.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatano, 1 Juni 2016

NISHATI YA UHAKIKA INAHITAJIKA KWA UKUAJI WA UCHUMI – PROFR. MUHONGO

MH1 
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akiongoza kikao kilichoshirikisha watendaji kutoka kampuni zinazojishughulisha na utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi za Statoil na ExxonMobil pamoja na Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC)
MH2
Meneja Mkazi wa Kampuni inayojishughulisha na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta ya Statoil Tanzania, Øystein Michelsen, (kushoto) akielezea shughuli zakampuni hiyo kwa Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kulia)
MH3
Meneja Mkazi wa Kampuni inayojishughulisha na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta ya Statoil Tanzania, Øystein Michelsen akisisitiza jambo katika kikao hicho.
MH4
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (mbele) akiongoza kikao kilichoshirikisha watendaji kutoka kampuni zinazojishughulisha na utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi za British Gas (BG), Ophir, Pavilion pamoja na Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) 

 

                                                                               Na Greyson Mwase, Dar es Salaam

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amesema kuwa ili Tanzania iweze kuwa nchi ya viwanda, nishati ya uhakika inahitajika na kutaka makampuni kuwekeza katika uzalishaji wa umeme unaotokana na gesi.

Profesa Muhongo aliyasema hayo jijini Dar es Salaam katika nyakati tofauti alipokutana na watendaji wa kampuni zinazojishughulisha na Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi pamoja na wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) lengo likiwa ni kupokea taarifa ya maendeleo ya miradi mbalimbali ya makampuni hayo.

Kampuni hizo zinazofanya kazi kwa kushirikiana na Shirika la TPDC ni pamoja na British Gas (BG), Ophir, ExxonMobil na Statoil.

Profesa Muhongo alisema kuwa hakuna nchi yoyote duniani iliyopiga hatua kimaendeleo bila kuwa na nishati ya uhakika ya umeme na kuwataka wawekezaji kuchangamkia fursa kupitia gesi nyingi iliyogunduliwa.

Alitaja maeneo yanayohitaji uwekezaji katika kuzalisha umeme kwa kutumia gesi kuwa ni pamoja na Mtwara, Lindi, Somanga Fungu, na Mkuranga

Aliongeza kuwa viwanda 37 pamoja na vya sementi vinahitaji gesi na kusisitiza kuwa iwapo sekta ya gesi itatumiwa ipasavyo inaweza kuchangia nchi kupiga hatua na kuingia katika kundi la nchi zenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 kama Dira ya Maendeleo ya Taifa inavyosema.

Wakati huo huo Profesa Muhongo, aliwataka watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake kufanya kazi kwa kasi ili kuendana na kasi ya uwekezaji katika shughuli za utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta.

“Sekta ya gesi na mafuta ambayo ni mpya inahitaji umakini na kasi ili kuvutia wawekezaji zaidi,” alisisitiza Profesa Muhongo.

Akizungumzia mikakati ya serikali katika kuzalisha wataalam katika masuala ya mafuta na gesi Profesa Muhongo alisema kuwa serikali imekuwa ikitoa ufadhili kwa wanafunzi katika ngazi za shahada za uzamili na uzamivu katika vyuo vilivyopo nje ya nchi vyenye uzoefu katika fani hiyo, pamoja na uanzishwaji wa programu hizo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo cha Madini.

Alisema kuwa mpaka sasa kuna idadi ya takribani wanafunzi 98 waliohitimu masomo hayo na kuziomba kampuni hizo kuajiri wataalam hao ili wawe na mchango mkubwa kwenye sekta ya gesi.

“ Nia ya Serikali ni kuwa na wataalam wazawa ambao watanufaika kupitia uchumi wa gesi kwa kufanya kazi katika viwanda vya kuchakata gesi na kuzalisha umeme unaotokana na gesi,” alisema Profesa Muhongo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) Dk. James Mataragio alisema kuwa shirika hilo limekuwa likishirikiana na kampuni hizo katika hatua zote muhimu hususan katika kiwanda cha kuchakata gesi asilia kimiminika (Liquefied Natural Gas) na kuongeza kuwa mpaka sasa eneo kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda limeshapatikana.

Alisema kuwa, Tanzania inatarajia kuwa kitovu kikuu cha gesi barani Afrika kwani gesi nyingi itakayozalishwa itauzwa katika nchi nyingine.

Aliongeza kuwa nchi kama Uganda, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo na Zambia zimeonesha nia ya kuhitaji gesi kwa ajili ya kuzalisha nishati ya uhakika kwa kuwa nchi hizo zinatumia maji kuzalisha umeme ambapo uzalishaji wake hupungua hususan wakati wa kiangazi kutokana na kupungua kwa kina cha maji.

Naye Meneja Mkazi wa Kampuni ya Statoil Tanzania, Øystein Michelsen, alisema kuwa kampuni yake ipo tayari kushirikiana na Serikali kuhakikisha kuwa miradi yake inakamilika kwa wakati.

Alisema tangu kampuni hiyo kuanza shughuli zake nchini, imekuwa ikishirikiana na Serikali kwa kutoa ufadhili wa masomo katika masuala ya gesi na mafuta nje ya nchi kwa wanafunzi wanaofanya vizuri.

Aliongeza kuwa kampuni ya Statoil imekuwa ikitoa elimu ya ujasiriliamali kwa wakazi wa mkoa wa Mtwara ili waweze kushiriki katika uchumi wa gesi kupitia utoaji wa huduma zake kwa Kampuni hiyo.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni