.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Ijumaa, 3 Juni 2016

WAFANYAKAZI TAA WAFANYA USAFI KIGILAGILA RELINI DAR ES SALAAM

Wakazi wa Mitaa ya Kigilagila Relini na Vituka wakiwa pembeni ya kibao kinachokataza utupaji wa taka, katika eneo la nyuma ya Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), mara baada ya kumaliza kufanya usafi. Juni 5 ni Siku ya Mazingira Duniani.
Mkuu wa Kitengo cha Mazingira cha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Bw. Jofta Tuimanywa (aliyenyoosha mkono), akisisitiza jambo kwa wafanyakazi wenzake, wakati wakifanya usafi kwa kushirikiana na wakazi wa mitaa ya Kigilagila Relini na Vituka kwenye eneo la nyuma ya uzio wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA). Juni 5, 2016 ni Siku ya Mazingira Dunia
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Laurent Mwigune (mwenye suti) jana akishiriki zoezi la kufanya usafi maeneo mtaa wa Kigilagila Relini, ikiwa ni muendelezo wa zoezi la usafi kuelekea Siku ya Mazingira Duniani, Juni 5, 20916

Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Paul Rwegasha (mbele anayetzama kamera), akizungumza na wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), na Wakazi wa Mitaa ya Kigilagila Relini na Vituka, mara baada ya kumaliza kufanya usafi nyuma ya ukuta wa JNIA, ikiwa ni muendelezo wa kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, Juni 5, 2016.
  Wakazi wa Mitaa ya Kigilagila Relini na Vituka wakiwa wanashirikiana na Wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kufanya usafi eneo la nyuma ya Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA). Juni 5 , 2016 ni kilele cha Siku ya Mazingira Duniani
Antony Kipobota wa TAA (katikati mwenye shati la mistari) akishirikiana na wafanyakzi wenzake kuzoa taka ikiwa ni mwendelezo wa kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, Juni 5, 2016. Kaulimbiu Kitaifa ni Tuhifadhi vyanzo vya Maji kwa uhai wa Taifa letu.


KAIMU Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Paul Rwegasha amehimiza usafi maeneo yanayozunguka kiwanja hicho, ili kuepusha kuzaliana kwa ndege wanyama wa aina mbalimbali.

Bw. Rwegasha aliyasema hayo wakati akimwakilisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), Mhandisi George Sambali jana wakati wa kufanya usafi wa mazingira ulioongozwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Bw. Laurent Mwigune kwa wafanyakazi wa TAA kushirikiana na wakazi wa mtaa wa Kigilagila Relini ikiwa ni muendelezo kuelekea kilele cha Siku ya Mazingira Duniani, Juni 5, 2016, alisema uchafu unachangia ongezeko la ndege wanyama ambao ni hatari kwa ndege za abiria.

“Ndugu zangu tusiruhusu mazingira yetu yakawa machafu, kwani ni hatari kubwa kwa sisi kiwanja cha ndege, kwani ndege mnyama akiingia kwenye injini ya ndege ya abiria atasababisha hasara kubwa. Hivyo tujitahidi kufanya mazingira yetu yawe safi ili ndege kama kunguru na wengine wasizaliane hapo,” alisema Bw. Rwegasha.

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo iliyotolewa Kitaifa na Mhe January Makamba , Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ni Tuhifadhi Vyanzo vya Maji kwa Uhai wa Taifa letu.

Alimtaka Mwenyekiti wa Mtaa wa Kigilagila Relini na Vituka kuhakikisha dampo lisilo rasmi lililoanzishwa karibu na ukuta wa JNIA linaondolewa haraka, na waweke ulinzi kuzuia utupaji wa taka eneo hilo.

Aidha alisema TAA imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na majirani zake wanaozunguka JNIA, ili kuweka mazingira hayo katika hali ya usalama na usafi, lakini bado wapo wakazi wachache wanaosababisha uhusiano huo kulegalega kwa kufanya vitendo vya kutupa taka hovyo.

Alifafanua zaidi kuwa TAA inaendelea na zoezi la kufyeka vichaka vilivyozunguka JNIA, ili kuzuia uhalifu wa watu wabaya kutumia mwanya huo kuruka uzio na kuingia ndani ya kiwanja hicho.

“Sisi hatutanii tena tunaagiza hili dampo liondoke na tutaweka mabango ya kuzuia utupaji wa taka hapa, na Wenyekiti tunaomba mhakikishe mnawakamata wale wote watakaokiuka agizo hilo na tutawachukulia hatua za kisheria,” alisema Bw. Rwegasha.

Naye Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Kigilagila, Bi. Janeth Shepea alishukuru Menejimenti ya TAA kwa kujitoa kushiriki kwenye usafi wa mazingira. Aliwataka wakazi wa mitaa iliyo karibu na JNIA kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzake na endapo wataona wanaotupa taka maeneo hayo, basi afuate sheria kwa kumfikisha serikali ya mtaa ili hatua stahiki zichukuliwe.

“Ndugu zangu tuchukue kauli ya mkuu wetu wa Mkoa, Mheshimiwa Paul Makonda kuwa Wana Dar es Salaam tukatae uchafu, na ukimkuta mtu kabeba fuko tumsimamishe na kumhoji amebeba nini na kama ni taka ukiwa ni Mwananchi unaruhusiwa kumpeleka Serikali ya Mtaa na huko hatua zitachukuliwa, uchafu unaleta magonjwa ya kuambukiza kikiwemo kipindupindu,” alisema Bi. Shepea.

Awali Meneja Usalama wa TAA, Bw. Thomas Kimata aliwataka wananchi kuwa na mazoea ya kufanya usafi na kuacha kutupa taka jirani na ukuta wa uwanja huo kwani kufanya hivyo kunaziba mifereji na kuzuia maji kupita na kujaa ndani ya maeneo ya kiwanja hicho, hali ambayo inaweza kusababisha athari.

“Tumeamua kufanya usafi katika eneo hili ikiwa ni sehemu ya kuelimisha jamii umuhimu wa usafi na wasiendelee kutupa taka eneo hili, kwani itasaidia kuwaepusha na magonjwa ya mlipuko,” alisema Bw. Kimata.

Naye Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Vituka, Bi. Mary Jailos, alisema zoezi hilo la usafi ni endelevu na litakuwa likifanyika mara kwa mara ili kuhakikisha wananchi wa eneo hilo wanaishi katika mazingira yenye usafi.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA SHERIA NA MAHUSIANO TAA


Hakuna maoni :

Chapisha Maoni