UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni
ya 49 ya Kanuni za Bunge Toleo la Januari 2016, naomba kuwasilisha mbele ya
Bunge lako Tukufu Kauli ya Serikali juu ya madai ya kutoonekana kwa matumizi ya
shilingi trilioni 1.51 kwenye matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha
2016/2017.
2.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha
mwaka 2012/13 hadi 2016/17, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango ilikuwa
kwenye kipindi cha mpito cha miaka mitano ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa
kuandaa hesabu za Serikali kwa kutumia mfumo wa Viwango vya Kimataifa vya
Uhasibu katika Sekta ya Umma (International Public-Sector Accounting Standards
- IPSAS Accrual). Katika kipindi hicho, Serikali iliendelea kukusanya taarifa mbalimbali
kwa kutumia mfumo huu ili kutuwezesha kutambua kikamilifu hesabu za mali,
madeni pamoja na mapato yanayotokana na kodi. IPSAS Accrual ni mfumo wa kiuhasibu ambapo mapato yanatambuliwa
baada ya muamala husika kukamilika na sio wakati fedha taslimu inapopokelewa;
na matumizi yanatambuliwa wakati muamala wa matumizi umekamilika na sio wakati
fedha inalipwa. Mfumo huu ni mzuri na una faida nyingi ikiwa ni pamoja na
miamala ya Mapato na Matumizi kutambuliwa wakati husika na siyo wakati wa fedha
taslimu inapopokelewa au kulipwa.
3.
Mheshimiwa Spika,
matokeo ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa uandaaji wa hesabu kwa mfumo wa
IPSAS Accrual umeiwezesha Serikali na taasisi zake kutoa taarifa za kina na
zinazoonesha uwazi na uwajibikaji wa taasisi husika, hususan katika usimamizi
wa mali na madeni ya taasisi. Kuongezeka kwa uwazi, kumewawezesha watumiaji wa
hesabu kupata taarifa zinazowasaidia kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati.
4.
Mheshimiwa Spika,
kutokana na matumizi ya mfumo huu wa viwango vya Kimataifa vya Uhasibu katika
sekta ya umma, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu na Watanzania kwa ujumla
kwamba hakuna fedha taslimu ya shilingi trilioni 1.51 iliyopotea au kutumika
kwenye matumizi ambayo hayakuidhinishwa na Bunge. Hivyo basi, madai ya baadhi
ya watu wasiolitakia mema Taifa letu na Serikali yetu ya Awamu ya Tano hayana
msingi wowote wenye mantiki. Haya yanadhihirishwa na aya zifuatazo kwenye tamko
hili la Serikali.
5.
Mheshimiwa Spika, taarifa ya Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imeeleza jumla ya mapato yote ya
Serikali kwa mwaka 2016/17, yalikuwa shilingi trilioni 25.3 ambapo fedha hizi
zinajumuisha mapato ya kodi, mapato yasiyo ya kodi, mikopo ya ndani na nje pamoja
na misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.
6.
Mheshimiwa Spika, napenda kulitaarifu
Bunge lako Tukufu kwamba, kuanzia mwaka 2016/17, Mamlaka ya Mapato Tanzania
ilianza rasmi kuyatambua mapato kwa mfumo wa Accrual. Hivyo basi, kati ya mapato haya ya shilingi trilioni 25.3,
yalikuwemo pia mapato tarajiwa (receivables) kama mapato ya kodi yenye jumla ya
shilingi bilioni 687.3 pamoja na mapato ya kodi yaliyokusanywa kwa niaba ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya jumla ya shilingi bilioni 203.92 (transfer
to Zanzibar).
7.
Mheshimiwa Spika, katika uandishi wa taarifa ya ukaguzi, CAG alitumia taarifa za hesabu na
nyaraka mbalimbali ikiwa ni pamoja na Taarifa za Utekelezaji wa Bajeti (Budget
Execution Report) ambapo hadi kufikia tarehe 30 Juni 2017, mapato yalikuwa
jumla ya shilingi trilioni 25.3 na matumizi yalikuwa shilingi trilioni 23.79.
Matumizi haya hayakujumuisha shilingi bilioni 697.85 zilizotumika kulipa
dhamana na hati fungani za Serikali zilizoiva. Matumizi haya yalikuwa hayajafanyiwa
uhamisho (re-allocation) wakati ukaguzi unakamilika. Hivyo basi, baada ya
kufanya uhamisho jumla ya matumizi yote kwa kutumia Ridhaa za Matumizi
(Exchequer issues) yalikuwa shilingi trilioni 24.4.
8.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na ufafanuzi huo, shilingi trilioni 1.51
zilizodaiwa kutoonekana kwenye matumizi ya Serikali zilitokana na mchanganuo
ufuatao;
Maelezo
|
Shilingi Trilioni
|
Matumizi
ya dhamana na hati fungani zilizoiva
|
0.6979
|
Mapato
tarajiwa (Receivables)
|
0.6873
|
Mapato
ya kodi yaliyokusanywa kwa niaba ya Serikali ya Zanzibar
|
0.2039
|
Jumla
|
1.5891
|
Fedha
iliyotolewa zaidi ya mapato (Bank Overdraft)
|
(0.0791)
|
Fedha zilizodaiwa kutoonekana kwenye matumizi
|
1.51
|
9.
Mheshimiwa Spika, hii inamaanisha
kwamba, baada ya kupunguza mapato ya Zanzibar ya shilingi bilioni 203.92 na
kupunguza mapato tarajiwa ya shilingi bilioni 687.3, mapato halisi kwa mwaka
2016/17 yalikuwa shilingi trilioni 24.41. Aidha, baada ya kujumlisha matumizi ya dhamana na hati fungani zilizoiva za kiasi cha
shilingi bilioni 697.85 kwenye matumizi ya shilingi trilioni 23.79 yaliyooneshwa
katika Taarifa ya CAG, ridhaa za matumizi zilizotolewa zilikuwa shilingi
trilioni 24.49 na kuleta ziada ya matumizi ya shilingi bilioni 79.07
ikilinganishwa na mapato. Kwa mchanganuo huu, ni dhahiri kwamba kwa mwaka
2016/2017 matumizi ya Serikali yalikuwa makubwa kuliko mapato kwa shilingi
bilioni 79.09 ambazo ni Overdraft
kutoka Benki Kuu ya Tanzania. Utaratibu wa kutoa fedha zaidi ya mapato
(Overdraft facility) uko kwa mujibu wa kifungu cha 34 cha Sheria ya Benki Kuu
ya Tanzania ya mwaka 2006.
Hitimisho
10.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia
Wizara ya Fedha na Mipango imepata mafanikio makubwa katika uandaaji wa Hesabu
za Serikali kwa kutumia mfumo huo wa Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu katika
Sekta ya Umma (IPSAS Accrual). Itakumbukwa kwamba, katika Afrika, Tanzania ndio
nchi pekee iliyofanikiwa kwa kiwango kikubwa kuandaa hesabu kwa kuzingatia matakwa
ya IPSAS na kufanikisha kuandaa hesabu za Majumuisho kwa kuzingatia mfumo huo.
11.
Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo
haya ya Serikali, napenda kulitaarifa Bunge lako Tukufu na wananchi kwa ujumla
kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, ipo makini na haiwezi kuruhusu upotevu wa aina yoyote wa fedha za
umma. Dhamira ya Serikali ya Awamu ya
Tano ni kuona kwamba, kila mapato yanayokusanywa yanatumika ipasavyo na kwa
manufaa ya wananchi wa Tanzania.
12.
Mheshimiwa
Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, na naomba
kuwasilisha.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni