.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumanne, 1 Agosti 2017

WAZIRI MKUU ATEMBELEA MTAMBO WA KUSAFISHA DHAHABU CHUNYA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea na kujionea mtambo wa kisasa wa kusafisha dhahabu kwa asilimia 99 unaomilikiwa na kampuni ya Sunshine Group uliopo katika kata ya Matundasi wilayani Chunya mkoani Mbeya.

Ametembelea mtambo huo leo (Jumanne, Agosti 1, 2017) wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mbeya na kusema kuwa mtambo huo ni wa kwanza kuweza kusafisha dhahabu kwa kiwango hicho hapa nchini.

Amesema kwa Tanzania kampuni ya Sunshine Group ndiyo yenye mtambo wa kuweza kusafisha dhahabu na kufikia asilimia 99 ukilinganisha na makampuni mengine yanayomiliki migodi.

Pia Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kufanya mazungumzo na makampuni mbalimbali kwa ajili ya kuwekeza katika mradi wa ujenzi wa mtambo wa kuchenjulia makinikia ili kuweza kusafirisha dhahabu halisi.

Naye Ofisa Madini Mkoa wa Mbeya, Mhadisi Said Makwama amesema dhahabu inayosafishwa katika mtambo huo ikipelekwa nje ya nchi inaingizwa sokoni moja kwa moja tofauti na migodi mingine.

Mhandisi huyo alisema Sheria mpya ya Madini imesaidia Serikali kupata kodi ya juu itokanayo na Mrabaha wa asilimia 6 na ‘clearance and inspection fee’ ya asilimia moja ya thamani ya madini yanayosafirishwa ukilinganisha na mrabaha wa awali wa asilimia nne.

“Uzalishaji uliofanyika kwa mwezi Julai tu Serikali imepata mrabaha wa sh. milioni 333 ukilinganisha na sheria ya zamani Serikali ingepata shilingi milioni 191. Sheria mpya imewezesha Serikali kupata mapato zaidi ya sh. milioni 142. Awali ilikuwa inapata sh. milioni 191 kwa gramu 52. 518 kwa mgodi mmoja wa Sunshine.”

Kwa upande wake mbunge wa Chunya, Mheshimiwa Victor Mwambalaswa ameiomba Serikali kukubali maombi ya Kampuni ya Sunshine ya kujenga mtambo wa kuchenjulia mabaki ya mchanga wa dhahabu wilayani Chunya ili kuweza kuongeza fursa za ajira, ambapo Waziri Mkuu amesema suala hilo linashughulikiwa.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Sunshine Group Bw Leo Le alisema kampuni ya Sunshine Group ni ni miongoni mwa makampuni makubwa kutoka nchini China yaliyowekeza Tanzania, ambapo thamani ya uwekezaji wao ni zaidi ya Dola za Marekani milioni 100.

IMETOLEWA NA: 

OFISI YA WAZIRI MKUU, 
JUMANNE, AGOSTI 1, 2017

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni