.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumamosi, 5 Agosti 2017

BALOZI SEIF ATAKA LUGHA YA KISWAHILI IENZIWE

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akisalimiana na Muanzilishi na Mlezi wa Chama cha Lugha na Fasihi ya Kiswahili Tanzania { CHALUFAKITA } Profesa Madumla alipowasili kuwa mgeni rasmi katika usiku wa Mswahili ulioadhimishwa katika Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Kati kati yao ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mheshimiwa Riziki Pembe Juma.
Vijana wa Kikundi cha Utamaduni kutoka Kijiji cha Uroa Wilaya ya Kati wakiringa vyao wakati wakitoa burdani safi iliyosheheni lahaja za Kipwani kwenye maadhimisho ya Usiku wa Mswahili.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma kutoka Kulia akinengua aliposhindwa kukaa kwenye kiti wakati wa burdani ya Kikundi cha Utamaduni cha Mkoa Mjini Magharibi kilipokuwa kikitumbuiza kwenye Usiku wa Mswahili.
Eee! Msewe Mtamu bwana. Hivi ndivyo inavyojionyesha Picha hii wakati wana Kikundi cha Utamaduni wakifanya vitu vyao kwa maringo wakati wa maadhimisho ya Usiku wa Mswahili hapo Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na Waswahili ndani ya Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi wakati wa maadhimisho ya Usiku wa Mswahili.
Balozi Seif akimkabidhi zawadi mshindi wa kwanza la shindano la Mwalimu Mbunifu katika lugha ya Kiswahili Inocent Huale kutoka Shule ya Sokondari ya Mtakatifu ST. Steven ya Kilimanjaro.

Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Elimu Zanzibar Mh. Riziki Pemba Juma, Munzilishi na Mlezi wa Chama cha Lugha na Fasihi ya Kiswahili Tanzania Profesa Madumla na kushoto ya Balozi Seif ni Mshauri wa Rais wa Zanzibar katika masuala ya Utamaduni Bwana Chimbeni Kheir na Mkuu wa Wilaya ya Mjini Bibi Marina Thomas.
Balozi Seif akimkabidhi zawadi mshindi wa Tatu wa Shindano la Mwalimu Mbunifu Mwalimu Atupakiswe Mlawa wa Shule ya Wasichana Ruvu Mkoani Pwani.
 
Picha na – OMPR – ZNZ.
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali alisema Lugha ya Kiswahili imeonyesha wazi kwamba ni bidhaa inayouzika Kimataifa kiasi cha kuweza kuchangia pato la Taifa sambamba na kufaidisha hata Mtu mmoja mmoja.

Alisema lugha hiyo Maarufu Duniani kwa hivi sasa inaendelea kutoa mchango mkubwa wa Kiuchumi kwa Watu wengi waliopata bahati ya kuajiriwa kufundisha Lugha hiyo ndani na nje ya Nchi ikiwemo Sweden, Ujerumaji, Marekani, China, Uganda na Rwanda.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo katika hafla Maalum ya Usiku wa Mswahili iliyofanyika katika Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi uliopo Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Alisema Kiswahili hivi sasa kimekuwa sana na kutumiwa na Watu mbali mbali hata katika Vikao vikubwa vya Umoja wa Mataifa ya Bara la Afrika {AU} na ile ya Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki { EAC }.

Balozi Seif alitoa rai katika ufundishwaji wa Lugha ya Kiswahili ni vyema ukaenda sambamba na Utamaduni wa Mswahili ambao kwa kutumia mbinu hiyo Wanafunzi maskaulini wataweza Kuutambua Utamaduni wao.

Alisema mfumo huo utaleta matunda hususan kwa wanafunzi wa kigeni ambao wao watapata fursa ya kuutangaza Utamaduni wa Mswahili katika Mataifa yao iwao watafundishwa kuitia madarasa ya mapishi ya vyakula vya asili kama manda, bumbwi, makopa, mabopwe na msambwija.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitahadharisha kwamba zipo tabia za baadhi ya Watu kubeza Utamaduni wa Mswahili hasa wa kutotumia Lugha ya Kiswahili kwa fasaha.

Alisema Serikali imeandaa mikakati maalum kuhakikisha kuwa Kiswahili kinaendelezwa na kusimamia maendeleo ya Lugha hiyo na wakati huo huo Baraza la Kiswahili Tanzania { BAKITA} na lile la Zanzibar { BAKIZA } kuwakutanisha Waswahili waliojiunga kwenye vyama tofauti katika makongamano na majadiliano kuhusu Kiswahili.

Balozi Seif alielezea faraja yake kutokana na uwamuzi wa Taasisi zinazosimamia Taalum ya Lugha ya Kiswahili kuwapatia motisha Walimu Wabunifu wanaosimamia na kufundisha Lugha hiyo na kuacha mazoea ya kuona walimu wa Taaluma ya Sayansi ndio pekee wanaostahiki heshima hilo.

Alisema maamuzi ya kuwazawadia walimu hao ni jambo jema na lenye manufaa katika Sekta ya Elimu kama inavyoelezwa na wanafalsafa waliobobea katika Sekta hiyo akina Plato na Aristotle waliosisitiza kuwazawadia wanataaluma wanaofganya vizuri katika fani zao.

“ Hongereni sana na endeleeni kuutunza Utamaduni wetu. Waswahili tuna useni wetu usemao:- Mkataa kwao mtumwa, lazima tukitunze na kukithamini kilicho chetu ”. Alisema Balozi Seif.

Alifahamisha kwamba jambo hilo litawajenga Walimu ari katika kutumia mikakati na mbinu stahiki za kiufundishaji ambazo zitawafanya Wanafunzi kuipenda, kuijali na kuithamini Lugha ya Kiswahili.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuomba Uongozi wa Chama cha Lugha na Fasihi ya Kiswahili Tanzania { CHALUFAKITA } utakapoandaa matukio mengine kushirikiana kwa karibu na vyama, taasisi na jumuiya zote zinazohusiana na Lugha na Utamaduni katika kuuenzi, kuutunza na kuuendeleza Utamaduni wa Mswahili.

Akitoa Taarifa ya Shindano la Mwalimu Mbunifu lililoandaliwa na Chama cha Lugha na Fasihi ya Kiswahili Tanzania { CHALUIFAKITA } Katibu wa Chama hicho Dr. Othman Ponera alisema maandiko ya Walimu 83 yalipokewa na Chama hicho kutoka kwa Walimu mbali mbali walioshiriki kwenye kinyang’anyiro hicho.

Dr. Ponera alisema maandiko hayo yalifanyiwa kazi na Majaji walioteuliwa kuendesha shindano hilo kutoka ndani na nje ya Tanzania na hatimae kupata washindi Kumi waliofikia asilimia zisizopungua 60.

Alisema kundi hilo la Walimu kumi Wabunifu wa Usomeshaji wa Lugha ya Kiswahili ndio walioibuwa washindi Watatu wa kwanza walioingia Fainali iliyolenga kupatikana Nukta 40 ili kufikisha Nukta 100 za shindano hilo.

Mapema Katibu wa Baraza la Kiswahili Zanzibar {BAKIZA} Bibi Mwanahija Ali Juma alisema chama cha Lugha na Fasihi ya Kiswahili Tanzania { CHALUIFAKITA } kina lengo la kuona Lugha ya Kiswahili inaendelea kukua na kuimarika siku hadi siku.

Bibi Mwanahija alisema wakati umefika sasa kwa Taasisi, Jumuiya na hata wafadhili wa ndani na nje ya Nchi kufikiria wazo la kuhamasisha Walimu na Wanafunzi katika kukiendeleza Kiswahili katika mfumo unaotumiwa kama ule wa kuwazawadia wale waliofanya vyema kwenye Mitihani yao ya Masomo mengine ya Sayansi.

Katika hafla hiyo Maalum ya Usiku wa Mswahili Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi zawadi kwa washindi wtatu wa kwanza wa shindano ya Mwalimu Mbunifu sambamba na wale walimu waliomo katika kundi la washindi kumi.

Walioongoza mshindi kwa kwanza ni Mwalimu Inocent Haule kutoka Shule ya Mtakatifu ST. Steven ya Kilimanjaro aliyepata nukta 76, wa Pili Mwalimu Ali Shaaban kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana wasioona ya Korogwe Tanga na Watatu ni Mwalimu Atupakiswe Mlawa wa Shule ya Wasichana Ruvu Mkoani Pwani.

Hafla hiyo ya Usiku wa Mswahili iliyojumisha pia wawakilishi wa Vyama vya Kiswahili kutoka Rwanda, Uganda na Kenya ilipambwa na vyakula vya Asili vilivyoandaliwa maalum ili kuleta raha na furaha kwa Waswahili waliohudhuria maadhimisho hayo.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

5/8/2017.




Hakuna maoni :

Chapisha Maoni