.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumanne, 6 Juni 2017

WAZIRI MKUU AAGIZA UJENZI WA MAABARA UKAMILISHWE HARAKA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Waziri wa Nchi, Ofisi Rais (TAMISEMI), Bw. George Simbachawene ahakikishe Halmashauri zote zinakamilisha ujenzi wa maabara za sayansi ili vifaa vilivyoletwa visikae bohari kwa muda mrefu.

“Vifaa vya maabara vitatolewa katika shule za Tanzania Bara zilizokamilisha majengo na miundombinu muhimu ya maabara. Hivyo, ni vizuri sasa Halmashauri zote ambazo shule zake hazijakamilisha ujenzi wa maabara ziongeze bidii ili ziweze kunufaika na utaratibu huu. Mheshimiwa Waziri wa Nchi TAMISEMI simamia suala hili,” amesema.

Ametoa agizo hilo leo (Jumanne, Juni 6, 2017) wakati akizungumza na viongozi, walimu na wanafunzi wa shule za sekondari wanaosoma masomo ya sayansi waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa usambazji wa vifaa vya maabara kwa shule za sekondari Tanzania bara iliyofanyika kwenye viwanja vya Lugalo jeshini, jijini Dar es salaam.

Waziri Mkuu pia alimwagiza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako ahakikishe anawasiliana na Waziri mwenzake wa Zanzibar ili wabadilishane uzoefu na utaratibu huo uweze kuzinufaisha pande mbili za Muungano.

“Tunapoimarisha elimu nchini ni vizuri jitihada hizi zikahusisha pande zote mbili za Muungano. Hivyo, wekeni utaratibu wa kubadilishana uzoefu na wenzetu wa Zanzibar, ili jitihada hizi zinufaishe pande zote mbili za Muungano,” amesema.

Akizindua mpango huo, Waziri Mkuu amesema usambazaji wa vifaa hivyo ni kwa ajili ya shule 1,696 za sekondari nchini ambazo zilikamilisha ujenzi kabla ya tarehe 30 Desemba mwaka jana.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuhutubia hadhira hiyo, Prof. Ndalichako alisema ununuzi wa vifaa hivyo umegharimu sh. bilioni 16.9 kutokana na michango ya washirika wa maendeleo kutoka Benki ya Dunia, Shirika la Misaada ya Maendeleo ya Kimataifa (DfID) na Shirika la Misaada ya Maendeleo la Sweden (CIDA).

Alisema usambazaji wa vifaa hivyo utafanyika kwenye kanda 11 za kielimu na utahusisha shule za wananchi 1,625 na shule kongwe 71. “Wizara ya Elimu imenunua vifaa hivyo chini ya programu ya Lipa Kulingana na Matokeo. Vifaa hivi, vinakidhi ufundishaji kwa vitendo kwa asilimia 100 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita,” alisema.

Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi alisema Jeshi la Wananchi wa Tanzania litahakikisha linavisambaza vifaa hivyo katika kanda zote 11 zilizoteuliwa.

Akifafanua kuhusu maghala ya jeshi kutumika kutunzia vifaa hivyo na kemikali, Dk. Mwinyi alisema Serikali imepata unafuu mkubwa kwa kutumia maghala hayo na hivyo kuokoa fedha ambazo zingetumika kulipia sehemu nyingine.

Naye Mshauri wa Elimu kutoka DfID, Bi. Tanya Zebroff akitoa salamu kwa niaba ya washirika wa maendeleo alisema wamefurahi kupata fursa ya kuisaidia Seriakli ya Tanzania na watoto wa Kitanzania katika suala la elimu.

Tulipata fursa ya kutembelea mabanda na kuangalia vifaa vya maabara vilivyooneshwa, pia tumezungumza na wale watoto. Tumeona hamasa waliyonayo watoto wale ambao ni wanasayansi wa siku zijazo, tumefarijika sana,” alisema.

IMETOLEWA NA: 

OFISI YA WAZIRI MKUU, 
JUMANNE, JUNI 6, 2017.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni