Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwashukuru wananchi na wadau mbali mbali waliojitolea kuchangia mfuko wa Chuo cha Elimu ya Biashara ambao umepangwa kutumika katika ujenzi wa majengo mapya ya chuo hicho.
Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Elimu ya Biashara Profesa Matthew Luhanga akimkabidhi kikapu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ambacho kimewekwa michango ya fedha kwa ajili ya kutunisha mfuko wa chuo cha Elimu ya Biashara.
Mwenyekiti wa Bodi ya chuo cha Elimu ya Biashara Profesa Matthew Luhanga akielezea malengo ya chuo hicho katika ujenzi wa majengo ya kisasa yatakayokidhi mahitaji ya wanafunzi.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Shilingi Milioni Mia Tano na Elfu Tisa { 500,009,000/- } zimechangwa na nyengine kutolewa ahadi na wakereketwa mbali mbali wa Sekta ya elimu kuchangia mfuko wa Chuo cha Elimu ya Biashara { CBE } kwa lengo la kujenga majengo mapya ya chuo hicho Jijini Dar es salaam.
Kati ya fedha hizo Shilingi Milioni 400,000,000/- pekee zimechangwa na wahadhiri, Wafanyakazi, Walimu na wanafunzi wa chuo hicho na shilingi Milioni 104,479,000/- zilizotolewa ahadi na washirika mbali mbali wa maendeleo ya Elimu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliongoza harambe maalum ya kuchangisha fedha hizo kwenye chakula cha usiku kilichoandaliwa na Uongozi wa Chuo hicho hapo Hoteli ya Serena Jijini Dar es salaam.
Washiriki wa chakula hicho walionekana kuhamasika vyema kuchangia mfuko huo baada kuelewa changamoto zinazokikabili chuo cha Elimu ya Biashara hasa uchakavu na ufinyu wa majengo ya chuo hicho sambamba na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewapongeza Wananchi na wadau mbali mbali nchini kwa utayari wao wa kuchangia sekta ya elimu hapa Nchini.
Balozi Seif alisema Serikali zote mbili ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar zimekuwa zikikabiliana na changamoto zinazotokana na sekta ya elimu.
Alisema upanuzi wa ubora wa elimu Nchini umekuwa ukifanywa ili kuwapa fursa wasomi kuvitumia vizuri vipaji vyao na hii inatokana na kipaumbele kilichowekwa ndani ya mpango wa maendeleo ambao sekta ya elimu imepewa nafasi pana.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi pamoja na Bodi ya Chuo cha Elimu ya Biashara { CBE } kwa malengo uliojiwekea kwenye mpango huo wa kukusanya shilingi Bilioni moja.
“ Kwa nini tusiendelee kuchangia maendeleo ya elimu sisi wenyewe badala ya nguvu nyingi kuzitumia kwenye harusi na mambo mengine ya hanasa “. Alisema Balozi Seif.
Alielezea faraja yake kutokana na mabadiliko makubwa ya mfumo wa elimu uliopo Tanzania uliopelekea kuongezeka kwa idadi ya vyuo vya elimu ya juu ambapo kwa sasa vimefikia 60.
Mapema Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Elimu ya Biashara Profesa Matthew Luhanga alisema ipo haja ya kuhamasishwa wananchi wajikite zaidi katika kuhakikisha kwamba watoto wao wanapata elimu ya juu.
Profesa Luhanga alisema asilimia 44% ya vijana kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 wahudumiwe ipasavyo katika kupatiwa elimu itakayowawezesha kujidumu kimaisha.
Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Chuo cha Elimu ya Biashara alieleza kwamba uharibifu mkubwa unaofanywa nchini unatokana na vitendo vya Vijana waliokosa elimu.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni