WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
Tanzania siyo lango la kupitishia dawa za kulevya kwenda nchi za nje
hivyo ameagiza ulinzi uimarishwe katika mipaka yote.
Amesema kunatabia ya baadhi ya watu
wasiokuwa waaminifu kutumia Tanzania kama njia ya kupitisha dawa za
kulevya kwa ajili ya kupeleka nchi za Afrika ya Kusini, Malawi na
Zambia.
Alitoa kauli hiyo jana jioni
(Jumamosi, Julai 29, 2017) alipozungumza na watumishi wa kituo cha
forodha cha Kasumulu kilicho katika mpaka wa Tanzania na Malawi
wilayani Kyela.
Waziri Mkuu alisema ili kuhakikisha
jambo hilo linadhibitiwa ni vema ukaguzi wa watu wanaopita kwenye
maeneo hayo pamoja na mizigo ukaimarishwa.
“Endeleeni kufanya upekuzi wa kina
wa magari, watu na mizigo yote yote katika mipaka yetu. Tanzania siyo
lango la kupitishia dawa za kulevya na Serikali haitakubaliana na
jambo hilo.”
Pia aliwataka viongozi hao
kuhakikisha biashara zote za magendo zinazifanyika mipakani, zikiwemo
za kubadilisha fedha zinadhibitiwa kwa kuwa zinaikosesha Serikali
mapato.
Alisema ni vema yakawepo maduka ya
kubadilishia fedha katika maeneo hayo ili kudhibiti biashara hiyo
ambayo kwa sasa inafanywa kimagendo huku Serikali ikikosa kodi.
“Biashara za magendo zidhibitiwe
katika maeneo haya na yaanzishwe maduka ya kubadilishia fedha ili
biashara hiyo ifanyike kihalali. Pia imarisheni vyanzo vya mapato.”
Pia Waziri Mkuu aliwataka Maofisa wa
Uhamiaji katika mikoa hiyo ya mipakani kuhakikisha wanadhibiti
uingiaji holela wa raia wa kigeni kwa lengo la kuimarisha ulinzi
nchini.
Waziri Mkuu alisema katika baadhi ya
maeneo kwa sasa zimeanza kuonekana silaha ambazo hapo awali
hazikuwepo na ndizo zinazosadikiwa kutumika katika matukio ya
kihalifu.
Awali, Bw. Taniel Magwaza ambaye ni
Afisa Mfawidhi wa Uhamiaji alisema watahakikisha wanafanya kazi kwa
weledi katika kupambana na biashara za magendo kwenye mpaka huo.
Alisema mbali na kupambana na
biashara za magendo pia watadhibiti uingiaji wa wahamiaji haramu kwa
kushirikiana na watumishi idara zote waliopo katika mpaka huo wa
Kasumulu.
Bw. Magwaza alisema katika doria
zilizofanywa mwaka 2016/2017 jumla ya wahamiaji haramu 87 walikamatwa
na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Alisema wahamiaji hao walitokea nchi
za Malawi (30), Ethiopia (47), Burundi (6) Jamuhuri ya Kidemokrasi ya
Congo (DRC) (4), ambapo baadhi walirudishwa makwao na wengine
walifungwa katika Gereza la mkoa wa Mbeya.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 30, 2017
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni