.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Ijumaa, 13 Januari 2017

MAKAMU WA RAIS, SAMIA SULUHU HASSAN AONGOZA KIKAO CHA KUJADILI MUUNGANO

Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu akiongoza Kikao cha Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya MapinduzI ya Zanzibar kuhusu masuala ya Muungano kilichofanyika kwenye ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi mjini Zanzibar, Januari 13, 2017.

Kikao cha kamati ya pamoja ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu masuala ya Muungano kimekutana kimekutana chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan.

Wajumbe wa Kikao hicho ambao ni Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Manaibu Makatibu Wakuu , Watendaji na baadhi ya Wataalmu wa pande zote mbili za Tanzania walikutana katika Ukumbi wa Mikutano wa Baraza la Wawakilishi wa zamani uliopo Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Akiwasilisha Taarifa ya Maazimio ya Kikao cha Mawaziri wa SMT na SMZ Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania anayeshughulikia Mazingira na Muungano Mh. Januari Makamba alisema kikao hicho kilijadili Agenda 10 na Mada Mbili.

Mh. Makamba alisema moja ya miongoni mwa agenda Kuu za Vikao hivyo ni ile ya chimbuko la changamoto za Muungano ambazo nyingi zilizokuwa zikileta kero upande mmoja wa Muungano zimeshapatiwa ufumbuzi.

Alisema ushiriki wa wataalamu pamoja na watendaji waandamizi wa pande mbili za Muungano katika vikao vya kujadili changamoto zinazolalamikiwa na sehemu zote husika kuanzia ngazi ya chini na kuwasilishwa kwa Makatibu Wakuu na hatimae Mawaziri wa pande hizo umesaidia kupunguza kero hizo.

Waziri Januari Makamba alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na usajili wa vyombo vya moto, Gharama za deni la Tanesco kwa Zeco, utumishi wa wafanyakazi wa Zanzibar kwa Taasisi za Muungano, uvuvi wa bahari kuu pamoja na Zanzibar kutofaidika na miradi ya Afrika Mashariki.

Alieleza kwamba yapo masuala ambayo kimsingi yahitaji matayarisho ya kubadilishwa kwa Sheria kwenye Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania baadaye yaridhiwe na Baraza la Wawakilishi akilitolea mfano lile la Uvuvi wa Bahari Kuu.

Akichangia kwenye kikao hicho Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa Kassim ameiagiza Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa kuandaa utaratubu mzuri wa ujio wa Viongozi Wakuu wa Mataifa ya Nje wanaofanya ziara Nchini Tanzania kufika Zanzibar.

Mh. Majaliwa alisema utaratibu huo ambao ulikuwa ukitumika siku za nyuma ni vyema ukawasilishwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili ipate fursa ya kujipanga mapema jinsi inavyoweza kufaidika na ujio wa Viongozi hao wa Kimataifa.

Waziri Mkuu Majaliwa aliwaeleza wajumbe wa Kikao hicho kwamba katika azma ya kuhakikisha Muungano wa Tanzania unaimarika kwa pande zote mbili utaratibu wa Viongozi Wakuu wa Upande wa Tanzania Bara umeshaandaliwa kwa kufanya ziara za kukagua miradi ya maendeleo upande wa Zanzibar.

Alisema wapo baadhi ya Mawaziri wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano tayari wameshafanya ziara kama hizo hasa wale wanaohusika na Wizara za Muungano ambazo zina Taasisi zake upande wa Zanzibar.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitahadharisha kwamba wapo baadhi ya watu wasioutakia mema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao tayari umeshatimiza miaka 53 sasa.

Balozi Seif alisema watu hao hutumia mapungufu na changamoto zilizopo katika baadhi ya kero za Muungano kwa kupotosha kwa makusudi dhamira na malengo la Muungano ambayo ni Umoja na Mshikamano wa Wananchi wa pande zote mbili.

Akikiahirisha Kikao hicho cha cha kamati ya pamoja ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu masuala ya Muungano Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan alisema kitendo cha Serikali zote mbili kuwatumia Wataalamu wao katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto za Muungano kimesaidia kuleta suluhu na ufumbuzi wa mambo mengi.

Hata hivyo Mh. Samia alisema kutokana na mabadiliko ya dunia yanayokwenda kwa kasi katika harakati za Kimaisha katika mfumo wa teknologia ya Kisasa ya Habadi na Mawasiliano changamoto za Muungano zitaendelea kuibuka nyengine mpya.

Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hatua iliyofikia ya kupitisha sheria ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar baada ya Bunge la Muungano kupitisha sheria ya kuiwezesha Zanzibar ijitegemee yenyewe katika masuala hayo.

Mh. Samia alieleza kwamba Wananchi wasingependa kuona suala la mafuta na Gesi asilia linarejea tena kwenye masulala yanayoleta kero ndani ya Muungano wa Tanzania.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
14/1/2017.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni