Na Jenikisa Ndile-MAELEZO
Watanzania wameaswa kuzingatia namna bora ya kuhifadhi mazingira, upangaji wa matumizi bora ya ardhi na utekelezaji wa mipango ili kuleta tija na maendeleo endelevu nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Sazi Salula leo jijini Dar es salaam alipokuwa akifungua Mkutano wa wadau wa mazingira unaohusu utekelezaji wa miradi ya majaribio ya Mkakati wa Kupunguza Uharibifu wa Misitu (MKUHUMI) nchini.
Bw. Sazi alisema kuwa mipango hiyo ya MKUHUMI inalengo la kuondoa umasikini kwa watanzania waishio vijijini ambao wapo karibu na hifadhi za misitu inasimamiwa na kutekelezwa kwa kushirikiana na Serikari ya kijiji ili kuhakikisha mafanikio yanapatikana kwa kuzingatia utekelezaji na usimamizi wa sheria kupitia kamati za vijiji.
Majaribio ya sera ya mazingira yamefadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Norway ili kuboresha na kushughulikia masuwala ya ardhi, misitu na kupunguza gesi joto kwa kuhimiza jamii kupanda miti kwa shughuli za maendeleo endelevu nchini.
Mipango hiyo inatekelezwa katika wilaya za Sumbawanga, Lindi, Kilwa, Zanzibar, Pemba, Kigoma na Kondoa ambapo sera hiyo imewapa elimu ya kujenga utayari wa shughuli za MKUHUMA na kuwezesha ushiriki mpana wa wadau ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake Kiongozi wa miradi ya majaribio ya MKUHUMI Merja Makela alisema kuwa taasisi yake imefanikiwa kutokana na kusimamia miradi hiyo ambayo imepokelewa na kutekelezwa kama ilivyopangwa katika maeneo husika nchini.
Naye Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Julius Ningu alisema kuwa kwa tathmini iliyofanyika mwaka 2013, asilimia 55 ya ardhi ya Tanzania imefunukwa na misitu ambapo juhudi zinaendelea kufanyika kwa kuwaelimisha watanzania kuendelea kuitunza misitu hiyo kwa manufaa ya sasa na baadaye.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni