibu huo. Nitumie fursa hii kuwapongeza kwa dhati viongozi wa mikoa, wilaya, halmashauri na Serikali za Mitaa walioitikia kwa dhati wito wa Serikali kujielekeza katika kuvutia na kuwezesha uwekezaji. Niwatake pia viongozi wa Halmashauri zote nchini kuiga mfano wa wenzao wanaofanya jitihada zote katika kuhakikisha kuwa Halmashauri zinaandaa mazingira mazuri na maeneo ya uwekezaji kwa ajili ya sekta binafsi.

43.     Mheshimiwa Spika, Serikali pia kupitia mashirika yake mbalimbali imeanza kuwekeza katika ujenzi wa viwanda, mwitiko wa pekee na wa kupongezwa ni wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, ambapo PPF na NSSF wanashirikiana kuwekeza katika kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari katika eneo la Mkulazi na Mbigiri (Morogoro); na LAPF wanajenga machinjio ya kisasa ya nyama (kwa Makunganya – Morogoro). Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) linashirikiana na sekta binafsi kwa ajili ya uwekezaji katika eneo la viwanda la TAMCO – Kibaha kwa uendelezaji wa viwanda vya nguo na uunganishaji wa magari na matrekta, ambapo kiwanda cha kuunganisha matrekta kimefikia hatua ya kuanza majaribio. Hatua nyingine zinazoendelea chini ya NDC ni pamoja na jitihada za kufufua Kiwanda cha General Tyre (Arusha); hatua za awali za uwekezaji katika mradi wa uchenjuaji wa Magadi Soda (Bonde la Engaruka). NDC pia kwa ubia na kampuni ya TCIMRL ya China imewekeza katika miradi ya Mchuchuma na Liganga.

Ujenzi wa Miundombinu na Mazingira Wezeshi
44.     Mheshimiwa Spika, ujenzi wa uchumi wa viwanda unahitaji miundombinu ya uhakika. Hivyo, Serikali imeendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kuimarisha na kuboresha miundombinu na huduma za uchumi wa viwanda. Miongoni mwa miradi hii ni: ujenzi wa mtambo wa kufua umeme wa Kinyerezi II (MW 240); upanuzi wa mtambo wa kufua umeme wa Kinyerezi I (MW 185); ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kV 400 Iringa – Singida - Shinyanga (km 670), kV 220 Makambako – Songea (km 250), na North West Grid kV 400 (Mbeya – Sumbawanga – Mpanda - Kigoma – Nyakanazi km 1,148); usambazaji umeme Vijijini na Makao Mkuu ya Wilaya (REA Turnkey Phase III), ambapo wateja 146,831 sawa na asilimia 58.7 ya lengo wameunganishwa; na ukarabati wa njia ya reli ya kati. Kwa upande wa barabara hatua iliyofikiwa ni kukamilika kwa ujenzi wa barabara za Masasi – Songea – Mbambabay, sehemu ya Namtumbo – Tunduru (km 193), na Tunduru – Mangaka – Mtambaswala (km 202.5); barabara ya Dodoma – Babati (km 261); Bagamoyo – Msata na daraja la Ruvu chini; na kukamilika kwa Daraja la Kilombero katika barabara ya Ifakara – Mahenge. Ujenzi wa barabara ya Kidahwe – Kasulu – Kibondo – Nyakanazi unaendelea na umefikia asilimia 16.4; na ujenzi wa barabara za juu za TAZARA na Interchange ya Ubungo umeanza.

Kufungamanisha Ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya Watu
45.     Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu Serikali inaendelea kutekeleza sera ya elimumsingi bila malipo; uboreshaji wa miundombinu na huduma za kujifunzia na kufundishia; kukamilika kwa ujenzi wa mabweni katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; kutoa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; kukamilika kwa ujenzi wa Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Kampasi ya Mloganzila; na kukamilika kwa ukarabati wa vyuo vya ualimu kumi. Katika kuimarisha ujuzi na stadi za kazi, Serikali imekamilisha matayarisho ya Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2017, Miongozo ya Mafunzo Kazini kwa vitendo kwa wanafunzi (Apprenticeship Framework) na mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu (Internship Framework). Vile vile, Serikali imeingia mikataba na viwanda vya TOOKU Garment na Mazava Fabrics kwa ajili ya kutoa mafunzo ya stadi za ubunifu na ushonaji wa nguo viwandani. Maeneo mengine yaliyozingatiwa ni pamoja na kupanua miundombinu ya upatikanaji wa maji safi na salama mijini na vijijini; huduma za afya na upimaji wa maeneo ya makazi.

46.     Mheshimiwa Spika, maeneo mengine yaliyoendelea kutekelezwa ni yale yaliyotoa fursa za ajira na ushiriki wa wananchi wengi katika shughuli za uchumi wa viwanda, ikiwa ni pamoja na: kuandaliwa kwa program ya muda mrefu na mfupi ya upimaji na umilikishaji wa ardhi hususan kwa matumizi ya kilimo; kukamilika kwa ukarabati wa maghala 106 katika Halmashauri za Wilaya za Iringa, Mufindi, Mbeya, Songea, Kalambo, Mbozi, Momba na Njombe; na kuingizwa nchini kwa tani 231,140 za mbolea.

47.     Mheshimiwa Spika, katika kuhamishia Shughuli za Serikali Kuu Dodoma: awamu ya kwanza imekamilika ambapo majengo ya ofisi za wizara katika kipindi cha mpito na nyumba za makazi kwa baadhi ya viongozi zimepatikana. TBA na Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma wanaendelea na kukamilisha ukarabati wa nyumba za makazi na ofisi. Vile vile, Serikali kwa kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma inaendelea na upimaji wa viwanja vya makazi na ofisi, ambapo watumishi wa Umma wameandaliwa mkakati maalum utakaosaidia upatikanaji wa viwanja kwa ajili ya makazi. Aidha, Shirika la Nyumba la Taifa linaendelea na ujenzi wa nyumba mpya 300 za makazi na zinazotarajiwa kukamilika Septemba, 2017. Kwa upande mwingine, Serikali inaendelea na mazungumzo na kampuni binafsi kutoka Switzerland, China na Zimbabwe na pia ya ndani ambayo yameonesha nia ya kushiriki katika ujenzi wa miundombinu ya maji kwa mji mpya wa Dodoma. Taasisi za Serikali kama vile TBA, TANESCO, SUMATRA, TEMESA, TANROADS, TTCL na Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma zimekamilisha maandalizi ya awali ya kuboresha miundombinu muhimu inayohitajika kuwezesha uendeshaji wa Serikali bila vikwazo katika kipindi hiki.

Utekelezaji wa Bajeti ya Maendeleo
48.     Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2016/17 Serikali ilipanga kutumia Shilingi bilioni 11,820.503 kwa ajili ya bajeti ya maendeleo, ambapo, Shilingi bilioni 8,702.697 zilikuwa za ndani na bilioni 3,117.805 za nje. Hadi Aprili 2017, fedha zilizokuwa zimetolewa ni Shilingi bilioni 4,516.7, sawa na asilimia 38 ya bajeti ya maendeleo, ikijumuisha fedha zilizotolewa kwa Halmashauri. Fedha za maendeleo zilizotolewa zinajumuisha Shilingi bilioni 3,608.9 fedha za ndani na Shilingi bilioni 907.8 fedha za nje. Kwa ujumla kiasi cha fedha kilichotolewa ni chini ya maoteo ya mtiririko wa fedha kwa wakati husika. hii ilichangiwa na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuchelewa kupatikana kwa misaada na mikopo ya kibiashara kufuatia majadiliano na Washirika wa Maendeleo na mabenki kuchukua muda mrefu, kupanda kwa riba ya mikopo ya kibiashara katika soko la fedha kimataifa hivyo Serikali kufikia maamuzi ya kuahirisha kuchukua mikopo husika. Hata hivyo, miradi ambayo ina vyanzo vya fedha mahsusi kama vile Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Mfuko wa Barabara, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Mfuko wa Maji na Mfuko wa Reli ilipatiwa fedha zote zilizokusanywa katika kipindi husika.

49.     Mheshimiwa Spika, Mikakati mbalimbali imewekwa kuhakikisha fedha zilizopangwa kwa ajili ya matumizi ya miradi ya maendeleo zinapatikana kwa kiasi cha kuridhisha. Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kuendelea na majadiliano baina ya Serikali na Washirika wa Maendeleo ili kuhakikisha fedha za misaada na mikopo nafuu zinapatikana kama zilivyoahidiwa; kuimarisha makusanyo ya ndani ya Serikali; na kuendelea kuboresha mazingira ya uendeshaji biashara ili kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi nchini. Aidha, Serikali ipo katika hatua za mwisho za majadiliano na benki ya Credit Suisse ili kupata mkopo wa Dola za Marekani Milioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Changamoto za Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya 2016/17
50.     Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya mwaka 2016/17 umekabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na mwenendo wa upatikanaji wa fedha, upatikanaji wa maeneo ya uwekezaji na matayarisho hafifu ya miradi ambapo kwa baadhi ilionekana bayana kuwa ama ipitiwe upya au majadiliano yaanze upya ili kulinda maslahi ya Taifa.

(i)      Mwenendo wa Upatikanaji wa Fedha: Kwa upande wa upatikanaji wa fedha kutoka makusanyo ya mapato ya ndani, haya yamekuwa yakiongezeka na yamekuwa yakipatikana kwa wakati. Kumekuwepo na kuchelewa kupatikana kwa mikopo yenye masharti nafuu na ya kibiashara kutoka nje; na Majadiliano kuchukua muda mrefu hivyo kuchelewa kupatikana kwa fedha za kuelekeza baadhi ya miradi ya maendeleo.

Kumekuwa na kuchelewa kwa ukamilishaji wa taratibu za kufikia maafikiano na wakopeshaji, hivyo, mikopo kuchelewa kupatikana. Katika mwaka 2016/17, kwa makusudi kabisa, ilionekana ipo haja ya kusitisha mchakato wa kukopa baada ya riba za mabenki duniani kupanda sana kufikia wastani wa asilimia 9 kutoka asilimia 6.

Zipo hatua mbalimbali zilizochukuliwa kukabiliana na changamoto hii. Pamoja na kuzidi kuimarisha makusanyo ya ndani ya Serikali, msisitizo ni kuhakikisha kuwa fedha zinazopatikana zinaelekezwa kwenye miradi yenye tija; kuendelea kuboresha mazingira ya uendeshaji biashara ili kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi nchini, ikiwa ni pamoja na wawekezaji wadogo hususan upatikanaji wa mikopo nafuu na maeneo ya uwekezaji na pia kuhuisha sheria, kanuni, taratibu na kupunguza ada, kodi na tozo za uwekezaji na uendeshaji biashara. Aidha, Serikali inaendelea na majadiliano na baadhi ya taasisi za fedha na mabenki ili kupata mkopo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

(ii)    Upatikanaji wa Maeneo ya Uwekezaji: Baadhi ya miradi imekuwa na utekelezaji hafifu kutokana na kuwepo migogoro ya ardhi na kutokamilika kwa hatua za kulipa fidia. Uhakiki umeonesha kuwepo kwa udanganyifu katika gharama na watu wanaostahili kulipwa fidia katika maeneo mengine. Hali hii ililazimisha madai kupitiwa upya  na hivyo kuchelewa kuanza kwa utekelezaji. Hatua zilizochukuliwa na Serikali ni kuongeza kasi ya kupata Maeneo Maalum ya Uwekezaji (EPZ na SEZ) na maeneo ya viwanda kwa ngazi zote za mikoa. Halmashauri zote zimeagizwa na tayari baadhi zimetenga maeneo ya viwanda na biashara ndogo ndogo. Vile vile, mashirika ya umma yenye ardhi kama vile NDC yametumia maeneo hayo kuingia ubia na wawekezaji binafsi.

(iii)  Mapungufu katika Maandalizi ya Miradi: Serikali katika hatua za kuimarisha maandalizi ya miradi, ambapo imeandaa na kuweka utaratibu wa maofisa kutumia kikamilifu Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma. Pamoja na kuandaa Mwongozo huo, Serikali imechukua hatua ya kutoa mafunzo kwa wataalam 422 wanaohusika na uratibu wa miradi ya maendeleo kwa Mikoa na Halmashauri zote pamoja na Wizara, Taasisi, Idara Zinazojitegemea na Wakala wa Serikali.

51.     Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo yapo katika kitabu cha Mpango (Sura ya Tatu).


MPANGO WA MAENDELEO WA MWAKA 2017/18
Mazingira Yanayoongoza Mpango
52.     Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/18 ni wa pili katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21). Msukumo wake ni kufanikisha utekelezaji wa malengo ya Mpango wa Miaka mitano hasa kwa miradi ambayo utekelezaji wake unaendelea tokea 2016/17.

53.     Mheshimiwa Spika, utayarishaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/18 umezingatia yafuatayo kama mwongozo: Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17 - 2020/21); sera na mikakati mbalimbali ya kisekta, kikanda (EAC na SADC) na Umoja wa Afrika; Agenda ya 2030 ya Malengo ya Maendeleo Endelevu; Agenda ya 2063 ya Maendeleo ya Afrika; na Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Vile vile, umezingatia mwenendo wa uchumi wa Taifa, kikanda na kidunia kwa mwaka 2016 na maoteo kwa mwaka 2017. Umezingatia pia hali halisi ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2016/17 na changamoto za utekelezaji zilizojitokeza.

Ushirikishwaji wa Jamii katika Maandalizi ya Mpango
54.     Mheshimiwa Spika, mchakato wa maandalizi ya Mpango huu umezingatia dhana ya ushirikishi mpana wa wadau ikiwa ni pamoja na Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Taasisi za Serikali, Taasisi za Utafiti na Elimu ya Juu, Sekta Binafsi na Washirika wa Maendeleo. Pia uliweza kupata maoni ya Waheshimiwa Wabunge katika mkutano wa Tano wa Bunge la 11 kuhusu Mapendekezo ya Serikali kwa Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2017/18. Katika mkutano tajwa, waheshimiwa wabunge walitoa maoni na mchango mkubwa uliotuwezesha kuandaa Mpango huu. Miongoni mwa maoni mahsusi ya Waheshimiwa Wabunge ni kuwa: Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha standard gauge upewe kipaumbele; kuboresha mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara; utekelezaji wa mkakati wa kujenga zahanati katika kila kijiji na vituo vya afya kila kata; kuimarisha upatikanaji wa madawa na vifaa tiba; kuendeleza maeneo ya viwanda vidogo, na maeneo mahsusi ya EPZ/SEZ; kutoa kipaumbele kwa utekelezaji wa miradi ya makaa ya mawe - Mchuchuma na chuma - Liganga; kuboresha elimu ya juu na kuongeza wigo wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi; kuboresha miundombinu ya barabara; na programu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

55.     Mheshimiwa Spika, maoni na ushauri wa wadau wengine ambao umezingatiwa katika maandalizi ya Mpango huu ni pamoja na: Kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mpango; upatikanaji wa mikopo ya muda mrefu na nafuu; uimarishwaji wa miundombinu msingi ya bandari na nishati ya umeme; na kuboresha utoaji wa huduma msingi za ustawi wa jamii hususan elimu, afya, maji, uboreshaji wa mipango miji, nyumba na makazi, na utunzaji wa mazingira.

Shabaha na Malengo ya Uchumi Jumla kwa mwaka 2017/18
56.     Mheshimiwa Spika, Shabaha na malengo ya uchumi jumla katika kipindi cha mwaka 2017/18 ni kama ifuatavyo:-
(i)         Kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 7.1 mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2016;
(ii)        Kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja;
(iii)      Kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani (ikijumuisha ya Serikali kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa) kufikia asilimia 16.5 ya Pato la Taifa;
(iv)      Mapato ya kodi kufikia asilimia 14.2 ya Pato la Taifa mwaka 2017/18;
(v)        Matumizi ya Serikali kufikia asilimia 24.9 ya Pato la Taifa;

(vi)      Kuwa na nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) ya asilimia 3.8 ya Pato la Taifa;
(vii)    Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango kinachokidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne (4); na
(viii)   Kuhakikisha utulivu wa thamani ya Shilingi ya Tanzania.

Maeneo ya Kipaumbele 2017/18

57.     Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia shabaha na malengo haya, miradi iliyobainishwa kuwa ya kipaumbele kwa Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2017/18 ni ile inayotarajiwa kutoa matokeo makubwa kuendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mpango wenyewe. Mingi ya miradi hii utekelezaji wake ulianza mwaka 2016/17, hivyo inaendelea. Hii ni pamoja na miradi ya: ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha Standard Gauge; Kuhuisha Shirika la Ndege Tanzania, hususan kukamilisha malipo ya ununuzi wa ndege 4; miradi ya Chuma cha Liganga na Makaa ya Mawe ya Mchuchuma; Uanzishwaji/Uendelezaji wa Kanda Maalum za Kiuchumi; Mtambo wa Kuchakata Gesi Asilia - Lindi; na Shamba la Kilimo na Uzalishaji Sukari Mkulazi. Malengo ya utekelezaji kwa maeneo haya kwa mwaka 2017/18 yameainishwa katika kitabu cha Mpango wa Maendeleo kwa Mwaka 2017/18 (Sura ya nne).

58.     Mheshimiwa Spika, miradi mingine ya kipaumbele  itakuwa katika maeneo yafuatayo:
(a)     Ujenzi wa Msingi wa Uchumi wa Viwanda: ikihusisha miradi ya:- Uendelezaji wa Eneo la Viwanda TAMCO - Kibaha; Tathmini ya matumizi ya eneo la Kiwanda cha General Tyre – Arusha; Mradi wa Magadi Soda – Bonde la Engaruka, Arusha; kuimarisha Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Wajasiriamali (NEDF); uendelezaji wa maeneo ya viwanda vidogo katika mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Kigoma na Mtwara; ujenzi wa ofisi za SIDO katika mikoa mipya. Maeneo mengine ni pamoja na kuendeleza viwanda vya ngozi, kupanua mnyororo wa thamani wa pamba hadi nguo na uzalishaji wa madawa na vifaa tiba nchini. Kwa lengo hili, Serikali itaendelea kuhamasisha uwekezaji binafsi hususan katika viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana kwa wingi nchini ikiwa ni pamoja na viwanda vya kusindika nyama, maziwa, maji, misitu, chokaa, mawe urembo, gypsum na mazao ya vyakula na matunda. Serikali itaendelea kuziimarisha taasisi zake ili kuwekeza katika viwanda kwa njia ya PPP.

(b)     Kufungamanisha Ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya Watu: Miradi katika eneo hili ni ile inayolenga kuimarisha upatikanaji wa fursa za: Elimu na Mafunzo ya Ufundi: Kugharamia Elimumsingi bila malipo; Kupanua ruzuku na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu; Ununuzi wa vifaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum; ukarabati na upanuzi wa Maktaba ya Mkoa – Dodoma; na ujenzi wa Vyuo vitano vya VETA katika Mikoa ya Geita, Simiyu, Njombe, Rukwa na Kagera. Kwa upande wa Afya na Maendeleo ya Jamii ni: hatua zitaendelezwa za kuboresha Hospitali za Rufaa na mikoa; kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kisasa; kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi katika hospitali, vituo vya afya na zahanati; kuongeza udhibiti wa magonjwa ya kuambikiza; na kudhibiti maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI, hususan kwa vijana. Miradi ya Maji: ukarabati na upanuzi wa huduma za maji Vijijini; kuboresha huduma za maji katika Jiji la Dar es Salaam; mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Kahama, Nzega, Igunga, Tabora hadi Sikonge; ujenzi, ukarabati na upanuzi wa huduma za maji mijini na vijijini; na kutoa maji mto Ruvuma kwenda Manispaa ya Mtwara-Mikindani; kujenga na kuimarisha hifadhi ya vyanzo vya maji na misitu, upandaji miti, uvunaji wa maji, kuhimiza matumizi ya teknolojia jadidifu na hifadhi ya mazingira. Hatua nyingine ni pamoja na kupanua upatikanaji wa maji safi, utunzaji wa mazingira, na kuimarisha uhimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.

(c)      Mazingira Wezeshi kwa Uendeshaji Biashara: katika eneo hili, Serikali itaendelea na azma yake ya kupanua miundombinu ya huduma za kiuchumi kufikia azma yake ya kuboresha mazingira ya biashara ikihusisha miradi inayoendelea ya ukarabati wa miundombinu ya reli; miradi ya barabara na madaraja katika barabara za Kidahwe – Kasulu – Kibondo – Nyakanazi, Manyoni – Tabora – Uvinza, Tabora – Koga – Mpanda; Ujenzi wa barabara za juu za TAZARA na Ubungo Interchange; ujenzi wa Daraja la Selander na miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (awamu ya II, III na IV) jijini Dar es Salaam. Aidha, miradi ya bandari ikijumuisha bandari za Dar es Salaam, Mtwara, Tanga, Bagamoyo, bandari kavu ya Ruvu na bandari za Maziwa Makuu (Victoria, Tanganyika na Nyasa). Kwa upande wa usafiri wa anga, Serikali itaendelea na ujenzi wa jengo la abiria (terminal III) katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere; upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma, Tabora na Mwanza; ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Geita, Sumbawanga, Shinyanga, Mtwara, Musoma, Iringa na Songea; na ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro.

(d)     Kuimarisha Utekelezaji wa Mpango na Miradi: Serikali itaendelea kuchukua hatua ya kuimarisha mitaji ya benki za ndani za maendeleo (TIB na TADB) na kuanza utaratibu wa kuzitumia kama vyombo vyake vya ukusanyaji wa mikopo ya muda mrefu na ya gharama nafuu kwa wawekezaji. Aidha, eneo hili litajumuisha miradi ya kuendeleza na kusimamia matumizi ya ardhi; kuimarisha mipango miji; maendeleo ya nyumba na makazi; kuweka mfumo utakaowezesha nchi kufaidika na ushirikiano wa kikanda na kimataifa; kuimarisha utawala bora na utawala wa sheria.

Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuchochea ushiriki na maendeleo ya sekta binafsi, hususan, sekta binafsi ya ndani, katika utekelezaji wa Mpango na ujenzi wa viwanda. Serikali itaendelea kuboresha kanuni, taratibu na mifumo ya taasisi ya usimamizi wa biashara na uwekezaji nchini. Kwa kuzingatia hili, Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali, ikiwa ni pamoja na:

(i)       Kufanya mapitio ya sera, sheria na taratibu zinazochochea ushiriki wa sekta binafsi, ama kuwekeza moja kwa moja au kwa ubia na sekta ya umma;
(ii)      Kutenga maeneo ya uwekezaji ili kupunguzia sekta binafsi usumbufu hususan upatikanaji wa ardhi ikiwa ni pamoja na kutenga maeneo mahsusi ya uwekezaji (EPZ, SEZ na kuanzisha land bank chini ya TIC), na kuyawekea maeneo hayo miundombinu msingi, na kuikodisha kwa wawekezaji kwa gharama nafuu;
(iii)    Kujenga miundombinu wezeshi (barabara, umeme, maji na reli) na kuifikisha katika maeneo ya shughuli za wawekezaji;
(iv)    Kusimamia utekelezaji wa sheria na taratibu na kuhakikisha kuwepo kwa amani na usalama;
(v)      Kuimarisha mifuko maalum ya kuchochea ushiriki wa sekta binafsi, kwa mfano SAGCOT Catalytic Fund na PPP Facilitation Fund;
(vi)    Kuboresha huduma kwa wawekezaji, ikiwa ni pamoja na kuimarisha “one stop centre” chini ya TIC, bandari ya Dar es Salaam na vituo vya utoaji huduma ya pamoja mipakani (one stop border post); na
(vii)  Kuweka utaratibu utakaoboresha upatikanaji wa mikopo ya muda mrefu kwa gharama nafuu ikiwa ni pamoja na kuimarisha mitaji ya benki maalum za maendeleo (TADB) na (TIB).

(e)      Kuhamishia Makao Makuu ya Shughuli za Serikali Kuu Dodoma: katika mwaka 2017/18 Serikali itaendelea na utekelezaji wa azma ya kuhamishia shughuli za Serikali makao makuu Dodoma. Katika utekelezaji wa azma hii, Wizara zimeelekezwa kutenga fedha za kugharamia stahili za watumishi kwa kutumia ukomo wa bajeti uliotengwa kwenye mafungu yao. Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kuratibu upatikanaji wa maeneo ya kujenga ofisi na nyumba za viongozi wa Serikali kwa kuzingatia mahitaji na maboresho ya mpango wa ardhi katika mji wa Dodoma.

59.     Mheshimiwa Spika, kwa kuitikia wito wa Serikali wa kujenga uchumi wa viwanda, mifuko ya hifadhi ya jamii imeonesha nia ya kuwekeza katika miradi ya viwanda katika maeneo mbalimbali nchini. Baadhi ya miradi ambayo inatarajiwa kutekelezwa na mifuko hii katika mwaka 2017/18 ni pamoja na ufufuaji wa: kiwanda cha sukari katika Gereza la Mbigiri Dakawa Morogoro; kiwanda cha kutengeneza viatu katika Gereza la Karanga Moshi; kiwanda cha nguo cha urafiki; Dar Es Salaam; kiwanda cha Morogoro Canvas Mill; kiwanda cha chai cha Mponde kilichopo Lushoto Mkoani Tanga; kiwanda cha Kilimajaro Machine Tools, Kilimanjaro (KMTC) na kiwanda cha Kubangua Korosho cha Tandahimba na Newala. Vile vile, mifuko hii inatarajia kuanzisha viwanda vipya katika maeneo mbalimbali, vikiwemo: kiwanda cha dawa; kiwanda cha kuzalisha bidhaa za hospitali na gesi ya oksijeni; kiwanda cha kusindika zabibu, Chinangali Dodoma; viwanda vya kusindika nafaka na ukamuaji wa mafuta; na kiwanda cha kuzalishaji wanga kutokana na zao la muhogo na viazi vitamu huko Lindi.60.     Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu Miradi ya Kipaumbele yapo katika kitabu cha Mpango (Sura ya Nne).

61.     Mheshimiwa Spika, vipo vihatarishi mbalimbali ambavyo vinaweza kuathiri utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Vihatarishi hivyo vinaweza kuwa vya ndani au vya nje. Kihatarishi kikuu cha ndani ni ufinyu wa rasilimali fedha na uwepo wa tofauti za mpangilio wa vipaumbele, mpango-kazi na mtiririko wa upatikanaji fedha baina ya taasisi za utekelezaji. Vihatarishi vya nje ni pamoja na: mitikisiko ya kiuchumi kikanda na kimataifa; majanga asilia na athari za mabadiliko ya tabianchi; na mabadiliko ya kiteknolojia.

62.     Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau katika kutekeleza Mpango huu, imebainisha na kuweka tahadhari kwa kuchukua hatua zifuatazo:- kuandaa bajeti yenye mwelekeo wa kupunguza utegemezi wa kibajeti kwa kuwianisha vyanzo vya  mapato na mkakati wa kuyakusanya na kuwianisha matumizi na upatikanaji wa mapato ya Serikali; kuboresha mazingira ya biashara kwa lengo la kuimarisha sekta binafsi kuchangia utekelezaji wa baadhi ya miradi; na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu Mpango na namna bora ya utekelezaji ili kuongeza ushiriki wa jamii na sekta binafsi.

Ugharamiaji wa Mpango 2017/18
Sekta ya Umma
63.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Shilingi bilioni 11,999.6 zimetengwa kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo Shilingi bilioni 8,969.8 ni fedha za ndani na Shilingi  bilioni 3,029.8 ni fedha za nje. Hivyo, fedha zilizotengwa katika bajeti ya maendeleo zimeongezeka kutoka Shilingi bilioni 11,820.5 mwaka 2016/17 hadi Shilingi bilioni 11,999.6 kwa mwaka 2017/18, ikiwa ni sawa na asilimia 38 ya bajeti yote. Kiasi hiki ni kikubwa kwa asilimia 1.2 ya makadirio ya kutenga Shilingi bilioni 11.80 kila mwaka kutoka mapato ya  Serikali kama ilivyojidhihirisha katika mapitio ya utekelezaji kwa mwaka 2016/17. Serikali itahakikisha kuwa kiasi cha fedha kilichopangwa kwa matumizi ya maendeleo kinapatikana na kugawiwa kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo iliyokusudiwa na kwa wakati. Hivyo, pamoja na juhudi za kupanua na kukusanya mapato katika vyanzo vya kawaida vya Serikali, msisitizo umewekwa katika kubaini na kukusanya kutoka vyanzo vipya. Mfumo wa ukusanyaji katika baadhi ya maeneo utafanyiwa mabadiliko ili kuongeza ufanisi.

Mashirika na Taasisi za Umma
64.     Mheshimiwa Spika, katika historia ya nchi yetu na pia nchi nyingi zinazoendelea, Mashirika ya Umma yamekuwa na mchango mkubwa katika kuchangia maendeleo ya nchi husika. Kwa kutambua hili, Serikali imeelekeza mashirika na taasisi zake za umma za kibiashara kuchangia katika  kugharamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini. Taasisi hizi zinaweza kutekeleza hili kupitia mapato na/au kwa kukopa kwa ridhaa ya Serikali kutokana na dhamana ya mali zao ili kugharamia utekelezaji wa miradi itakayobainishwa kuwa ya kipaumbele.

Sekta Binafsi
65.     Mheshimiwa Spika, kama ilivyojidhihirisha mwaka 2016/17, sekta binafsi, ya ndani na nje, imepokea kwa hamasa wito wa Serikali wa kuchochea uwekezaji hasa katika maeneo mengine zaidi ya kilimo na madini. Serikali kupitia Baraza la Taifa la Biashara itaendelea kusimamia utekelezaji wa maazimio yenye lengo la kuimarisha mazingira wezeshi ya uwekezaji na uendeshaji biashara nchini. Katika kuvutia uwekezaji kwa njia ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, Serikali itaendelea kuimarisha Mfuko wa fedha wa miradi ya ubia (PPP Facilitation Fund) kwa lengo la kugharamia uandaaji wa upembuzi yakinifu kwa miradi inayotarajiwa kutekelezwa kwa njia ya ubia kati ya Serikali na sekta binafsi. Matokeo tarajiwa ni ongezeko la uwekezaji wa sekta binafsi katika miradi ya kipaumbele kwa njia ya ubia. Serikali pia imeamua, kwa makusudi kuondoa mlolongo wa kodi kwa sekta ya kilimo na biashara ndogo ndogo kwa ajili ya kuinua uwekezaji katika sekta hizi. Vile vile, imechukua hatua za kuhakikisha upatikanaji wa maeneo ya viwanda na biashara ndogo kwa urahisi. Msukumo pia umewekwa kuboresha upatikanaji wa mikopo ya gharama nafuu na ya muda mrefu kwa wawekezaji, ikiwa ni pamoja na kuimarisha benki za maendeleo nchini.

66.     Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu Ugharamiaji wa Mpango yapo katika kitabu cha Mpango (Sura ya Tano).

Ufuatiliaji, Tathmini na Utoaji wa Taarifa

68.     Mheshimiwa Spika, Serikali katika kuimarisha eneo hili imeamua kuweka mfumo wa mafunzo na malezi yatakayoharakisha kuimarisha utaalam wa kupanga, kutayarisha, kusimamia, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa miradi. Ninatumia fursa hii kuwaelekeza Maafisa Masuhuli kutenga fedha za ufuatiliaji na tathmini kama sehemu ya gharama za utekelezaji wa miradi husika.69.     Mheshimiwa Spika, hatua pia zimechukuliwa kwa lengo la kuhuisha nyenzo za ufuatiliaji na tathmni. Hii ni pamoja na kuandaa na kutoa mafunzo juu ya matumizi ya Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma. Kwa mwaka 2017/18, mafunzo yatatolewa kwa maofisa wa ufuatiliaji na tathmini kuwawezesha kujua hatua za msingi katika kuandaa, kuratibu na kutathmini miradi ya maendeleo. Serikali kupitia Tume ya Mipango itaandaa mfumo wa kuhifadhi taarifa za miradi ya maendeleo kwa ajili ya kuimarisha upatikanaji wa taarifa za ufuatiliaji na tathmini.

70.     Mheshimiwa Spika, kwa lengo la kuimarisha vigezo vya kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa miradi, Serikali kupitia Tume ya Mipango itaratibu zoezi hilo kupitia Mkakati wa Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano. Hatua hii itasaidia kuboresha upatikanaji wa taarifa za ufuatiliaji na tathmni ya miradi husika kwa kuzingatia vigezo vya utekelezaji vilivyokusudiwa kwa kipindi husika.

71.     Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu Ufuatiliaji, Tathmini na Utoaji Taarifa yapo katika kitabu cha Mpango (Sura ya Sita).

MAJUMUISHO NA HITIMISHO
Majumuisho
72.     Mheshimiwa Spika, tangu Serikali ilipotangaza dhamira ya kujenga uchumi wa viwanda kumekuwa na mwitiko wa uwekezaji, wa umma na binafsi, unaotia matumaini makubwa. Jitihada hizi hazina budi kuungwa mkono, hususan, kwa kuweka kusudio la kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na uendeshaji biashara nchini. Hivyo, hatua za mapitio ya sera, sheria, kanuni na mfumo taasisi wa usimamizi zitaendelea kuimarishwa ili kuhakikisha kuwa tunakuwa na mfumo unaoakisi kusudio hili kwa vitendo. Aidha, hasa kutokana na ukweli kuwa sehemu kubwa ya viwanda vitakavyoanzishwa vitatumia malighafi zinazopatikana kwa wingi hapa nchini, hatua za makusudi zitaendelea kuchukuliwa kwa lengo la kuongeza uzalishaji, tija na ubora wa malighafi zinazozalishwa nchini ili kukidhi mahitaji ya soko linalozidi kukua na kubadilika.

73.     Mheshimiwa Spika, kuna kasi kubwa ya mabadiliko ya mfumo wa maisha na matarajio ya jamii, hasa kundi kubwa la vijana. Matarajio haya ya vijana yanaweza kufikiwa tu ikiwa wataweza kuajiriwa au kuwa na shughuli za kujiajiri wenyewe. Kwa mantiki hii ni wajibu wa msingi kabisa wa Serikali kuzidi kupanua fursa za uwekezaji. Uwekezaji unaweza kuwa ama wa Serikali moja kwa moja, ubia kati yake na sekta binafsi au wa sekta binafsi moja kwa moja. Kwa kutambua hili, Serikali inahitaji sana ushirikiano na mshikamano kati yake na sekta binafsi. Ushirikiano na mshikamano huu unapaswa kuwa mpana na wa kina katika nyanja zote, kuanzia kuibua, kupanga, kutekeleza na kufuatilia na kutathmini hatua za utekelezaji. Katika kutekeleza hilo, msukumo umewekwa katika kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi kwa kuandaa mikutano na mashauriano ya mara kwa mara ikiwa pamoja na ya Baraza la Biashara Tanzania (TNBC) itakayojadili na kutoa mapendekezo ya namna ya kuondoa changamoto zilizopo.

74.     Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano ilitangaza toka mwanzo kabisa azma yake ya kujitanabaisha kuwa ya ukweli na uwajibikaji hasa katika kusimamia matumizi ya rasilimali zinazopatikana kwa manufaa ya Taifa na kila mwananchi. Kutokana na hili, Serikali inaendelea kujielekeza katika kuimarisha makusanyo ya mapato ya ndani kwa kufanyia mapitio ya mifumo na muundo wa usimamizi wa makusanyo ya kodi, malimbikizo ya kodi, kupanua wigo wa kodi kwa kusajili walipa kodi wapya, pamoja na utekelezaji wa mikakati ya kuongeza makusanyo ya kodi. Msukumo pia umewekwa katika kuongeza matumizi ya teknolojia ya kielektroniki ili kupunguza athari za mapungufu ya kibinadamu katika kukusanya, kutunza na kuhifadhi fedha na kumbukumbu. Hatua hizi zote ndizo zitawezesha ustawi wa uchumi na utekelezaji bora wa Mpango wa Maendeleo.

75.     Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyopatikana katika uchumi na utekelezaji wa Mpango yamechangiwa na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wakiwemo nchi marafiki, washirika wa maendeleo, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla. Kwa niaba ya Serikali, ninawashukuru wadau hao kwa michango yao.

76.     Mheshimiwa Spika, kabla ya kumaliza hotuba yangu napenda kumshukuru Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu K. Kijaji (Mb), Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Wizara zote, Wakuu wa Idara za Serikali na Taasisi zinazojitegemea kwa ushirikiano wao wakati wote wa maandalizi ya kutayarisha Taarifa ya Hali ya Uchumi 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/18. Kipekee napenda kuwashukuru watendaji wote wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiongozwa na Katibu Mkuu Bw. Doto James kwa kusimamia vizuri kazi za kila siku za Wizara. Aidha, niwatambue Bw. Maduka Kessy, Kaimu Katibu Mtendaji, viongozi na watumishi wote wa Tume ya Mipango kwa kufanikisha maandalizi ya hotuba hii.

Hitimisho
77.     Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote kwa kunisikiliza. Aidha, hotuba hii na vitabu vya Hali ya uchumi 2016, na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/18 vinapatikana katika tovuti ya Wizara ya Fedha na Mipango www.mof.go.tz na www.mipango.go.tz.

78.     Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba sasa Waheshimiwa Wabunge wapokee, kujadili na kupitisha Taarifa ya Hali ya Uchumi 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/18.

79.     Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni