Na mwandishi wetu, Zanzibar
Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (TADB) imewahakikisha kuwapatia mikopo wakulima wa Zao la Karafuu visiwani Zanzibar katika kuhakikisha inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta Mapinduzi yenye tija katika wakulima hao.
Hayo yalielezwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga wakati akitoa mada juu ya fursa zinazopatikana kwa ajili ya wakulima na wadau wa kilimo cha karafuu visiwani Zanzibar katika Kikao cha Wadau wa Karafuu kilichokuwa kinafanyika mjini Unguja.
Bw. Assenga alisema kuwa Serikali inatambua changamoto wanazokutana nazo wakulima nchini na hivyo uanzishwaji wa TADB unalenga kutekeleza hatua mbalimbali zikilenga kuharakisha mapinduzi na maendeleo katika Sekta ya Kilimo ikiwemo uendelezaji wa zao la karafuu ambalo ni zao kuu la biashara visiwani Zanzibar.
“Tunatambua kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) iliweka Mkakati Maalum wa miaka 10 (2011 -2021) wa kuongeza uzalishaji, usafirishaji, ubora na tija wa zao la karafuu kwa kutambua hilo Benki inakuja kuongeza kasi juhudi hizi za Serikali,” alisema.
Alisema kwa kutambua juhudi za SMZ zao la karafuu lilipewa kipaumbele cha pekee miongoni mwa minyororo ya thamani ya kwanza kuanza kupatiwa mikopo na Benki hiyo kwa ajili ya uongezaji wa thamani mazao mbalimbali nchini.
Aliongeza kuwa maeneo yanayowekewa mkazo katika undelezaji wa kilimo cha karafuu ni pamoja na uongezaji tija wa kilimo cha karafuu ambapo TADB inatoa mikopo na kusaidia shughuli mbali mbali za uongezaji tija wa mazao yatokanayo na kilimo cha karafuu.
“Katika kuhakikisha kuwa uongezaji tija wa kilimo cha karafuu unafanyika ipasavyo Benki inashirikisha wadau wa Kilimo, utafiti na huduma za ugani na ili kuwapatia wakulima mafunzo ya kilimo cha kisasa cha karafuu na kutumia mbinu bora za kilimo ili kuongeza mazao ya karafuu,” Bw. Assenga alisema.
Bw. Assenga aliongeza pia Benki inatoa mikopo kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo za kilimo (mbegu bora na miche ya karafuu yenye kuvumilia magonjwa, wadudu, na inayotoa mazao mengi na kiwango kikubwa cha karafuu, mbolea, madawa na mengineyo); na kugharamia teknolojia bora na nafuu ya umwagiliaji (panapohitajika).
Aliyataja maeneo mengine yanapatiwa mikopo ni pamoja na ununuzi wa vifaa, mashine na mitambo mbalimbali ya kilimo cha karafuu na mtaji kwa ajili ya uendeshaji wa shamba, uongezaji wa thamani na gharama za uhifadhi na masoko
Bw. Assenga alisema kuwa TADB pia inatoa mikopo kwa ajili ya uendelezaji wa zao la karafuu katika kusaidia uwekezaji kwa ajili ya ujenzi, ununuzi wa mitambo na ufungaji wa mitambo ya usindikaji wa karafuu kwa ajili ya kuongeza thamani mazao ya karafuu. Ikiwemo ununuzi wa mashine bora za uvunaji, ukaushaji, usafirishaji na uhifadhi wa karafuu; ununuzi wa vifaa vya teknolojia ya kisasa kwa ajili ya kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno. Mikopo mingine ni kwa ajili ya ununuzi wa mitambo ya usindikaji pamoja na vifungashio vya karafuu; uchambuzi wa madaraja na ubora wa karafuu na uwekaji wa utambuzi wa muuzaji; na kugharamia mahitaji mengineyo ili kuongezea karafuu thamani.
Kwa upande wa miundombinu ya masoko, Kaimu Mkurugenzi huyo alisema kuwa Benki inatoa mikopo kwa zao la karafuu kwa lengo la kuendeleza miundombinu ya masoko kama vile ujenzi wa maghala/vifaa vya kuhifadhia karafu na mazao yake na miundombinu ya masoko; kugharamia usafirishaji wa karafuu na mazao yake yaliyo tayari kwenda sokoni. Mikopo mingine ni kwa ajili ya uanzishaji wa mifumo ya upatikanaji wa taarifa za masoko, kuwezesha uhusiano wa masoko ya ndani na masoko ya kikanda na kugharamia mahitaji mengineyo ya kuwezesha miundombinu ya masoko.
Naye, Mkurugenzi wa Biashara na Mikopo wa TADB, Bw. Augustino Chacha amesema kuwa TADB inatoa mikopo ya aina tatu ambayo ni Mikopo ya Muda Mfupi (Hadi Miaka Miwili (2)), Mikopo ya Muda wa Kati (Zaidi ya Miaka 2 hadi Miaka Mitano (5)) na Mikopo ya Muda Mrefu (Zaidi ya Miaka 5 hadi Miaka Kumi na Mitano (15)).
“Mikopo hii ni ya riba nafuu ambayo inalenga katika kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini,” alisema.
Karafuu ni zao la kipaumbele katika uchumi wa Zanzibar ambapo Serikali ya Mapinduzi kupitia Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) imekuwa ikifanya Mageuzi makubwa katika Sekta nzima ya Karafuu ikiwa ni pamoja na kutengeneza Sheria, Sera na Miongozo madhubuti ya kusimamia Sekta hii ambapo faida, tija na ustawi wa maisha ya wanaotegemea kupata kipato katika zao hili unaonekana.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni