Wa mwanzo kutoka kushoto ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Kenya Bwa Raila Odinga, Rais Mstaafu wa Zanzibar Bw. Rupiah Banda na Rais Mstaafu wa Zanzibar ambae ndie mwenyekiti wa Mkutano huo Dr. Amani Abeid Karume.
Picha na – OPMR – ZNZ.
Wakati umefika sasa kwa Dunia kujikita zaidi katika kukabiliana na migogoro isiyokwisha kwenye baadhi ya Mataifa inayozaa makundi ya wakimbizi kutokana na vita vinavyosababishwa na ukabila na mfumo mbaya wa siasa unaozalisha wanawake wajane na watoto yatima na kuwafanya kukosa haki zao za msingi za kibinaadamu katika kuishi maisha ya salama na furaha.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein alisema hayo wakati akiufungua Mkutanbo wa Kimataifa wa siku Mbili juu ya kukuza amani na maendeleo endelevu unaofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort nje kidogo ya Mjini Zanzibar na kuhuduriwa na Viongozi kadhaa wastaafu Barani Afrika wakiwemo pia wafanyabiashara maarufu.
Dr. Shein ambae Hotuba yake ilisomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Dunia imekuwa ikishuhudia ongezeko kubwa la akina Mama na Watoto walemavu wasio na hatia hasa katika Bara la Afrika wanaoendelea kuteseka kwenye kambi za wakimbizi kutokana na Nchi zao kukosa utulivu wa Kisiasa uliosababishwa na mapigano yasiyokwisha.
Alisema mfumko huu wa wakimbizi usipotafutiwa mbinu za kudhibitiwa mapema kwa kuandaliwa mazungumzo ya kusaka suluhu kati ya makundi yanayohitilafiana kutatua matatizo yanayojitokeza upo uwezekano mkubwa wa kuzalisha utitiri wa umaskini kwenye mataifa yaliyokumbwa na vita.
Rais wa Zanzibar alizitolea mfano Nchi zilizokumbwa na vita vya muda mrefu za Sudan, Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Burundi na Somalia ambazo Wananchi wao waliokimbia vita hivi sasa wengi kati yao wanaishi vilema pamoja na kukumbwa na umaskini uliopindukia mapaka.
“ Migogoro hii ya kivita na Kikabila isiyokwisha hivi sasa tayari imeshazalisha upweke kwa baadhi ya familia, umaskini, ulemavu na kubwa zaidi watoto wa wakimbi hao kukosa haki yao ya msingi ya kupatiwa Taaluma “. Alisema Dr. Shein.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mainduzi aliipongeza Jumuiya ya Afrika Mashariki { EAC },Taasisi ya Global Peace Foundation {GPF },Zayedesa, Cloud Media pamoja na IGAD kwa ubunifu wao wa kuandaa Mkutano huo wa Kimataifa na kupendekeza kufanyika Zanzibar uliolenga kutafuta mbinu za kuleta suluhu Kutokana na mizozo ya Kisiasa na Kikabila inayoendelea katika baadhi ya Mataifa ya Afrika.
Alisema kitendo cha Taasisi hizo kuamua Mkutano wao wa kukuza amani na Maendeleo endelevu kuufanyia Visiwani hapa umeipatia Heshima kubwa Zanzibar katika ramani ya Dunia.
Dr. Shein alielezea matumaini yake kwamba Mkutano huo utatoa mwanga kwa viongozi wa Mataifa ya Bara la Afrika ambao wapo wawakilishi wa Nchi zao kwenye Mkutano huo kuelekeza nguvu zao katika kuheshimu haki za Binaadamu pamoja na kudumisha utawala bora kwa lengo la kustawisha wananchi wao.
Mapema Mwenyekiti wa Mkutano huo wa kujadili Amani na Maendeleo endelevu Rais Mstaafu wa Zanzibar Dr. Aman Abeid Karume alisema Mataifa ya Bara la Afrika bado yana wajibu wa kuendelea kushirikiana katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi wake hasa wakimbizi.
Dr. Karume alisema ushirikiano huo uende sambamba na ushirikishwaji wa makundi ya Kidini yanayoonekana kuwa na nguvu katika Jamii jambo ambalo yakitumika vyema yanaweza kuwaongoza wafuasi wake kujiepusha na vishawishi vinavyozaa migogoro ya kisiasa na kikabila.
Mwenyekiti huyo wa Mkutano wa Amani na Maendeleo endelevu alishauri kuundwa kwa kamati za mitaa zitakazosaidia kutoa miongozo mizuri kwa ajili ya kukabiliana mapema na changamoto zitakazoibuka kwenye maeneo yanayowazunguuka.
Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dr. Richard Zezibera alisema Zanzibar itaendelea kuheshimika kama kituo cha Taaluma katika masuala ya kukabiliana na migogoro ya kisiasa na kikabila Duniani.
Dr. Richard alisema Jamii ya Kimataifa ilikuwa ikishuhudia jinsi Visiwa vya Zanzibar vilivyokuwa kiungo muhimu cha mawasiliano na kuwa kituo kikuu cha Biashara katika Karne ya 18 ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.
Katibu Mkuu huyo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki alizipongeza Taasisi za Global Peace Foundation, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na IGAD kwa juhudi zao zilizopelekea kufanikisha maandalizi ya Mkutano huo wa Kimataifa wa Amani na Maendeleo Endelevu.
Wakitoa Salamu zao kwenye Mkutano huo baadhi ya Viongozi wastaafu wa Mataifa ya Afrika walisema bado Nchi za Afrika zinapaswa kutatua matatizo yao wenyewe kwa kwenyewe kwa kutumia vikao vya usuluhishi watakavyoviunda.
Viongozi hao wastaafu wakiongozwa na Rais Mstaafu wa Zambia Bwana Rupiah Banda walisema kwamba wakati umefika kwa Wananchi wa Mataifa ya Bara hili kutambua kwamba chanzo cha umaskini uliokithiri katika baadhi ya Nchi hizo ni migogoro ya vita inayosababishwa na siasa chafu na kuendeza na ukabila.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni