Ijumaa, 17 Februari 2017
BARABARA YA ARUSHA –KITETO - KONGWA KUFANYIWA USANIFU - WAZIRI MKUU
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaanza kufanya upembuzi na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kutoka Arusha – Kiteto – Kongwa ili ijengwe kwa kiwango cha lami.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Alhamisi, Februari 16, 2017) wakati akizumgumza na mamia ya wakazi wa mji wa Orkesumet, wilayani Simanjiro akiwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani Manyara.
Amesema Serikali imepanga kuiombea fedha za kazi ya ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa km.430 kwenye mkutano ujao wa bajeti na kwamba imepanga kutafuta wakandarasi wengi na kuwagawa kwa vipande ili barabara hiyo ijengwe kwa kipindi kifupi.
“Barabara yenu nimeiona. Imo kwenye Ilani ya CCM. Ujenzi wake utaanzia Arusha –Mbauda – Simanjiro – Kiteto hadi Kongwa. Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameahidi kuwa Serikali hii haitawaangusha na itawahudumia wananchi wote bila kujali itikadi za kisiasa,” amesema Waziri Mkuu huku akishangiliwa na wakazi hao.
Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa maji kwenye mji wa Orkesumet ambao ni Makao Makuu ya wilaya ya Simanjiro, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendela kutoa fedha kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji kutoka Ruvu hadi kwenye mji huo.
Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa umeme, Waziri Mkuu aliwahakikishia wakazi hao nia ya Serikali ya kufikisha umeme katika vijiji vya wilaya hiyo.
“Serikali imeamua kupeleka umeme kwenye vijiji 8,000 na kati ya hivyo, vijiji vya Simanjiro vimo,” alisema wakati akijibu hoja za wabunge wa jimbo juu ya kero zinazowakabili wakazi hao.
“Serikali imepanga kufikisha umeme kupitia miradi ya REA. Wakandarasi wameshapewa kazi, na sasa wameenda kutafuta vifaa. Tumeamua hivi sasa kama kuna vijiji vya mbali na line ya umeme, au ni gharama sana kuwapelekea umeme kwa sababu ya umbali, hao ni lazima wapatiwe umeme wa solar na tutaweka sola katika kila nyumba,” amesema.
Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa ifikapo Mei 30, mwaka huu kazi hiyo iwe imekamilika katika wilaya ya Simanjiro. “Vijana wa Simanjiro acheni kulalamika kuwa hakuna ajira. Tumieni fursa hii kujipanga na muweke vitega uchumi vya kibiashara kama vile saluni za kunyoa nywele au vibanda vya kuweka muziki kwenye simu za viganjani,” amesema.
Akizungumzia kuhusu migogoro ya ardhi ambayo iliandikwa kwenye mabango, Waziri Mkuu alimtaka Mkuu wa Wilaya hiyo, Eng. Zephania Chaula afuatane na Afisa Ardhi wa Wilaya na waende kwenye vijiji husika kusikiliza malalamiko ya wananchi hao.
“DC simamia hilo na hakikisha hayo masuala yanamalizwa. Afisa ardhi ahakiki malalamiko ya wakazi wa vijiji husika.” Akifafanua kuhusu baadhi wa watu kujimilikisha maeneo makubwa ya ardhi, Waziri Mkuu alisema Sheria ya Ardhi namba 5 inaainisha kuhusu umiliki wa ardhi na kwa Serikali ya Kijiji hairuhusiwi kutoa ardhi zaidi ya ekari 50.
“Na kama ni kwa ruhusa ya Halmashauri, nayo pia mwisho wake ni kutoa ekari 500. Zaidi ya hapo, ni lazima hiyo ardhi itolewe kwa kibali cha Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo kama kuna mtu amepata eneo kubwa zaidi yapo, muulizeni kapewa na nani? Je ana kibali cha Rais,” alihoji.
“Kama ni migogoro ya mipaka ya wilaya wala hiyo haina tatizo kwa sababu GN zipo. Viongozi wa wilaya husika, kaeni pamoja, angalieni hizo GN na mmalize hayo matatizo,” alisisitiza.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, FEBRUARI 16, 2017.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni
(
Atom
)
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni