WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia Oktoba mwaka huu, Serikali imekwishapeleka zaidi ya sh. bilioni 177 kwenye halmashauri mbalimbali nchini ili kutekeleza miradi ya maendeleo.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Novemba 3, 2016) Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Bibi Munde Tambwe aliyetaka kupata kauli ya Serikali kuhusu ucheleweshwaji wa fedha za bajeti ya maendeleo katika halmashauri mbalimbali nchini.
“Kwa kuwa Serikali ina mifumo, miongozo, sheria na taratibu za kupeleka fedha kwenye halmashauri mara baada ya kikao cha bajeti. Mheshimiwa Waziri Mkuu unatoa kauli gani kuhusu ucheleweshwaji wa fedha hizo katika halmashauri nchini zikiwemo za mkoa wa Tabora? Alihoji Mheshimiwa Munde.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu amesema: “Baada ya Bunge kuridhia na kutoa mamlaka ya matumizi ya fedha, Serikali ilianza kujiridhisha uwepo wa mfumo sahihi ya makusanyo na mapato na matumizi yake. Ni kweli kwamba Serikali yetu baada ya kikao cha bajeti inawajibika kutekeleza maamuzi ya Bunge kwa kupeleka fedha zilizopangwa.”
Waziri Mkuu amesema Serikali ilianza kupeleka watumishi watakaosimamia ukusanyaji mapato katika halmashauri zote nchini. Kutathmini miradi yote iliyoanza ambayo haijaendelezwa pamoja na mipya ili kutambua thamani na kisha kupeleka fedha.
Amesema Serikali itaendelea na upelekaji wa fedha kwenye halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo. Amezisisitiza halmashauri hizo kuendelea kukusanya mapato ndani ili kuongezea bajeti kwa fedha wanazopelekewa na watumie mfumo wa kielektroniki ili kudhibiti mapato hayo.
Aidha, Waziri Mkuu amezitaka halmashauri zote nchini zihakikishe fedha zinazopelekwa katika maeneo yao zinatumika kama ilivyokusudiwa kwa miradi husuka. Amewasihi Wabunge wafuatilie na wasimamie matumizi ya fedha hizo ili miradi iliyopangwa iweze kukamilika.
Wakati huo huo; Waziri Mkuu amesema Serikali haijafilisika na kuhusu suala la mfuko wa jimbo bado unatambulika na fedha zitapelekwa kwenye majimbo na wabunge watajulishwa kiasi kilichopelekwa ili waweze kuratibu miradi yao ya maedndeleo.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la mbunge wa jimbo la Ukonga Mheshimiwa Mwita Waitara aliyetaka kupatiwa kauli ya Serikali kuhusu kutopelekwa kwa fedha za mfuko wa jimbo.
Pia Mheshimiwa Waitara alilalamikia kitendo cha jimbo lake kutengewa fedha kidogo katika mgawo wa mfuko wa jimbo ambazo ni sh. milioni 16 licha ya kuwa na wananchi wengi huku jimbo la Segerea alilosemma lina watu wachache likitengewa sh. milioni 33. Ameiomba Serikali ingalie upya ugawaji huo kulingana na mazingira ya jimbo husika.
Waziri Mkuu amesema kumejitokeza matatizo kwenye halmashauri zenye majimbo zaidi ya moja na Serikali inaendelea kufanya sensa kutambua idadi ya wananchi kwenye majimbo hayo ili itakapopeleka fedha iweze kuzingatia idadi hiyo na kuwawezesha wabunge kupanga miradi ya maendeleo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
ALHAMISI, OKTOBA 3, 2016
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni