.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Ijumaa, 24 Machi 2017

MAJALIWA: TANZANIA INAUTASHI WA DHATI KUBORESHA MAZINGIRA YA UWEKEZANI NA BIASHARA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli inautashi wa dhati wa kuboresha mazingira ya uwekezani na biashara nchini kwa kuondoa rushwa na urasimu katika sekta ya umma, hivyo amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Mauritius kuja nchini.

Amesema Tanzania imefanya mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa kubadili mifumo yake ya kisheria, kitaasisi na kifedha ili kuhakikisha wawekezaji wanahudumiwa ipasavyo na kupewa umuhimu wanaostahili kwani ni wadau muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Waziri Mkuu amesema hayo jana (Alhamisi, Machi 23,2017) wakati akifungua kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Mauritius lilifanyika katika Hotel ya Labourdonnaise mjini Port Louis nchini Mauritius. Kongamano hilo liliandaliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Alisema Tanzania ina uchumi imara unaofuata misingi ya soko huria, ambapo mwekezaji ana uhuru wa kufanya biashara bila ya kuingiliwa na Serikali, hivyo sekta binafsi imepewa kipaumbele katika shughuli za kiuchumi na kibiashara nchini.

“Kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli nawakaribisha kwa mikono miwili kuja na kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali zikiwemo za viwanda na utalii na kutembelea vivutio vya utalii na kupata burudani ya aina yake na kwa wafanyabiashara Tanzania ni mahali pazuri kwa kuwekeza,” alisema.

Alisema TIC na Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar kwa pamoja vimeweka taratibu ambazo zinamwezesha mwekezaji kupata mahitaji yake muhimu ya kuwekeza katika kituo kimoja (One stop Centre).

Alibainisha baadhi ya mahitaji hayo kuwa ni huduma za kusajili kampuni, kodi, uhamiaji, leseni za biashara, ardhi pamoja na masuala mbalimbali yanayohusu uwekezaji. Hali ambayo inachangia Tanzania kupata wawekezaji wengi kutoka ndani na nje.

Waziri Mkuu alisema wawekezaji wanaokuja kuwekeza Tanzania wanatoka katika mataifa mbalimbali kama Marekani, Canada, Afrika Kusini, Kenya, Autsralia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na hivi karibuni wanatarajia wawekezaji kutoka nchini Mauritius.

“Ujio wa wawekezaji hawa haukuwa wa bahati bali ni kutokana na mazingira mazuri yaliyowekwa na Serikali pamoja na suala zima la soko kubwa la bidhaa zao na huduma. Soko hili linalozidi watu milioni 300 katika nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika linatoa uhakika wa soko kubwa kwa mwekezaji yeyote anayekuja Tanzania kuwekeza,”.

“Kuwekeza nchini Tanzania kunampa fursa mwekezaji kupata fursa maalumu kupitia Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) na ile ya Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na soko la nchi ambazo hazipakani na bahari. Nchi ambazo Tanzania ina mahusiano nazo mazuri ya kibiashara ni Rwanda, Burundi, Uganda, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Zambia.

Waziri Mkuu aliongeza kuwa katika kuheshimu wawekezaji Tanzania imesaini mikataba mbalimbali inayolenga kuwalinda popote walipo kama Multilateral Investment Guarantee Agency (MIGA) na Africa Trade Insurance Agency.

Alisema Tanzania mbali ya hali ya amani na utulivu wa kisiasa, pia imebarikiwa kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali asilia ambazo zinatoa fursa nzuri kwa mwekezaji. “Hii ni pamoja na ardhi yenye rutuba nzuri kwa kilimo, madini ya kila aina kuanzia dhahabu, almasi, makaa ya mawe, tanzanites, chuma na gesi asilia,”.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na Waziri Mkuu wa Mauritius Mheshimiwa Pravind Kumar Jugnauth, Prime Minister of the Republic of Mauritius; Waziri wa Mambo ya Nje wa Mauritius Bw. Seetanah Lutchmeenaaraidoo, Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohammed, Balozi wa Heshma wa Tanzania nchini Mauriutius Bw. Cliford Tandali.

Wengine ni Mwenyekiti wa ‪Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Godfrey Simbeye,, Executive Director of Tanzania Investiment Centre; ‪Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Bw. Clifford Tandar pamoja na Maofisa wa Serikali ya Tanzania na Mauritus

IMETOLEWA NA: 

OFISI YA WAZIRI MKUU, 
IJUMAA, MACHI 24, 2017.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni