.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatatu, 5 Juni 2017

WAZIRI MKUU AAHIDI KUTUMA MKAGUZI GAIRO

GAIA01
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwahutubia mamia ya wakazi wa mji wa Gairo kwenye uwanja wa shule ya msingi Gairo ‘A’ uliofanyika Juni 3, 2017. Waziri Mkuu alikuwa wilayani humo kwa ziara ya siku moja. (Picha na OWM).
GAIA1
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisikiliza maelezo yanayotolewa na Mbunge wa Gairo, Bw. Ahmed Shabiby kuhusu mradi wa maji wa mjini Gairo unaosimamiwa na MORUWASA ambao haujakamilika wakati alipofanya ziara ya siku moja wilayani humo, Juni 3, 2017. Kulia ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Eng. Gerson Lwenge. (Picha na OWM).

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema atatuma mkaguzi aende kuchunguza hali ya upatikanaji wa dawa kwenye zahanati na kituo cha afya cha mjini Gairo, mkoani Morogoro.

Ametoa ahadi hiyo jana (Jumamosi, Juni 3, 2017) wakati akiwahutubia wakazi wa mji wa Gairo na vitongoji vyake kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Gairo ‘A’.

Waziri Mkuu alifikia uamuzi huo baada ya kumhoji Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Albert Lyaruu kama anamiliki duka la dawa au la na kujibiwa kwamba hana duka la dawa. Lakini pia Dk. Lyaruu alikiri kwamba baadhi ya watumishi wa idara yake wanayo maduka ya dawa.

“Sasa ni lazima nilete mkaguzi kutoka ofisi yangu ili tupate picha halisi kama dawa zinazoletwa zinafika, na kama zinafika zinatumikaje. Huyu mkaguzi atakuja kukukagua wewe mwenyewe na kwenye zahanati zako,” alisema Waziri Mkuu.

“Kwenye mkutano wangu na watumishi wa Serikali nimewaeleza kwamba ninyi ni desk officers (maafisa wa kukaa ofisini tu), wala hamuendi vijijini kuona hali halisi ikoje. Ndiyo maana wananchi hawa wanalalamikia kukosa dawa na wewe wala hujui,” alisema.

“Ni lazima uende kwenye vituo vya afya na zahanati na ucheki matumizi ya dawa la sivyo unaweza kupata kesi kama ya Shinyanga ambapo mganga wa kituo cha afya alikutwa na dawa za Serikali nyumbani kwake, baada ya wanachi kumwekea mtego hadi akakamatwa.”

“Serikali haizuii watumishi kuwa na maduka ya dawa, tunachokataa sisi ni kuchukua dawa za Serikali ambazo zinatakiwa kuwatibu wananchi na kuzipeleka kwenye maduka yenu. Tumezuia pia kuwepo kwa maduka ya watu binafsi nje ya hospitali, zahanati au kituo cha afya,” alisisitiza.

Waziri Mkuu aliwataka wananchi wa Gairo wawe macho na walinde mali za umma na inapobidi watoe taarifa mara tu wanapobaini kuna mtu anatumia mali ya umma vibaya.

Waziri Mkuu alikuwa amemwita jukwaani, Dk. Lyaruu ili aeleze ni kiasi gani cha fedha amepokea kutoka Serikalini kwa ajili ya ununuzi wa dawa. Alipotoa mchanganuo wake, wananchi waliohudhuria mkutano huo walizomea na kudai kuwa siyo kweli.

“Ninapokea sh. milioni 109 kila robo mwaka. Na katika kipindi cha miezi mitatu ya mwisho tumepokea shilingi milioni 109 na kati ya hizo tunatoa asilimia 33 ambazo ni sawa na sh. milioni 36 kununua dawa na vifaa tiba. Kwa hiyo hadi sasa hali ya dawa ni nzuri na upatikanaji wake ni kati ya asilimia 85 hadi 90,” alisema Dk. Lyaruu.

Kutokana na majibu yake hayo, wananchi walimzomea daktari huyo na kudai kuwa wananunua dawa hizo kwenye maduka ya dawa. “Tunanunua Waziri Mkuu,” walisikika wakisema.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi waliohudhuria mkutano huo kwamba dawa zinazopatikana kwenye zahanati zinatofautiana na dawa zinazopelekwa kwenye kituo cha afya, hospitali ya wilaya au ya mkoa. Wilaya ya Gairo haina hospitali ya wilaya.

“Mmesikia ushahidi kuwa Serikali inaleta sh. milioni 109 kila mwezi na yeye anazigawa kwa mujibu wa kanuni. Hizi dawa siyo kila ngazi ya tiba unapata dawa za aina zote. Zahanati kuna dawa zake, na kwenye kituo cha afya pia kuna dawa zake. Za kwenye hospitali ya wilaya hazipatikani kwenye kituo cha afya,” alisema.

Pia alitumia fursa hiyo kuwahimiza wajiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili waweze kupata huduma za matibabu bila kulazimika kuwa na fedha taslimu pindi wanapougua wao wenyewe au wanafamilia wao.

“Ninawasihi mjiunge na Bima ya Afya ya Jamii ili muweze kupata huduma za matibabu hata kama huna fedha. Kiasi unachotoa na Serikali inaongeza kiasi hicho hicho. Lazima Baraza la madiwani likae na kuamua ni kiwango gani mtachangia. Ukishalipia, utatibiwa katika hospitali na zahanati yoyote ndani ya halmashauri yako.”

Akigusia sekta ya elimu, Waziri Mkuu alisema Serikali imepeleka sh. milioni 419 ili kuongeza vyumba vya madarasa kwenye wilaya hiyo. “Tumeanza kupelekea sh. milioni 500 kwa kila halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu. Na hapa kwenu tumeleta sh. bilioni 1.2 ili kukamilisha ujenzi wa ofisi za halmashauri,” alisema.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni