Na Shushu Joel, Busega
WITO umetolewa kwa wananchi wilayani Busega mkoani Simiyu hususani kwa kundi la vijana kujishughulisha na shughuli za ujasiriamali kwa kuanzisha viwanda vinavyotumia nishati ya umeme ili waweze kujiinua katika vipato vyao.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Eraston Mbwilo katika wilaya hiyo alipokwenda kujitambulisha kwa wananchi wa eneo hilo na watumishi wote katika wilaya hiyo ya Busega.
Mkuu huyo wa mkoa aliyasema hayo alipokutana na vijana waendesha pikipiki wa Nyashimo na kuwaambia kuwa, vijana walio wengi siku hizi wanapenda kuonekana watanashati na kushinda mitaani katika makundi mabaya ambayo hayawasaidii chochote.
Hivyo aliwataka vijana wilayani Busega kujiunga na vikundi vidogo vidogo vya ujasiriamali vinavyoweza kuwainulia kiuchumi na kuwanufaisha, na pia kuondokana na janga la umasikini kwa vijana.
Vijana wengine nchini wanapenda kucheza michezo michafu ikiwemo uchezaji wa kamali hivyo aliwatahadharisha vijana wa Busega kuwa katika makundi yasiyofaa katika jamii inayowazunguka na badala yake kuwa na makundi mazuri yaliyo na tija kwao ili waweze kupiga hatua Fulani katika sekta ya maendeleo.
Kwa upande wao vijana wa wilaya hiyo ya Busega ikiwakilishwa na mwenyekiti wa waendesha bodaboda walimwambia mkuu huyo wa mkoa kuwa mpaka sasa wao wanamiliki pikipiki ya kikundi waliyopewa na mbunge wao ambaye pia ni waziri wa mifugo na uvuvi Dk Kaman, mara baada ya risala hiyo fupi kwa mkuu wa mkoa maye aliwaambia atawapa shilingi laki tano ili waweze kutunisha mfuko wao.
Aidha aliwapa pongezi viongozi wote wa halmashaul ya Busega kwa ushirikiano wa dhati na mbunge wa jimbo hilo pamoja na wananchi katika kufanikisha suala la maendeleo yao ikiwemo ufanikishaji mkubwa wa maabara,Afya na barabara zinazopitika bila shaka yeyote ile wilayani humo.
Pia Mbwilo ameagiza mwezi ujao ni lazima mradi wa maji wilayani Busega ukamilike
Hata hivyo mkuu huyo wa mkoa alimtaka mkurugenzi wa halmashauli ya wilaya ya Busega kuweza kuwapa mikopo vijana walio na vikundi vya ujasiriamali.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni