.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Ijumaa, 9 Juni 2017

SERIKALI YAOKOA SH. BILIONI 53.9 - WAZIRI MKUU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imefanikiwa kuokoa shilingi bilioni 53.9 kutokana na uchunguzi na operesheni mbalimbali zilizochukuliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika mwaka 2016/2017.

Amesema kiasi hicho cha fedha ni kikubwa mno ikilinganishwa ni shilingi bilioni 7.0 tu ambazo ziliokolewa katika mwaka 2015/2016.

Ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Juni 9, 2017) wakati akifungua semina ya Mtandao wa Wabunge wa Afrika walio katika Mapambano ya Rushwa (APNAC) tawi la Tanzania kwenye ukumbi wa African Dream mjini Dodoma.

Akizungumzia hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa, Waziri Mkuu amesema Serikali imeanza kupata mrejesho mzuri kwamba watumishi wa umma wanawajibika ipasavyo na vitendo vya rushwa vinaendelea kupungua.

“Baadhi ya hatua tulizochukua ni pamoja na kuimarisha taasisi yetu ya TAKUKURU; kuimarisha matumizi ya mashine za kielektroniki ili kupunguza mianya ya kupoteza mapato; kuanzisha mahakama ya mafisadi; kusimamia nidhamu katika utumishi wa umma na kuchukua hatua za haraka za kinidhamu na za kisheria dhidi ya watuhumiwa wote wa rushwa na ufisadi,” amesema.

Amewaomba wabunge waendelee kuiunga mkono Serikali kwani haina mzaha kwenye mapambano hayo. “Serikali haina mzaha kwenye mapambano dhidi ya rushwa na tutaendelea na mapambano hayo. Hivyo, ninaomba waheshimiwa wabunge muendelee kutuunga mkono katika mapambano haya, twende kwa wananchi tukatoe wito kwao watuunge mkono kwenye vita hii,” amesisitiza.

“Tayari tumefanya tathmini na kubaini mianya ya rushwa katika sekta za ardhi, uchukuzi, biashara na maji na hivyo kuziba mianya hiyo. Tutaendelea kuiwezesha TAKUKURU ili iendelee na kazi nzuri waliyoianza ya kubaini mianya na kutoa ushauri wa kuziba mianya hiyo ya rushwa. Lengo letu ni kuwekeza zaidi kwenye kuzuia, kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba”.
 

Mapema, akizungumza katika semina hiyo, Waziri wa Nchi (OR-Utumishi), Bibi Angela Kairuki amesema TAKUKURU kwa kushirikiana na taasisi zilizo chini yake wako njiani kuanzisha mtaala wa masomo ili rushwa ifundishwe tangu shuleni.

“Napenda kuwahakikishia waheshimiwa wabunge kwamba Serikali ya awamu ya tano haitakubali kuona rushwa ikiota mizizi. Tunaamini wanafunzi wakijengewa uwezo tangu utotoni, watachukia rushwa na hatimaye tutakuwa na Taifa lenye watu waadilifu,” amesema.


Amesema kutokana na zoezi la kupunguza watumishi hewa, hadi kufikia Aprili mwaka huu, Serikali imekwishapokea sh. bilioni 1.2 kwenye akaunti maalum ya TAKUKURU iliyoko HAZINA ambazo zinatokana na makusanyo kutoka kwa waliokuwa watumishi hewa.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa UNDP, Bw. Godfrey Mulisa alisema wataendelea kushirikiana na Bunge katika miradi mbalimbali ikiwemo shughuli zinazofanywa na APNAC.

Awali, Mwenyekti wa APNAC tawi la Tanzania, Bw. George Mkuchika alisema hadi sasa wabunge wapatao 148 wamekwishajiunga na mtandao huo na kwamba anaamini hadi Bunge hili litakapomaliza muda wake, zaidi ya robo tatu ya wabunge watakuwa wamejiunga.
 

Alisema Tanzania ni miongoni mwa Mabunge 20 barani Afrika ambayo ni wanachama wa APNAC.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
40480 - DODOMA. 
IJUMAA, JUNI 9, 2017.​

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni