.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Ijumaa, 20 Aprili 2018

RAIS MHE. DKT. MAGUFULI AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA WAGENI KUTOKA UMOJA NA AFRIKA (AU) NA MISRI IKULU JIJINI DAR ES SALAAM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Kamishna wa Amani na Usalama wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Balozi Smail Chergui Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo na Kamishna wa Amani na Usalama wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Balozi Smail Chergui Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Kamishna wa Amani na Usalama wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Balozi Smail Chergui Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Waziri Mkuu Mstaafu wa Misri ambaye kwasasa ni Mshauri wa Rais wa Misri Injinia Ibrahim Mahlab kabla ya kuanza mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza jambo na Waziri Mkuu Mstaafu wa Misri ambaye kwasasa ni Mshauri wa Rais wa Misri Injinia Ibrahim Mahlab kabla ya kuanza mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Waziri Mkuu Mstaafu wa Misri ambaye kwasasa ni Mshauri wa Rais wa Misri Injinia Ibrahim Mahlab mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo na Waziri Mkuu Mstaafu wa Misri ambaye kwasasa ni Mshauri wa Rais wa Misri Injinia Ibrahim Mahlab Ikulu jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU

MATUKIO MBALIMBALI KUTOKA BUNGENI MJINI DODOMA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu, Jenista Mhagama, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Wenyeulemavu, Antony Mavundebungeni mjini Dodoma Aprili 20, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, akijibu maswali Bungeni mjini Dodoma Aprili 20, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson, akizungumza Bungeni mjini Dodoma Aprili 20, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalim akijadili jambo na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Wenyeulemavu, Antony Mavunde, Bungeni mjini Dodoma Aprili 20, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akioneshwa kitu na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile, kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Aprili 20, 2018, kulia ni Mbunge wa Viti Maalum, Halima Bulembo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

SERIKALI YATOLEA UFAFANUZI ULIPAJI WA PENSHENI WASTAAFU WA SHIRIKA LA POSTA NA SIMU

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)

Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma

Serikali imeeleza kuwa haiwezi kuhamisha jukumu la kulipa pensheni ya Wastaafu wa Shirika la Posta na Simu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenda kwenye mojawapo ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kuwa zoezi la kuunganisha Mifuko ya Pensheni halijakamilika.

Hayo yamesemwa Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Ludewa Mhe. Deo Ngalawa (CCM), aliyetaka kufahamu, lini Serikali itakuwa tayari kuhamisha jukumu la kuwalipa Wastaafu wa lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki kwenye moja wapo ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji alisema kuwa Serikali kupitia Shirika la Posta inaendelea na jukumu la kuwalipa pensheni ya kila mwezi Wastaafu wa shirika hilo.

“Uamuzi wa kuhamisha au kuendelea na utaratibu wa sasa utatolewa baada ya zoezi la kuunganisha mifuko ya pensheni kukamilika”, alisema Dkt. Kijaji.

Katika maswali ya nyongeza Mhe. Ngalawa alihoji kwakuwa Shirika la Posta limekuwa likisuasua katika kujiendesha na miongoni mwa mambo yanayosababisha ni ulipaji wa pensheni za Wastaafu hao, Serikali haioni ni wakati wa kulitua mzigo Shirika hilo na kuchukua jukumu hilo.

Mhe. Ngalawa alieleza kuwa kuanzia mwaka 2015 malipo ya pensheni kwa Wastaafu yalipanda kutoka Sh. 50,000 hadi Sh. 100,000 lakini kuna baadhi ya Wastaafu hawajabadilishiwa pensheni zao. Alitaka kujua lini Serikali itabadilisha pensheni hizo ili ziwe sawa kwa wote.

Dkt. Kijaji alisema kuwa baada ya Shirika la Posta kulipa Wastaafu huwasilisha madai yake Hazina na Serikali imekuwa ikirejesha fedha hizo kwa wakati na hakuna madai ya ziada.

Alifafanua kuwa Serikali kupitia Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii imekuwa ikilipa ongezeko la pensheni kwa Wastaafu kwa wakati, na kukiri kuwa Wastaafu wachache wamekuwa wakipeleka kesi za kutoongezewa pensheni zao kutokana na sababu mbalimbali.

Dkt. Kijaji alisema kuwa Hazina imekuwa ikipokea malalamiko hayo na kuyashughulikia, ametoa wito kwa Wastaafu wote yenye malalamiko wafike Hazina ili waweze kusaidiwa.

WAZIRI MKUU AKUTANA NA BALOZI WA CHINA NCHINI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mbunge wa Kuteuliwa, Abdallah Bulembembo, kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Aprili 20, 2018, kutoka kushoto ni Mbunge wa Karagwe, Innocent Bashungwa, wa kwanza kulia ni Mbunge wa Mtama, Nape Mnauye na wapili kulia ni Mbunge wa Sumbawanga mjini, Aeshi Hilaly. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mbunge wa Viti Maalum, Munira Mustafa Khatib, kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Aprili 20, 2018, kulia ni Mbunge wa Viti Maalum, Halima Bulembo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini, Eng. Ramo Makani, kwenye jengo la Utawala Bungeni mjini Dodoma Aprili 20, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Balozi wa China nchini Tanzania, Bi. Wang Ke, ofisini kwake Bungeni mjini Dodoma Aprili 20, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Balozi wa China nchini Tanzania, Bi. Wang Ke, ofisini kwake Bungeni mjini Dodoma Aprili 20, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WASIOLIPA KODI YA ARDHI KUCHUKULIWA HATUA

Na Mahmoud Ahmad,Arusha.

Kamishna Msaidizi wa Ardhi kanda ya Kaskazini Leo Komba amesema kuwa serikali itawachukulia hatua wamiliki wa ardhi wasiolipa kodi ya ardhi kwa mujibu wa sharia ya ardhi Namba 4 ya mwaka 1999 hivyo amewataka kulipa kodi hiyo kwa wakati ili kuepuka kufikishwa mahakamani.

Akizungumza jijini Arusha Komba alisema kuwa wizara imejipanga kikamilifu kusimamia taratibu za kuwafikisha mahakamani wadaiwa wote watakaokaidi kulipa kodi ya ardhi na kukusanya kodi ya pango la ardhi kwa kila kipande cha ardhi kilichomilikishwa kwa mujibu wa sharia.

Aidha alisema kuwa Wizara imerahisisha ulipaji wa kodi ya pango la ardhi ambapo mmiliki akishapata Ankara ya madai anaweza kulipa kwa kutumia simu ya kiganjani .

“Pamoja na suala zima la ulipaji kodi la Ardhi ,Mhe.Waziri wa Ardhi ameanzisha kampeni ya Funguka kwa Waziri wa ardhi kuondoa migogoro ya ardhi ,Hivyo wale wananchi wenye kero za ardhi wanatakiwa kujaza fomu ambazo zipo kwenye ofisi zote za Halmashauri na Ofisi za wakuu wa Wilaya ili Waziri atatue kero hizo” Alisema Kamishna

Naye Afisa Ardhi Mwandamizi Thadeus Riziki amesema kuwa ardhi ambazo hutozwa kodi hiyo ni zile ardhi ambazo zimepimwa na zina hatimiliki,maeneo ambayo hayajapimwa mengi hayajaingizwa katika mpango wa kulipa kodi.

Afisa huyo alisema kuwa serikali ina mpango wa kupima maeneo ambayo hayapimwa na pia kurasimisha makazi holela ili waweze kupatiwa huduma muhimu za kijamii.

Alisema kuwa ni vyema wananchi wakajijengea utaratibu wa kulipa kodi kwa wakati ili kuepuka usumbufu ikiwemo kufikishwa mahakamani .

LIGI KUU YA WANAWAKE YA SERENGETI PREMIUM LITE HATUA YA NANE BORA KUENDELEA WIKIENDI,SERENGETI YAGAWA MAVAZI RASMI KWA TIMU

Ligi Kuu ya Wanawake ya Serengeti Premium Lite Hatua ya Nane Bora inatarajia kuendelea Wikiendi hii.

Jumamosi Aprili 21,2018 zitachezwa mechi Tatu na mchezo mmoja utachezwa Jumapili Aprili 22,2018.

Jumamosi Kwenye Uwanja wa Karume Evergreen watawakaribisha Alliance ,Wakati kwenye Uwanja wa Mbweni JKT Quenns watakuwa wenyeji wa Simba Queens nayo Kigoma Sisterz ikiwa Uwanja wa Tanganyika kuwaalika Baobab.

Mchezo wa Panama dhidi ya Mlandizi Queens wenyewe utachezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Samora Iringa.

Ligi hiyo ilisimama kupisha maandalizi ya timu ya Taifa ya Wanawake iliyokuwa na mchezo wa kufuzu fainali za Africa kwa Wanawake dhidi ya Zambia.

Katika hatua nyingine Wadhamini wa Ligi hiyo ya Wanawake kampuni ya Bia ya Serengeti kupitia Bia yake ya Serengeti Premium Lite,imekabidhi mavazi rasmi kwa timu zote.

Meneja Masoko wa Serengeti Anitha Msangi amesema Serengeti inaamini kuwa kuidhamini Ligi Kuu ya Wanawake wanachangia kuleta maendeleo ya Mpira wa Wanawake.

Amesema Mashabiki wanayo nafasi kubwa katika maendeleo ya Mpira wa Wanawake na kuwataka waweze kujitokeza kuunga mkono Ligi Kuu ya Wanawake pamoja na kuziunga mkono timu za Wanawake.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA TFF

BENKI YA KILIMO TANZANIA KUFUNGUA OFISI ZA KIKANDA KWA AWAMU

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)

Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma

Serikali imeeleza kuwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) inatekeleza Mpango wa Miaka Mitano (2017- 2021), wa kusogeza huduma karibu na wateja kwa kuanzisha ofisi za Kikanda katika Kanda ya Kaskazini, Kusini, Kati, Ziwa, Nyanda za Juu Kusini na Zanzibar kwa awamu.

Hayo yameelezwa Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), wakati akijibu maswali ya msingi ya Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Jacqueline Msongozi (CCM), aliyetaka kujua lini Serikali itapeleka Benki ya Kilimo katika Mkoa wa Ruvuma ili wananchi waweze kukopeshwa.

Aidha, Mhe. Msongozi alitaka kufahamu utayari wa Serikali kupunguza riba ya mikopo wanayokopeshwa Wakulima katika Benki hiyo.

Akijibu maswali hayo, Dkt. Ashatu Kijaji alisema kuwa hadi kufikia Juni 30, 2018 Ofisi ya Kanda ya Kati, Dodoma, itakuwa imefunguliwa ambayo pia itakuwa ni Makao Mkauu ya Benki hiyo.

“Baada ya ufunguzi wa ofisi ya Kanda ya Kati kukamilika Benki Itafanya uchambuzi wa fursa zilizopo Kikanda na hivyo kuchukua hatua na taratibu za kufungua ofisi nyingine kulingana na upatikanaji wa rasilimali fedha”, alisema Dkt. Kijaji.

Alisema kuwa Benki hiyo inatoa mikopo kwa kutumia mfumo wa makundi, kundi la kwanza wakulima wadogo wadogo kwa riba ya asilimia 8- 12, kundi la pili la miradi mikubwa ya kilimo kwa asilimia 12 – 16 kwa mwaka na kundi la mwisho ni mikopo ya ushirika ambapo riba yake inaendana na hali ya soko la matumizi ya mkopo.

Kuhusu kupunguza riba kwa wakopaji, Dkt. Kijaji alibainisha kuwa majadiliano ya kiwango cha riba yanaweza kufanyika kulingana na historia ya mkopaji.

SERIKALI YAANZISHA MPANGO WA KUTOA MAFUNZO KWA VIJANAKUKIDHI MAHITAJI YA VIWANDA VYA NGUO

Mhe. Charles J. Mwijage (Mb), Waziri wa viwanda, biashara na uwekezaji, akizungumza wakati akifungua mkutano wa wadau wa sekta ya pamba na mavazi katika halfa iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hazina- Mjini Dodoma leo 20 Aprili, 2018. Picha Zote Na Mathias Canal, NFRA
Baadhi ya wakuu wa mikoa inoyozalisha Pamba kwa wingi wakifatilia mkutano wa wadau wa sekta ya pamba na mavazi katika halfa iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hazina- Mjini Dodoma leo 20 Aprili, 2018.
Mgeni-Rasmi Waziri wa viwanda, biashara na uwekezaji, Mhe. Charles J. Mwijage (Mb), akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa sekta ya pamba na mavazi katika halfa iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hazina- Mjini Dodoma leo 20 Aprili, 2018.
Naibu waziri wa Kilimo, Mhe. Dkt Mary Mwanjelwa akijadiliana na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Antony Mtaka wakati wa mkutano wa wadau wa sekta ya pamba na mavazi katika halfa iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hazina- Mjini Dodoma leo 20 Aprili, 2018.
Waziri wa kilimo, Mhe. Dkt Charles Tizebawakati akifatilia kwa makini mkutano wa wadau wa sekta ya pamba na mavazi katika halfa iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hazina- Mjini Dodoma leo 20 Aprili, 2018.
Baadhi ya wadau wa sekta ya pamba wakifatilia kwa makini mkutano wa wadau wa sekta ya pamba na mavazi katika halfa iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hazina- Mjini Dodoma leo 20 Aprili, 2018.

Na Mathias Canal, Dodoma

Serikali kwa kushirikiana na viwanda vya nguo na mavazi imeanzisha mpango maalum wa kutoa mafunzo ya ushonaji kwa vijana kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya viwanda vya nguo.

Upatikanaji wa ujuzi wa aina hiyo utapunguza gharama kwa wawekezaji na kuongeza ufanisi katika uzalishaji. Vilevile, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kupitia msaada wa Gatsby Africa, kimeendelea kutoa mafunzo ya Shahada ya Teknolojia ya Nguo (Textile Degree) ambapo, mwaka 2016/2017, Chuo kilitoa wahitimu 44 ikilinganishwa na wahitimu 13 kwa mwaka 2015/2016. Lengo ni kuhakikisha kuwa kuna wataalam wa kutosha wa fani ya ubunifu na uzalishaji mavazi nchini.

Hayo yamebainishwa na Mhe. Charles J. Mwijage (Mb), Waziri wa viwanda, biashara na uwekezaji, wakati akifungua mkutano wa wadau wa sekta ya pamba na mavazi katika halfa iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hazina- Mjini Dodoma leo 20 Aprili, 2018
Alisema kuwa Tanzania ni moja ya nchi zinazozalisha pamba kwa kiasi kikubwa barani Afrika, ikiwa na zaidi ya wakulima 500,000 wanaolima pamba katika eneo linalokadiriwa kufikia hekta 412,000 katika mikoa 13 nchini. 

Sekta ya nguo na mavazi ni moja ya sekta za Kipaumbele katika kusukuma gurudumu la maendeleo nchini na inahusisha mnyororo mrefu wa uongezaji thamani kuanzia kuchambua pamba (ginneries); kusokota nyuzi (spinning); kuseketa vitambaa (weaving); kufuma vitambaa (knitting),kuchapa na kutia rangi (processing) na kushona mavazi (garments).
Aliongezaa kuwa Sekta hii ni moja ya sekta muhimu katika kutekeleza dhamira ya Serikali ya kuanzisha viwanda vinavyoajiri watu wengi kwa wakati mmoja. Sekta hii itawezesha kupunguza uingizaji wa nguo kutoka nje na kuongeza matumizi ya pamba inayolimwa nchini pamoja na malighafi nyingine zinazopatikana nchini kama vile magadi na gesi asilia.
Hata hivyo, Serikali imeendelea kuzishawishi taasisi za Umma kwa kuanzia majeshi na hospitali ili wanunue nguo na mavazi yanayozalishwa na viwanda vya ndani. 

 Lengo ni kuhakikisha kuwa utaratibu wa makusudi unawekwa kwa Taasisi za umma kutumia bidhaa zinazozalishwa na viwanda vyetu hapa nchini. Kwa mfano uvaaji wa fulana aina ya Polo Shirt kwa wafanyakazi wote katika siku moja ya wiki, na pia wanafunzi wote shule za msingi na sekondari kuvaa sare hizo. Inakadiriwa kuwa kuna jumla ya wanafunzi milioni 15 na wafanyakazi wa sekta zote za umma wanafika 25,000.
Mhe Mwijage alisema kuwa Utengenezaji wa fulana moja ya polo unakadiriwa kutumia wastani wa gramu 300 za pamba, sketi moja inakadiriwa kutumia gramu 600 za pamba, kaptula moja inakadiriwa kutumia gramu 600 za pamba. Hivyo jumla ya gramu 900 za pamba zitahitajika kutengeneza sare kwa mwanafunzi mmoja awe wa kike au wa kiume.
Kama ikikadiriwa kila mwanafunzi atavaa wastani wa sare (sketi & shati au kaptula na shati) mbili tu kwa mwaka gramu 1800 (sawa na kilo 1.8) za pamba zitahitajika kwa mwanafunzi mmoja, hivyo wastani wa kilo 27,000,000 (sawa na tani 27,000) zitahitajika kwa mwaka. 

Endapo mahitaji yaliyokusudiwa yakipitishwa tunategemea kwamba viwanda vya ndani vitakuwa na uwezo wa kutumia asilimia 17 ya pamba yote inayozalishwa nchini kwa mwaka. Hii itahamasisha uzalishaji wa pamba, kuongeza ajira na kuongeza kipato.
“Serikali inakamilisha taratibu za kuidhinisha ‘’ Blue Print’’ ambayo imeainisha maeneo ya kufanyia maboresho ya Kisera na Kisheria ili kuhamasisha uwekezaji katika Sekta mbalimbali za uchumi ikiwemo sekta ya pamba nguo na mavazi” Alikaririwa Mhe Mwijage

Pia,aliwashukuru Wadau wa sekta ndogo ya pamba, nguo na Mavazi kwa kazi kubwa wanayofanya katika uzalishaji, biashara na wadau wengine kwa michango yao katika kuendeleza sekta hii.

Mkutano huo umehusisha Wizari ya Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara wa Fedha na Mipango, Wizara ya Kilimo; Waheshimiwa Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge za Viwanda, Biashara na Mazingira; Bajeti; Kilimo, Mifugo na Maji; na Uwekezaji Mitaji ya Umma, Wakuu wa Mikoa; Makatibu Wakuu, Wawakilishi wa Sekta Binafsi, Maafisa wa Serikali na Taasisi za Serikali.

MAFURIKO JANGWANI KUPATIWA UFUMBUZI

Baadhi ya Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika(SADC) wakiwa kwenye majadiliano ya pamoja ambapo walizungumzia vipaumbele vinne, ikiwemo kuendeleza sekta ya viwanda pamoja na kukuza umoja wa kikanda katika sekta ya fedha na uwekezaji, mjini Washington DC Marekani.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akisikiliza majadiliano katika mkutano wa SADC, ambapo alishauri katika utaratibu wa uandaaji wa bajeti ni vyema Mawaziri wa Fedha wakashirikishwa. Kushoto kwake ni Gavava wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Florens Luoga, mjini Washington DC Marekani.
Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia kwa makini majadiliano kati yake na Benki ya Dunia ya namna yakumaliza tatizo la mafuriko eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam. Wapili kulia ni Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), kushoto kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar Bw. Khamis Mussa Omar na wa kwanza kulia kwake ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Florens Luoga na wa pili kulia kwake ni Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Bw. Charles Kichere mjini, Washington DC Marekani.
Ujumbe wa Benki ya Dunia ukiongozwa na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Somalia, Burundi na Malawi Bi. Bella Bird. (upande wa kulia mwenye scarf shingoni) wakijadiliana na ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) namna ya kutatua changamoto za mafuriko eneo la Jangwani, mjini Washington DC Marekani.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango)

Na. WFM- Washington D.C

Benki ya Dunia (WB) imekubali kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na athari za mafuriko zinazosababishwa na mvua kubwa zinazonyesha kila mwaka katika Jiji la Dar es Salaam na kuleta madhara makubwa hususan katika eneo la Jangwani jijini humo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) wakati akizungumza na ujumbe wa Benki ya Dunia ulioongozwa na Mkurugenzi wa Benki hiyo kwa nchi za Tanzania, Somalia, Burundi na Malawi Bi. Bella Bird, katika mikutano ya kipupwe inayoendelea mjini Washngton DC.

Dkt. Mpango amesema kuwa Benki ya Dunia imekubali kusaidia kukabiliana na mafuriko katika bonde la mto Msimbazi hasa katika eneo la kutoka Magomeni Mapipa kwenda Faya na tayari Benki hiyo imeanza zoezi la kutafiti eneo la Jangwani ili kuweza kuangalia namna nzuri ya kugharamia uboreshaji wa mifereji katika bonde la mto Msimbazi ili kumaliza kero hiyo kwa wananchi wa Dar es Salaam.

“Tumewaeleza Benki ya Dunia changamoto hii ambayo imekuwa inajirudia kila mara na kusababisha upotevu wa maisha ya watu, kusababisha kufungwa kwa barabara , watu kushindwa kwenda kazini na wanafunzi kushindwa kwenda shule, hivyo wameonesha nia ya kumaliza kero hii kwa wananchi “ Alisema Dkt. Mpango.

Amesema kuwa baada ya timu ya Benki ya Dunia kumaliza kufanya kazi yao kwa kushirikiana na Manispaa ya jiji la Dar es Salaam, Serikali inaamini njia ya kudumu itapatikana na kuondokana na tatizo hilo la mafuriko ya mara kwa mara katika eneo la Jangwani.

TUMBAKU MORO, UCHUKUZI SC ZANG'ARA MEI MOSI

 Kikosi cha timu ya soka ya Uchukuzi kikiwa pamoja na kocha wake Mkuu Zenno Mputa (kulia) na Mshauri wa timu Kennedy Mwaisabula (Mzazi), kinachoshiriki katika michuano ya Kombe la Mei Mosi inayofanyika katika viwanja mbalimbali mkoani Iringa. (Picha na Bahati Mollel wa TAA).
 Mshambuliaji Ramadhani Madebe (23 jezi nyekundu) wa Uchukuzi akiwa katika msitu wa wachezaji wa timu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Joseph Mlimi (2), Mohamed Koshuma (16) na Stephen Mgendi (12) katika mchezo wa michuano ya Mei Mosi uliofanyika kwenye jana uwanja wa Samora. Uchukuzi walishinda bao 1-0. (Picha na Bahati Mollel wa TAA).
 Kipa Stanley Mwalega (aliyesimama kushoto golini) wa Tanesco akijiandaa kudaka mpira uliopigwa na Emmanuel Kiwea (2) wa timu ya Tumbaku ya Morogoro wakati wakicheza mchezo wa mechi ya Kombe la Mei Mosi ulifanyika leo kwenye uwanja wa Samora mkoani Iringa.
Winga Salum Idd wa Tumbaku ya Morogoro (11) akikokota mpira kuelekea langoni mwa Tanesco wakati wa mchezo wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika leo kwenye uwanja wa Samora mkoani Iringa. Tumbaku walishinda mabao 2-0. (Picha na Bahati Mollel wa TAA).

Na Bahati Mollel-TAA, Iringa

TIMU za Tumbaku ya Morogoro na Uchukuzi zinaongoza katika mchezo wa soka kwa kushinda kwenye michezo yao ya michuano ya Kombe la Mei Mosi inayoendelea kwenye viwanja mbalimbali mkoani Iringa.

Tumbaku ipo katika kundi `A’ inaongoza kwa kuwa na pointi sita baada ya kushinda mechi mbili ikifuatiwa na timu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), RAS Iringa na Hifadhi ya Ngorongoro, ambazo zote hazina pointi.

Nayo Uchukuzi inaongoza kundi ‘B’ baada ya kushinda mchezo mmoja nakuwa na pointi tatu, wakifuatiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Geita Gold Mine (GGM) na NAO wote hawajakusanya pointi yeyote.

Katika hatua nyingine timu ya Tumbaku jana iliendeleza wimbi la ushindi kwa kuwafunga Tanesco magoli 2-0 katika mchezo uliofanyika leo kwenye uwanja wa Samora.

Washindi walipata bao lao la kwanza katika dakika ya 22 kwa njia ya penati lililofungwa Kelvin Makamba, baada ya mshambuliaji wao Issa Simbaliawa kufanyiwa madhambi na mlinzi wa Tanesco.

Bao la pili lilipachikwa katika dakika ya 32 na Ramadhani Shegodo aliyepata krosi safi kutoka kwa Idd Likasi.

Timu za soka zimegawanywa katika makundi mawili, ambapo kila kundi litatoa timu mbili zilizoshika nafasi za juu, na zitacheza hatua ya nusu fainali na fainali.

Mbali na soka michuano hiyo inashirikisha michezo ya netiboli, kuvuta kamba, karata, draft na bao kwa wanawake na wanaume.

Kesho timu ya kamba wanawake ya Tanesco itaumana na NAO, huku katika soka RAS Iringa watacheza na Hifadhi ya Ngorongoro katika uwanja wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Mkwawa, na timu ya Uchukuzi itakutana na Ngorongoro katika mchezo wa netiboli utakaofanyika Chuo Kikuu cha Katoliki (RUCU) na timu ya kamba ya wanawake ya Uchukuzi itavutana na MUHAS.

KAULI YA SERIKALI KUHUSU TRILIONI 1.5 BUNGENI DODOMA


UTANGULIZI

1.   Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 49 ya Kanuni za Bunge Toleo la Januari 2016, naomba kuwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu Kauli ya Serikali juu ya madai ya kutoonekana kwa matumizi ya shilingi trilioni 1.51 kwenye matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

2.   Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2012/13 hadi 2016/17, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango ilikuwa kwenye kipindi cha mpito cha miaka mitano ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa kuandaa hesabu za Serikali kwa kutumia mfumo wa Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu katika Sekta ya Umma (International Public-Sector Accounting Standards - IPSAS Accrual). Katika kipindi hicho, Serikali iliendelea kukusanya taarifa mbalimbali kwa kutumia mfumo huu ili kutuwezesha kutambua kikamilifu hesabu za mali, madeni pamoja na mapato yanayotokana na kodi. IPSAS Accrual ni mfumo wa kiuhasibu ambapo mapato yanatambuliwa baada ya muamala husika kukamilika na sio wakati fedha taslimu inapopokelewa; na matumizi yanatambuliwa wakati muamala wa matumizi umekamilika na sio wakati fedha inalipwa. Mfumo huu ni mzuri na una faida nyingi ikiwa ni pamoja na miamala ya Mapato na Matumizi kutambuliwa wakati husika na siyo wakati wa fedha taslimu inapopokelewa au kulipwa.

3.   Mheshimiwa Spika, matokeo ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa uandaaji wa hesabu kwa mfumo wa IPSAS Accrual umeiwezesha Serikali na taasisi zake kutoa taarifa za kina na zinazoonesha uwazi na uwajibikaji wa taasisi husika, hususan katika usimamizi wa mali na madeni ya taasisi. Kuongezeka kwa uwazi, kumewawezesha watumiaji wa hesabu kupata taarifa zinazowasaidia kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati.

4.   Mheshimiwa Spika, kutokana na matumizi ya mfumo huu wa viwango vya Kimataifa vya Uhasibu katika sekta ya umma, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu na Watanzania kwa ujumla kwamba hakuna fedha taslimu ya shilingi trilioni 1.51 iliyopotea au kutumika kwenye matumizi ambayo hayakuidhinishwa na Bunge. Hivyo basi, madai ya baadhi ya watu wasiolitakia mema Taifa letu na Serikali yetu ya Awamu ya Tano hayana msingi wowote wenye mantiki. Haya yanadhihirishwa na aya zifuatazo kwenye tamko hili la Serikali.

5.   Mheshimiwa Spika, taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imeeleza jumla ya mapato yote ya Serikali kwa mwaka 2016/17, yalikuwa shilingi trilioni 25.3 ambapo fedha hizi zinajumuisha mapato ya kodi, mapato yasiyo ya kodi, mikopo ya ndani na nje pamoja na misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.

6.   Mheshimiwa Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba, kuanzia mwaka 2016/17, Mamlaka ya Mapato Tanzania ilianza rasmi kuyatambua mapato kwa mfumo wa Accrual. Hivyo basi, kati ya mapato haya ya shilingi trilioni 25.3, yalikuwemo pia mapato tarajiwa (receivables) kama mapato ya kodi yenye jumla ya shilingi bilioni 687.3 pamoja na mapato ya kodi yaliyokusanywa kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya jumla ya shilingi bilioni 203.92 (transfer to Zanzibar).

7.   Mheshimiwa Spika, katika uandishi wa taarifa ya ukaguzi, CAG alitumia taarifa za hesabu na nyaraka mbalimbali ikiwa ni pamoja na Taarifa za Utekelezaji wa Bajeti (Budget Execution Report) ambapo hadi kufikia tarehe 30 Juni 2017, mapato yalikuwa jumla ya shilingi trilioni 25.3 na matumizi yalikuwa shilingi trilioni 23.79. Matumizi haya hayakujumuisha shilingi bilioni 697.85 zilizotumika kulipa dhamana na hati fungani za Serikali zilizoiva. Matumizi haya yalikuwa hayajafanyiwa uhamisho (re-allocation) wakati ukaguzi unakamilika. Hivyo basi, baada ya kufanya uhamisho jumla ya matumizi yote kwa kutumia Ridhaa za Matumizi (Exchequer issues) yalikuwa shilingi trilioni 24.4.


8.   Mheshimiwa Spika, kutokana na ufafanuzi huo, shilingi trilioni 1.51 zilizodaiwa kutoonekana kwenye matumizi ya Serikali zilitokana na mchanganuo ufuatao;

Maelezo
Shilingi Trilioni
Matumizi ya dhamana na hati fungani zilizoiva
0.6979
Mapato tarajiwa (Receivables)
         0.6873
Mapato ya kodi yaliyokusanywa kwa niaba ya Serikali ya Zanzibar
0.2039
Jumla
1.5891
Fedha iliyotolewa zaidi ya mapato (Bank Overdraft)
(0.0791)
Fedha zilizodaiwa kutoonekana kwenye matumizi
1.51
                                                                                       
9.   Mheshimiwa Spika, hii inamaanisha kwamba, baada ya kupunguza mapato ya Zanzibar ya shilingi bilioni 203.92 na kupunguza mapato tarajiwa ya shilingi bilioni 687.3, mapato halisi kwa mwaka 2016/17 yalikuwa shilingi trilioni 24.41. Aidha, baada ya kujumlisha matumizi ya dhamana na hati fungani zilizoiva za kiasi cha shilingi bilioni 697.85 kwenye matumizi ya shilingi trilioni 23.79 yaliyooneshwa katika Taarifa ya CAG, ridhaa za matumizi zilizotolewa zilikuwa shilingi trilioni 24.49 na kuleta ziada ya matumizi ya shilingi bilioni 79.07 ikilinganishwa na mapato. Kwa mchanganuo huu, ni dhahiri kwamba kwa mwaka 2016/2017 matumizi ya Serikali yalikuwa makubwa kuliko mapato kwa shilingi bilioni 79.09 ambazo ni Overdraft kutoka Benki Kuu ya Tanzania. Utaratibu wa kutoa fedha zaidi ya mapato (Overdraft facility) uko kwa mujibu wa kifungu cha 34 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006.

Hitimisho

10.              Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imepata mafanikio makubwa katika uandaaji wa Hesabu za Serikali kwa kutumia mfumo huo wa Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu katika Sekta ya Umma (IPSAS Accrual). Itakumbukwa kwamba, katika Afrika, Tanzania ndio nchi pekee iliyofanikiwa kwa kiwango kikubwa kuandaa hesabu kwa kuzingatia matakwa ya IPSAS na kufanikisha kuandaa hesabu za Majumuisho kwa kuzingatia mfumo huo.

11.               Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo haya ya Serikali, napenda kulitaarifa Bunge lako Tukufu na wananchi kwa ujumla kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ipo makini na haiwezi kuruhusu upotevu wa aina yoyote wa fedha za umma.  Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuona kwamba, kila mapato yanayokusanywa yanatumika ipasavyo na kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania.

12.              Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, na naomba kuwasilisha.

MAMA NI MUNGU WA PILI DUNIANI: AUNTY EZEKIEL


UNESCO YAWANOA MAFUNDI MITAMBO WA REDIO ZA JAMII 25

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), limeanza kutoa mafunzo ya siku saba kwa mafundi mitambo wa radio za jamii 25 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo katika utendaji kazi wao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Shirika hilo jijini Dar es salaam, mafunzo hayo yanagusa masuala yanayozunguka jamii namna ya kuyafanya kifanisi na kitaalamu ili kuweza kurusha matangazo yaliyomazuri kwa jamii ambayo yameanza Aprili 19 hadi Aprili 25 mwaka huu.

"Washiriki hawa wanatoka katika radio 25 za jamii zinazosaidiwa na shirika letu.Kubwa ni kuwapa mafundi mitambo hao elimu kuhusu namna ya kuifanya radio ya jamii kuwa bora wakati wa urushwaji wa matangazo kwa jamii husika,"imesema.

Imeongeza Unesco kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswis (SDC) husaidia radio za jamii na mtandao wa radio za jamii (TADIO).

Ufadhili huo umelenga kuhakikisha wananchi wa Tanzania hasa wale wa vijijini wanafanya uamuzi sahihi kuhusu maisha yao kwa kupata taarifa sahihi kutoka redioni.

Washiriki wanaofadhiliwa na SDC ni Nuru FM (Iringa), Pambazuko FM (Morogoro), Fadhila FM (Mtwara) Jamii Mtukwao FM (Mtwara), Loliondo FM (Arusha), Baloha FM (Shinyanga), Kahama FM (Shinyanga) Ileje FM (Songwe),Tripple A FM (Arusha) na Storm FM (Geita).

Pia Sengerema FM (Mwanza), Kwizera FM (Kagera), Dodoma FM (Dodoma), Kitulo FM (Njombe), Uvinza (Kigoma), Mpanda (Katavi), Pangani (Tanga), Boma (Kilimanjaro), Mazingira (Mara), Mtegani FM (Kusini Unguja),mkoani FM (Kusini Pemba), Micheweni FM (Kaskazini Pemba),Tumbatu FM (Kaskazini Unguja) na Ruangwa FM (Lindi).
Afisa Miradi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Rose Ngunangwa akifafanua jambo wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo mafundi mitambo wa radio za jamii 25 yaliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) yaliyoanza Aprili 19 hadi Aprili 25 mwaka huu.
Meneja wa Huduma za Ufundi kutoka TBC, Mhandisi Yusuph Afidhu akizungumza na washiriki kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo mafundi mitambo wa radio za jamii zilizopo Tanzania Bara na Zanzibar.
Mkuu wa Studio Redio ya TBC, Mhandisi Omary Salum akitoa mada kuhusu namna ya studio inavyobidi kuwa ili kuweza kurusha matangazo kistadi wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo mafundi mitambo wa radio za jamii 25 yaliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Baadhi ya mafundi mitambo wa radio za jamii wakifuatilia mada kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo kwa mafundi mitambo wa radio za jamii 25 yaliyofanyika katika ukumbi wa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

WAZIRI MKUU KUZINDUA MRADI WA KUONGEZA UWEZO WA KUHIFADHI NAFAKA TANZANIA JUMAMOSI 21 APRILI 2018

                                                                                                Na Mathias Canal, NFRA-Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) Tarehe 21 Apili 2018 atakuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa kuongeza uwezo wa uhifadhi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) katika dhifa itakayofanyika kwenye viwanja vya Ofisi za Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula zilizopo Mtaa wa Kizota eneo la Viwanda Mjini Dodoma.

Mradi huo utagharimu Dola za Kimarekani Milioni 55, ambao ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya Poland ikiwa ni sehemu ya kiasi cha Dola milioni 110 kilichotolewa kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, mikataba ya ujenzi ilianza kutekelewa tarehe 9 Disemba 2017 ambapo Mradi huo utatekelezwa na kampuni mbili za Kandarasi kutoka Poland ambazo ni (Feerum S.A na Unia Araj Realizacje Sp.o.o) huku msimamizi wa mradi ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa waandashi wa habari na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Bi Vumilia L. Zikankuba ameeleza kuwa Mradi huo utahusisha ujenzi wa vihenge vya kisasa, maghala ya kisasa, ujenzi wa ofisi na kutekelezwa katika maeneo nane ambayo ni (Babati)-Manyara, Dodoma, Makambako-Njombe, Mbozi-Songwe, Shinyanga, Songea-Ruvuma, Sumbawanga-Rukwa na Mpanda-Katavi.

Baada ya mradi kukamilika Wakala utakuwa umeongeza uwezo wa kuhifahi kwa 250,000 MT zaidi (vihenge vya kisasa 190,000MT na maghala 60,000 MT) jambo ambalo litakuwa chachu na mafanikio yenye tija katika kuunga mkono Juhudi za utendaji wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli.

Kupatikana kwa Mradi huo nchini ni jitihada za Serikali ambazo zitapelekea ukuaji wa uchumi nchini na kuchangia kuwezesha Tanzania ya viwanda ambapo kutawezesha maghala ya Wakala kuweza kuhifadhi akiba ya Chakula ambayo itaendana na mahitaji halisi ya dharura kulinganisha na ongezeko la watu nchini.

Hifadhi ya Chakula inayohitajika kukidhi mahitaji ya dharula kwa miezi mitatu ni zaidi ya tani 500,000 ukilinganisha na tani 150,000 iliyokuwa inahitajika miaka ya 2008 Wakala ulipoanzishwa.

Aidha, Zikankuba alisema kuwa technolojia itakayotumika katika ujenzi wa vihenge vya kisasa, itawezesha Wakala kupunguza gharama za uendeshaji; kuhifadhi chakula kwa muda mrefu zaidi; kupunguza upotevu wa zao la mahindi baada ya kuvuna (posthaverst loss), kuongeza soko la mahindi nchini na kuimarisha usalama wa nafaka inayohifadhiwa kwa kudhibiti sumukuvu (Aflatoxin) kwa mahindi yaliyohifadhiwa. Jitihada hizi zinalenga katika kuimarisha uwezo wa Taifa katika kuimarisha usalama wa chakula nchini.

TANZANIA KUNADI VIVUTIO VYA UTALII DUNIANI KUPITIA TAMASHA LA URITHI WA UTAMADUNI WA MABARA NCHINI UFARANSA

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla, Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha pili cha wadau wa utalii kutoka nchi mbalimbali zinazohusika na tamasha la ‘Urithi wa Utamaduni wa Mabara’ Jijini Dar es Saalam jana.

Tanzania ni miongoni mwa nchi 54 za bara la Afrika zitakazoshiriki katika tamasha la ‘Urithi wa Utamaduni wa Mabara’ linalotarajiwa kufanyika nchini Ufaransa katika mji wa ‘Cherbourg’ mwezi Julai mwaka huu.

Tanzania inashiriki tamasha hilo la kihistoria kwa mara ya kwanza ambapo itapata fursa ya kutangaza utamaduni wake na vivutio vya utalii vya mambo ya kale hivyo kuongeza idadi ya watalii na mapato.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha pili cha wadau wa utalii kutoka nchi mbalimbali zinazohusika na tamasha hilo Jijini Dar es Saalam jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla, alisema tamasha hilo litatoa fursa pana kwa nchi kutangaza vivutio vyake ikiwemo vile vya Zamadamu.

“Kimsingi tamasha hilo linatarajiwa kutoa fursa kwa Tanzania kutangaza vivutio vyake na hivyo kuvutia watalii wengi kuja nchini, kila nchi itapewa banda lake la kuonyesha vivutio vyake , Tanzania naamini inakuwa na vivutio vingi vyenye kupendeza watalii kama vile Zinjathropus, Ngoma za makabila mbalimbali pamoja na nyimbo.

“Baada ya tamasha hilo, kutakuwa na ongezeko kubwa la watalii nchini na ninaamini hata zile nchi ambazo hazina rekodi nzuri ya kuja Tanzania kwa wingi zilizopo Bara la Asia zitaanza kuja,’’. alisema Kigwangla.

Alisema tamasha hilo linalotarajiwa kuhusisha takriban nchi zote za bara la Afrika, zaidi limelenga kutangaza tamaduni na vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo katika mataifa yote yatakayoshiriki huku likitajwa kuwa tamasha bora na kubwa la utalii pengine kuliko matamasha mengine yote kutokana na kila nchi kujitokeza kuonyesha vivutio vinavyopatikana katika mataifa yao.

“Tanzania tunavyo vivutio mbalimbali tunavyotarajia kwenda kuvionyesha katika tamasha hilo, ukiacha vivutio vya mambo kale, tuna bonde la Olduvai Gorge na mengineyo, tunayoamini kuwa kupitia tamasha hilo tutaweza kuyatangaza na hivyo kuvutia watalii wengi kuja nchini” alisema Dkt. Kigwangalla.

Hata hivyo alisema baada ya kukamilika kwa tamasha hilo, Septemba mwaka huu hapa nchini kutakuwa na tamasha la ‘Urithi wa Mtanzania’ linalotarajiwa kufanyika kwa mara ya kwanza na litakuwa likifanyika kila mwaka kuadhimisha urithi wa Mtanzania.

Alisema tamasha hilo linalotarajiwa kufanyika kwa kipindi cha mwezi
mzima, pia litatoa fursa kwa kila wilaya kutangaza vivutio vyake, huku akizitaka kila wilaya kujiandaa na tamasha hilo, litakalotoa fursa pia kwa mikoa na wilaya hizo kukuza utalii wa maeneo yao.
Waziri Kigwangalla akisalimiana na baadhi ya wajumbe wa mkutano huo.
Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Asngya Bangu akiongoza zoezi la utambulisho.
  Baadhi ya washiriki wa mkutano huo kutoka nchi mbalimbali barani Afrika.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla, Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha pili cha wadau wa utalii kutoka nchi mbalimbali zinazohusika na tamasha la ‘Urithi wa Utamaduni wa Mabara’ Jijini Dar es Saalam jana.
Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Prof. Audax mabula akizungumza katika mkutano huo.
Picha ya pamoja ya Waziri Kigwangalla na washiriki wa mkutano huo.
Waziri Kigwangalla akifurahia jambo na baadhi ya washiriki wa mkutano huo.