.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatatu, 5 Juni 2017

KOROSHO SASA KULIMWA KATI, NYANDA ZA JUU


Majaliwa: Wabadhirifu ama zao au zetu

TAKUKURU: Leteni taarifa tufanye kazi
Na Mwandishi Wetu
“HONGERENI sana kwa kazi mnayoendelea kufanya ya kusimamia Korosho. Kwa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) za Februari, 2017, zao la Korosho limeingiza jumla ya dola za Marekani milioni 346.6, kulinganisha na mwaka 2016 ambako tulipata dola za Marekani milioni 184.9.
Kiasi hicho kinafanya Korosho kuwa zao namba moja kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni nchini. Nimefarijika sana kuungana nanyi wadau wenzangu wa zao la Korosho hapa Makao Makuu ya nchi, kujadili mustakbali wa zao hili muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu na kwa wakulima wa zao hili.
Salaam kutoka kwa Mheshimiwa Rais, anawatakia kikao chema. Ahadi ni kushughulika na wale wote watakaojihusisha katika kumnyima haki na manufaa mkulima mmoja mmoja au kikundi au ushirika,” hayo ni sehemu ya maneno ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Aliyatamka wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Wadau wa Tasnia ya Korosho nchini, uliofanyika Chuo cha Mipango, Dodoma, Mei 13 na Mei 14, mwaka huu.
Alisema Waziri Mkuu Majaliwa: “Nimekuja hapa kama mdau, lakini pia kwa dhamana niliyonayo. Kutokana na historia ya zao hili katika makuzi yangu, ninayo imani kwa zao hili, kwamba linaweza kubadili maisha ya watu wetu kuliko rasilimali nyingine tulizonazo. Serikali ya awamu ya tano italilinda zao la Korosho kwa kufa na kupona.
Mwelekeo wa Serikali kwenye Sekta ya Kilimo ni kuhakikisha kuwa kilimo kinakuwa sehemu muhimu ya kuimarisha uchumi wetu, kuongeza kipato cha mkulima, na kuchochea ukuaji wa viwanda ili kuongeza ajira.”
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa Korosho huendesha maisha ya kaya zaidi ya 500,000 kama zao kuu la kibiashara katika wilaya zaidi ya 30 katika Mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani na Tanga.
Na sasa idadi ya Watanzania watakaokuwa wakiguswa moja kwa moja na Korosho inatarajiwa kuongezeka zaidi, na pengine hata kufikia nusu ya Watanzania wote kutokana na mipango iliyo mbioni kutekelezwa, ya kupanua kilimo cha Korosho.
Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba; Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho (CBT) Hassan Jarufu na Kituo cha Utafiti wa zao la Korosho, Naliendele, Mtwara wamezungumzia uwezekano wa Korosho, ama maarufu kama “Dhahabu ya Kijani”, kulimwa katika sehemu nyingine za Tanzania.
Kwamba mbali na wakulima wa asili wa Korosho, Mikoa ya Pwani, Lindi, Tanga, Mtwara na Ruvuma, sasa utafiti umeonyesha Korosho inastawi pia katika Mikoa ya Dodoma, Mbeya, Njombe, Iringa, Morogoro, Tabora na Singida.
Hiyo ni takriban mikoa 12 kati ya mikoa yote nchini. Kwa mujibu wa Sensa ya Mwaka 2012, mikoa hiyo ina wakazi wapatao milioni 25. Tanzania inakadiriwa kuwa na jumla ya watu milioni 50.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu Jarufu anasema upanuzi huo wa eneo la kilimo cha Korosho unakwenda sambamba na uamuzi wa CBT kugawa bure kwa wakulima miche milioni 10 kila mwaka, kwa miaka mitatu, kuanzia na mwaka huu.
Lakini pia, kwa nia ya kuhakikisha ya kuwa mkulima wa Korosho anafaidika, Waziri, Dk. Tizeba amewatangazia wadau wa Tasnia ya Korosho kwamba Serikali msimu huu itagawa bure dawa ya sulphur ambayo ni muhimu sana katika kilimo cha Korosho na kwamba magunia yanayotumika kama vifungashio muhimu, nayo yatatolewa bure.
Ukiweka kando mipango hiyo mizuri ya kupanua kilimo cha Korosho, Tasnia ya Korosho kwa ujumla, inakabilia na changamoto nyingi.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, changamoto hizo ni pamoja na umri mkubwa wa mikorosho unaosababisha mavuno haba; ununuzi holela wa korosho kupitia “Kangomba”; ubadhirifu kwenye vyama vya ushirika, vyama vikuu na vya msingi; tozo nyingi zinazopunguza faida ya mkulima; utegemezi kwa soko la nje; uuzaji wa korosho ghafi badala ya kuziongeza thamani; Vyama Vikuu na Vyama vya Msingi kutokuwa na takwimu sahihi za idadi ya wakulima na mikorosho.
Mheshimiwa Majaliwa anasema kutokana na umuhimu wa zao la Korosho, Rais Dk. John Magufuli ameridhia kuchukua hatua kuliimarisha.
Hatua hizo ni pamoja na kufuta tozo tano kati ya tisa zilizokuwa zinalalamikiwa na wakulima wa Korosho. Tozo hizo ni ya kusafirisha korosho Sh. 50 kwa kilo; gharama ya Mtunza Ghala Sh. 10 kwa kilo kulipwa na mkulima; ushuru wa Chama Kikuu cha Sh. 20 kwa kilo; Kikosi Kazi cha ufuatiliaji zao Sh. 1 kwa kilo; na Makato ya unyaufu.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema pia kwamba Serikali imefuta kilichokuwa kinajulikana kama Mfuko wa Kuendeleza Zao la Korosho (CIDTF) na sasa shughuli zake zitafanywa na Bodi ya Korosho.
“Tumechukua pia hatua dhidi ya viongozi wa vyama vya ushirika wasio waaminifu. Na tutaendelea kuchukua hatua. Aidha, tunaendelea kufuatilia kwa karibu mienendo ya viongozi wa Serikali na Ushirika wanaojihusisha na ubadhirifu wa fedha za ushirika na wakulima,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa akiongeza:
“Tunaposema Hapa Kazi Tu, tunamaanisha kila mmoja atimize wajibu wake ipasavyo. Mkulima alime kwa kuzingatia stadi za kilimo; mnunuzi azingatie taratibu tulizojiwekea; kiongozi wa Ushirika aendeshe Ushirika kwa uadilifu mkubwa na msimamizi wa zao (Bodi), awe nahodha wetu kwenye kuimarisha zao husika kwa kuishauri vizuri Serikali kuhusu namna ya kwenda mbele zaidi.”
Akiwasilisha mada: Athari za Rushwa katika Tasnia ya Korosho nchini, katika Mkutano huo wa Wadau wa Tasnia ya Korosho, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Valentino Mlowola alisema taasisi yake itakuchukua hatua ikipata taarifa za rushwa.
“Wito wangu kwa wadau wa Korosho ni kuichukia rushwa na kuidhibiti; Ushirika imara na endelevu utajengwa na wadau wote iwapo mtaamua kufuata sheria, kanuni na taratibu mlizojiwekea na kuweka pembeni maslahi yenu binafsi.
TAKUKURU itaendelea kushirikana nanyi wakati wote na hatutosita kuchukua hatua pale mtakapotuletea taarifa za vitendo vya rushwa. Kuna malalamiko mengi kutoka kwa wakulima ambayo mengine yanasababishwa na ukosefu wa uadilifu na kuwapo kwa rushwa,” alisema.
Alisema Tasnia ya Korosho ina changamoto ambazo zinahusishwa moja kwa moja na wadau ambao ni Wazalishaji Korosho; Wanunuzi (Wafanyabiashara) na Watendaji wa Serikali/Wanasiasa na zimekuwa zikizua migogoro mingi.
“Makundi haya yanasababisha migogoro mingi kwenye vyama vya Msingi na Vikuu inayodidimiza dhana nzima ya Ushirika; Kutolipwa/ Kupunjwa fedha za mauzo ya Korosho baada ya Korosho zote kuuzwa minadani.
Kuna mlolongo wa kodi nyingi zinazotozwa kwenye mauzo ya Korosho, mfano; makato ya usambazaji wa fedha na kinachoitwa Task Force. Ugumu wa upatikanaji wa pembejeo kwa wakati. Huduma za Ugani kutosambaa kwa wakulima wengi. 

Changamoto zinazohusu maofisa wa umma na wanasiasa kutosimamia vyema Sheria na Taratibu zinazotawala sekta; kuwachanganya wafanyabiashara kwa kutoa maagizo ambayo wakati mwingine yanapingana na sera na sharia na kubuni Sera na Taratibu ambazo zinawaathiri wakulima na wafanyabiashara na kushirikiana na wafanyabiashara na kujipatia maslahi binafsi.”
Alisema alikuwa akiyasema hayo kutokana na ukweli kwamba na yeye amekuzwa na uchumi wa Korosho: “ nayasema haya kwa sababu nayajua kutokana na kuwa nimekuzwa na uchumi wa Korosho. Si kwa kuyasoma tu vitabuni”.
Maazimio kadhaa yalifikiwa katika Mkutano huo wa Wadau wa Tasnia ya Korosho nchini ambayo ni pamoja na Vyama vya Ushirika viajiri wafanyakazi wenye weledi akaunti za benki ili kurahisisha malipo, kuwezesha usalama wa fedha zao na kwa jumla kupunguza wizi na mitandao ya simu itumike kurahisisha malipo.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni