.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Alhamisi, 2 Juni 2016

PROF NTALIKWA AZINDUA BODI YA STAMICO, AITAKA KUHAKIKISHA INAENDESHWA KWA FAIDA

sta1 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Prof. Justin Ntalikwa (mbele) akiongoza kikao cha uzinduzi wa Bodi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) uliofanyika jijini Dar es Salaam.
sta2
Kaimu Kamishna wa Madini Nchini Mhandisi Ally Samaje akizungumza katika kikao cha uzinduzi wa Bodi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) uliofanyika jijini Dar es Salaam
sta3
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya madini Prof James Mdoe, akielezea historia ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) katika uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam.
sta4
Baadhi ya wajumbe wa Bodi Mpya ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) wakifuatilia kwa makini hotuba ya uzinduzi wa bodi hiyo iliyokuwa inatolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Prof. Justin Ntalikwa.(hayupo pichani).
sta5
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Prof. Justin Ntalikwa (mbele kulia) akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Balozi Alexander Muganda, (mbele kushoto) mara baada ya uzinduzi wa bodi hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam.
sta6
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Prof. Justin Ntalikwa (mbele kulia) akimkabidhi vitendea kazi mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dk. Lightness Mzava, (mbele kushoto) mara baada ya uzinduzi wa bodi hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam
sta7
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Prof. Justin Ntalikwa ( wa tatu kutoka kushoto waliokaa mbele) Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya madini Prof James Mdoe ( wa pili kutoka kushoto waliokaa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) mara baada ya kumalizika kwa uzinduzi huo.
 

                                                                                 Na Greyson Mwase, Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Prof. Justin Ntalikwa amezindua bodi ya wakurugenzi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na kuitaka bodi hiyo kuhakikisha kuwa shirika hilo linaendeshwa kibiashara na kuchangia katika ukuaji wa sekta ya madini.

Bodi hiyo iliyoteuliwa hivi karibuni na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo inaundwa na wajumbe watano ambao ni pamoja na Abdalah Musa, Dkt. Coretha Komba, Felix Maagi, Dkt. Lightness Mnzava, John Seka chini ya Mwenyekiti wake Balozi Alexander Muganda.



Profesa Ntalikwa alisema kuwa STAMICO ni Taasisi ya Serikali iliyopewa jukumu la kushiriki katika uwekezaji kwenye sekta ya madini kwa niaba ya serikali hivyo bodi ina wajibu mkubwa wa kusimamia shirika kwa manufaa ya taifa kwa kuhakikisha kuwa miradi yote iliyo chini ya shirika hilo inaendelezwa na kusimamiwa ipasavyo ili kuipatia Serikali manufaa mbalimbali ikiwepo gawio katika migodi ya ubia.

Aliendelea kusema kuwa kwa sasa STAMICO inaiwakilisha serikali katika miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mgodi wa Tanzanite unaomilikiwa kwa ubia kati ya Tanzanite One Mining Limited asilimia 50 na STAMICO asilimia 50; Mgodi wa Dhahabu wa Buckreef unaomilikiwa kwa ubia wa STAMICO kwa asilimia 45 na TANZAM2000 kwa asilimia 55.

Alitaja miradi mingine kuwa ni pamoja Mgodi wa STAMIGOLD wa Biharamilo unaomilikiwa kwa asilimia 100 na kampuni tanzu ya STAMIGOLD; Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira kwa asilimia 100 na Mradi wa Dhahabu wa Buhemba kwa asilimia 100.

Miradi mingine ni ya ununuzi wa madini ya bati (tin) kupitia kampuni tanzu ya Kyerwa Tin Company Limited na miradi ya utafutaji wa madini kwenye leseni mbalimbali za utafutaji wa madini zipatazo 49 zinazomilikiwa na shirika.

Aliongeza kuwa shirika linatoa huduma za uchorongaji na ushauri kwenye masuala ya madini pamoja na kusaidia wachimbaji wadogo hasa kwenye masuala ya kiufundi.

Alisisitiza kuwa kutokana na miradi mikubwa ya STAMICO, bodi ina kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa miradi yote ya shirika hilo inaendelezwa kwa faida

“Katika kusimamia shirika, mtazamo unatakiwa uwe ni wa kujiendesha siku za usoni kutokana na kuendesha miradi yenye faida na kuleta gawio serikalini. Alisema Prof. Ntalikwa

Aliendelea kusema kuwa ni vyema shirika liendeshwe kwa mtizamo wa kibiashara ili liweze kushindana na wadau wengine wanaowekeza katika sekta ya madini na kuleta manufaa yenye tija kwa taifa.

Aliwataka wajumbe wa bodi hiyo kupitia sera, sheria na miongozo mbalimbali katika sekta ya madini ili waweze kuisimamia STAMICO kwa ufanisi pamoja na kuhakikisha kuwa mikataba mbalimbali ambayo shirika linaingia inakuwa ni yenye manufaa.

Alisisitiza kuwa pale inapowezekana bodi inatakiwa kuboresha mikataba iliyopo kwa kukaa na wabia ili pande zote ziweze kunufaika na manufaa yatokanayo na miradi husika.

Wakati huohuo akizungumza katika uzinduzi huo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya madini Prof James Mdoe alisema kuwa STAMICO ina historia ndefu tangu kuanzishwa kwake miaka ya 1970 ambapo lilielekea kufa lakini lilirudi kwenye hadhi yake mwaka 2013

Alisema kuwa shirika la STAMICO likisimamiwa ipasavyo, linaweza kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia sekta ya madini.

“ Shirika hili lina miradi mingi na madini yapo mengi ambapo ninaamini kuwa iwapo itasimamiwa ipasavyo shirika lina mchango mkubwa sana wa kuifanya sekta ya madini kuchangia kwa asilimia kubwa katika pato la taifa,” alisema Prof. Mdoe.

Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo Balozi Alexander Muganda, akizungumza mara baada ya uzinduzi huo, alisema kuwa anamshukuru Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo kuwa na imani na bodi hiyo na kuahidi kufanya kazi kwa bidii katika kuhakikisha kuwa shirika hilo linapiga hatua kubwa katika mchango wake kwenye pato la taifa.

Alisema kuwa bodi yake imejipanga kuhakikisha kuwa shirika linasimamiwa kwa ufanisi mkubwa ili STAMICO iweze kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni