Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo ametoa dola za Marekani
milioni 100 (US$ 100m, sawa na shilingi za Tanzania bilioni 220) kutoka
katika Mfuko Mkuu wa Kushughulikia Dharura wa Umoja wa Mataifa (CERF)
kwa shughuli za misaada katika maeneo tisa yenye dharura duniani na
yasiyo na fedha za kutosha.
Tanzania—ambayo kihistoria imepokea
mamilioni ya wakimbizi kutoka nchi jirani kwa miaka mingi—imetengewa
dola za Marekani milioni 11 (Sawa na shilingi za Tanzania bilioni 24)
kutoka katika kiasi hicho kwa lengo la kushughulikia mahitaji ya
wakimbizi kutoka Burundi.
Zaidi ya raia 126,000 wa Burundi
wamekimbilia nchini Tanzania tangu mwezi Aprili, 2015, kufuatia
machafuko ya kisiasa nchini humo. Huku tayari wakimbizi 64,000 kutoka
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) wakiwa tayari nchini.
Tanzania
hivi sasa ina zaidi ya wakimbizi 193,000. Kutokana na ukweli kwamba
takribani wakimbizi 1,500 wanawasili nchini kila wiki, inabashiriwa
kwamba huenda idadi jumla ya wakimbizi ikafikia 230,000 hadi mwisho wa
mwaka 2016.
Hali hii inasababisha changamoto nyingi hasa katika kutoa
msaada na kinga ya kutosha kwa
wakimbizi.
Mchango huu mkubwa kutoka CERF utakuwa muhimu
sana katika kutoa misaada ya kiutu kwa wakimbizi wa Burundi wanaoishi
katika kambi za Nyarugusu, Nduta na Mtendeli katika mkoa wa Kigoma,
Kaskazini Magharibi mwa Tanzania, na vilevile kwa jamii za wenyeji
ambazo zinahitaji kwa haraka huduma bora za maji safi, usafi wa kutosha,
matunzo ya afya, chakula na makazi.
Sehemu ya fedha hizo pia itatumika
kushughulikia mlipuko uliopo wa ugonjwa wa kipindupindu ambao umeathiri
mikoa 19 nchini. Fedha za CERF kwa hiyo zitasaidia kuhakikisha kwamba
maeneo muhimu zaidi katika dharura yanafanyiwa kazi na kwamba wakimbizi
wanapewa kinga na huduma za msingi.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni