.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumanne, 20 Mei 2014

MAKAMU WA KWANZA WA RAIS ZANZIBAR, MAALIM SEIF KATIKA MAHAFALI YA MRADI WA ZEET

 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akikabidhi cheti kwa mwanafunzi Hamad Kombo Haji aliyehitimu mafunzo ya utalii, katika sherehe za mahafali na ufungaji wa mradi wa ZEET, kituo cha mafunzo ya amali Mkokotoni.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akihutubia, katika sherehe za mahafali na ufungaji wa mradi wa ZEET, kituo cha mafunzo ya amali Mkokotoni.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akikagua bidhaa za wajasiriamali katika kituo cha mafunzo ya amali Mkokotoni Zanzibar.
 

Mwakilishi wa taasisi ya SAZANI ASSOCIATES ya Uingereza Dr. Cathyrine, akizungumza katika sherehe za mahafali na ufungaji wa mradi wa ZEET, kituo cha mafunzo ya amali Mkokotoni.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akikagua bidhaa za wajasiriamali katika kituo cha mafunzo ya amali Mkokotoni Zanzibar. Hapa anaangalia umeme wa “solar” unaotengenezwa na vijana wa Wilaya ya Kaskazini “A” Unguja.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, wawakilishi wa mradi wa ZEET pamoja na baadhi ya wahitimu wa mafunzo ya utalii na ufundi umeme wa “solar”.
 

Baadhi ya washiriki katika sherehe za mahafali na ufungaji wa mradi wa ZEET, kituo cha mafunzo ya amali Mkokotoni. (Picha na Salmin Said, OMKR).

Na, Hassan Hamad (OMKR).
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema Serikali itaendelea kusimamia sera yake ya ajira ili kuhakikisha kuwa vijana wa Kizanzibari wanapewa kipaumbele katika nafasi za ajira.
Amesema mpango huo una lengo la kuwasaidia vijana wa Zanzibar kuweza kupata ajira katika sekta mbali mbali ikiwemo sekta ya utalii, hali itakayopelekea kupungua kwa tatizo la ajira kwa vijana wengi wanaohitimu masomo yao.
Mhe. Maalim Seif ametoa kauli hiyo katika sherehe za mahafali na ufungaji wa mradi wa kutoa elimu na mafunzo ya kuajirika Zanzibar (Zanzibar Enterprises and Employability Training-ZEET), zilizofanyika kituo cha mafunzo ya Amali 
Mkokotoni, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema ni ukweli usiopingika kuwa serikali haina uwezo wa kuwaajiri vijana wote wanaomaliza masomo, lakini imekuwa ikiwawezesha kwa kuwapatia mafunzo ya kuweza kuajirika na kujiajiri baada ya kumaliza mafunzo hayo.
Ameishukuru taasisi ya SAZANI ASSOCIATES pamoja na wafadhili wakuu wa mradi huo yaani COMIC RELIEF ya Uingereza, kwa kuweza kusimamia mradi huo wa miaka mitatu ambao amesema umepata mafanikio makubwa.


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amewahimiza wananchi wa Wilaya ya Kaskazini “A” kuutunza na kuuendeleza mradi huo ili uwe chaku ya maendeleo katika Wilaya hiyo na Taifa kwa Ujumla.
Mradi huo pamoja na mambo mengine umekuwa ukitoa mafunzo kwa wajasiriamali wa Wilaya ya Kaskazini “A” kwa fani za huduma na ukarimu pamoja na ufundi wa umeme wa kutumia nguvu za jua “Solar”.
Aidha amewapongeza waandaaji wa mradi huo kwa kuzingatia athari za kimazingira katika utekelezaji wa mradi huo, na kwamba maisha ya wanadamu yanategemea usimamizi bora wa mazingira.
“Sitoweza kuzungumzia kila kitu kilichopo hapa, lakini inaonekana muundo na mawazo ya kutengeneza mradi huu, yalikuwa ni ya kuona mbali, sababu kila ambacho kimefanywa, kwa vyovyote kimegusa mazingira na maisha endelevu. Ni hali ya kupigiwa mfano na wengine wanapaswa kujifunza kupitia kwenu”, alisisitiza Maalim Seif.
Amezishauri taasisi nyengine kuchukuwa juhudi za makusudi za kuendeleza vyanzo vya maisha endelevu, na kwamba Serikali itahakikisha kuwa kunakuwa na ufuatiliaji wa karibu, ili kuona kwamba kunakuwa na uwajibikaji wa hali ya juu katika kuiendeleza miradi hiyo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar pia alitumia fursa hiyo kuwatanabahisha wananchi za Zanzibar juu umuhimu wa kulinda na kuitunza amani iliyopo, kama msingi mkuu wa kujiletea maendeleo.
Amefahamisha kuwa bila ya Amani hakuna maendeleo yatakayopatikana, na kuwanasihi wananchi kuacha tofauti zao za kisiasa katika juhudi za kupiganiania maendeleo endelevu.
“Suala la amani ni lazima kwa maendeleo yetu, hivyo natoa wito kwa viongozi wa ngazi mbali mbali kusimamia kwa dhati suala la amani, na tofauti zetu za kisiasa zisigawanye Uzanzibari wetu, na wala tusifikirie kurudi tulikotoka”, alitanabahisha Maalim Seif.
Kuhusu suala la wajasiriamali, Maalim Seif ameitaka Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, kuwa karibu na wajasiriamali hao, ili kuhakikisha kuwa wanazalisha bidhaa zenye ubora unaostahiki, pamoja na kuwasaidia kutafuta masoko ya bidhaa zao ndani na nje ya nchi, na kuwahimiza kuzitumia ipasavyo fursa zinazojitokeza katika soko la pamoja la Afrika ya Mashariki.

Nae Mwakilishi wa taasisi ya SAZANI ASSOCIATES ya Uingereza Dr. Cathyrine amesema tayari vijiji ishirini vya Wilaya ya Kaskazini “A” vinanufaika na mradi wa umeme wa nguvu za jua kupitia ujuzi wa vijana wa Wilaya hiyo waliofunzwa kupitia mradi huo.
Aidha amesema mradi huo umeviwesha vikundi vipatavyo 30 vya wajasiriamali wa Wilaya hiyo, wakulima 150 na skuli 30 kwa kuwapatia mafunzo ya Afya na maisha endelevu.
Akitoa salamu kwa niaba ya Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mwalimu Mkuu wa kituo cha Mafunzo ya Amali Mkokotoni mwalimu Mkubwa Ibrahim Khamis amesema Mamlaka imeupokea mradi huo na itaendelea kushirikiana na wafadhili katika kuufanya kuwa endelevu.
Mamlaka hiyo imesema inawakarikibisha washirika wengine wa maendeleo kuweza kutoa mafunzo kwa vijana wengi zaidi, ili kuwawezesha vijana kuweza kujiajiri na hatimaye kupunguza tatizo la ajira nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “A” Bi. Riziki Juma Simai ameahidi kushirikiana na viongozi wa hoteli za Mkoa huo katika kuwatafutia vijana ajira, pamoja na kushirikiana na wajasiriamali kwa lengo la kusaidia upatikanaji wa soko la bidhaa zao.
Mwakilishi wa Jumuiya ya Labayka Zanzibar Hassan Jani Massoud, amewashukuru viongozi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja pamoja na viongozi wa mahoteli kwa ushirikiano walioutoa wakati wa utekelezaji wa mradi huo.
Pia ameishukuru Serikali kwa kuruhusu taasisi za kijamii kufanya kazi pamoja, na kwamba hatua hiyo inasaidia juhudi za kuikomboa nchi kutokana na tatizo la umaskini.
Mapema akisoma risala kwa niaba ya wahitimu hao, ndugu Maabadi Salum amesema, bado wanakabiliwa na tatizo la ajira, na kuiomba serikali kuwajengea mazingira bora ya kuweza kupatiwa ajira.
Kabla ya sherehe hizo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alipata fursa ya kutembelea maonyesho ya bidhaa mbali mbali zilizotayarishwa na wajasiriamali wa Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni