RAIS Dkt. John Magufuli amemuagiza
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kumsimamisha kazi Naibu Kamishna wa
Uhamiaji, Bi. Grace Hokororo asimamishwe kazi kwa tuhuma za kuingiza
nchini raia 50 wa Somalia na kuwapa vibali vya kuishi kinyume cha
taratibu.
Kauli hiyo imetolewa leo (Ijumaa,
Julai 28, 2017), na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mara baada ya
kumaliza kikao na Makamishna wa uhamiaji. Kikao hicho kilifanyika
Makao Makuu ya Uhamiaji jijini Dar es Salaam.
Pia Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba kuunda tume ya uchunguzi
kuhusu utoaji wa vibali uraia nchini.
Amesema haiwezekani raia wa kigeni
wanaingizwa nchini na wanapewa vibali vya kuishi bila ya kufanyiwa
uchunguzi wa kina. “Idara ya Uhamiaji tunaitegemea kusimamia mipaka
yetu na kuziba mianya ya watu kuingia bila ya kufuata taratibu lakini
kwa mapenzi yake Ofisa huyu ameruhusu Wasomali kuingia bila kufuata
taratibu.”
Waziri Mkuu amesema ni lazima
uchunguzi ufanyike ili kubaini “Tulidhani ni kitu gani kilimsukuma
kutoa vibali kwa Wasomali hao ambao hawakuwepo nchini wameingia na
kupewa vibali moja kwa moja kwa mapenzi yake tu sasa hii ni dosari
hatuwezi kuivumilia.”
Amesema Serikali inaitegemea Idara
ya Uhamiaji kwa kuzuia mianya ya uingiaji raia mbalimbali kutoka nje
ya nchi bila ya kufuata taratibu, hivyo Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli
ameagiza Ofisa huyo asimamishwe kazi na uchunguzi ufanyike ili
kubaini malengo yake.
"Hawa Wasomali aliowapa vibali
vya kuishi wala hawakuwa wanaishi nchini wameingia tu na kupewa
vibali, hivyo Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli ameagiza ofisa huyo
akae pembeni na achunguzwe ni kujua ni kitu gani kilimsukuma kutoa
vibali kwa raia hao."
Pia Waziri Mkuu ameiagiza idara ya
Uhamiaji wadhibiti kitengo cha utoaji hati za kusafiria za Kibalozi
na kwa wanaomaliza muda wasipewe tena. " Lazima hati hizo
zikaguliwe katika mipaka yote na maeneo yote ya usafiri ili kujua
kama huyo anayeitumia bado anahadhi hiyo na msiporidhika ichukuweni
kwani kuna watu wanazitumia vibaya."
Hata hivyo Waziri Mkuu ameagiza
uchungilzi wa kina ufanyike kwa watu wote walioomba hati za kusafiria
pamoja na vibali vya makazi kama wanakidhi matakwa ya kisheria kabla
ya kuwakabidhi.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni