Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa hesabu Tanzania Bw. Ludovick Utouh, amekutana na uongozi wa Chama cha
Wananchi (CUF) kujadiliana juu ya masuala ya fedha ya chama hicho kwa kipindi
cha miaka mitatu, kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2012.
Akizungumza katika
kikao hicho kilichofanyika ofisi kuu za CUF Buguruni, Bw. Ludovick amesema ni
jambo la faraja kuona chama hicho kimeonesha njia kwa vyama vyengine, kikiwa cha
mwanzo kukaguliwa na chombo hicho.
Bw. Ludovick ambaye
aliongoza ujumbe wa ofisi ya Mdhibiti na Mkuguzi Mkuu wa hesabu, ameelezea
kuridhishwa na muendelezo wa masuala ya fedha ndani ya chama hicho, na kuahidi
kutoa ripoti kamili katika kipindi cha siku 21.
Kikao hicho pia
kilimuhusisha Katibu Mkuu wa CUF ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad.
Wakati huo huo Maalim
Seif amefanya mahojiano na kampuni ya Global Publishers Limited ya Dar es
Salaam, inayochapisha magazeti ya Uwazi, Champion, Risasi, Ijumaa na Amani.
Pamoja na mambo
mengine kampuni hiyo ilitaka kujua juu maendeleo ya chama hicho, pamoja na
mafanikio, changamoto na utendaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Kuhusu maendeleo ya
chama hicho Maalim Seif amesema chama hicho hakijafifia kama inavyodaiwa na
baadhi ya watu, na badala yake kimezidi kuimarika katika mikoa mbali mbali ya
Tanzania.
Amesema lengo kuu la
chama cha siasa ni kushika hatamu za dola, na kwamba tayari chama hicho
kimekuwa sehemu ya serikali katika serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
Akipoulizwa kuhusu
madai ya kukidhoofisha chama hicho kutokana na kushikilia wadhifa wa Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar akiwa pia ni Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif alisema
kazi kubwa ya Katibu Mkuu ni kusimamia utekelezaji wa majukumu ya chama ambayo
hufanywa na wasadizi wake wakiwezo naibu makatibu wakuu pamoja na wagurugenzi.
Hivyo amesema nafasi
hiyo haiathiri ufanisi wa chama hicho, na kamwe haiwezi kuwa sababu ya
kuzorotesha maendeleo ya chama, na kutoa mifano kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye
ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Dkt. Ali Mohd Shein ambaye ni Makamu
Mwenyekiti wa CCM Zanzibar.
Maalim Seif pia
alizungumzia juu ya suala la dawa za kulevya ambapo alisema ofisi yake ikiwa
imepewa jukumu hilo, imekuwa ikipanga mikakati ya kila aina kuona kuwa tatizo
hilo linadhibitiwa.
Hata hivyo amekiri
kuwepo ugumu wa kukabiliana na tatizo hilo kutokana na jiografia ya Zanzibar
ambayo imekuwa na njia nyingi zisizo rasmi, zinazofikiriwa kuingizwa dawa hizo
ukitoa viwanja vya ndege na bandari zinazotambulika.
Amesisitiza haja kwa
watendaji wa mamlaka za viwanja vya ndege na bandari kuwa waadilifu, na
kuepukana na vishawishi vinavyoweza kupelekea uingizaji wa dawa za kulevya
katika maeneo hayo.
Aidha amesema kwa
sasa wamekuwa wakiweka udhibiti katika maeneo hayo yaliyo rasmi, pamoja na
kusambaza elimu kwa vijana wakiwemo wanafunzi, juu ya athari ya dawa hizo.
Amehimiza
mashirikiano baina ya vyombo vya dola na wananchi katika kukabiliana na tatizo
hilo ambalo limekuwa likiwaathiri zaidi vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.
“Tatizo hili
halitomuathiri mtoto wa fulani tu bali tujue kuwa vijana wengi hata watoto wa
viongozi na matajiri wanaathirika, kwa hivyo kitu cha msingi ni mashirikiano
baina ya vyombo vyetu vya dola na wananchi”, alisisitiza Maalim Seif.
Hassan Hamad. (OMKR)




Hakuna maoni :
Chapisha Maoni