Na: Veronica Kazimoto-Dar es Salaam
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Agosti, 2017 umepungua hadi kufikia asilimia 5.0 ikilinganishwa na asilimia 5.2 ilivyokuwa mwezi Julai, 2017. Hii inamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2017 imepungua ikilinganishwa na mwezi Julai, 2017.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii Ephraim Kwesigabo wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu amesema kupungua kwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Agosti, 2017 kumechangiwa na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula.
Kwa upande wa thamani ya shilingi ya Tanzania, Kwesigabo amesema uwezo wa Shilingi 100 katika kununua bidhaa na huduma umefikia Shilingi 92 na senti 20 mwezi Agosti 2017 ikilinganishwa na Shilingi 91 na senti 87 ilivyokuwa mwezi Julai, 2017.
Mfumuko wa Bei ambao hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi, una mwelekeo unaofanana na nchi ya Uganda ambapo Mfumuko wa Bei umepungua hadi asilimia 5. 20 mwezi Agosti, 2017 kutoka asilimia 5.70 mwezi Julai, 2017. Nchini Kenya, Mfumuko wa Bei wa mwezi Agosti, 2017 umeongezeka hadi asilimia 8.04 kutoka asilimia 7.47 mwezi Julai, 2017.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni