Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Mbunge Mteule wa Bunge la
Afrika Mashariki Mh. Maryam Ussi Yahya aliyeteuliwa tena mara ya Pili
kuendelea na nafasi hiyo walipofiki Ofisi kwake kushukuru baada ya
kumalizika kwa mchakato wa uteuzi huo.
Balozi Seif akimpongeza Mh. Ali
Hasnuu Makame aliyeteuliwa kuiwakilisha Zanzibar katika Bunge la
Jumuiya ya Afrika Mashariki mara baada ya kubadilishana nao mawazo
Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif Ali Iddi kati kati
waliokaa vitini akiwa katika Picha ya pamoja na Kundi la Mchakato wa
kuwapata Wanachama Wawili wa kuiwakilisha Zanzibar katika Bunge la
Afrika Mashariki.Kushoto ya Balozi Seif ni Naibu
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar Dr. Abdulla Juma Abdulla
Mabodi.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha
Mapinduzi Zanzibar Dr. Abdulla Juma Abdulla Mabodi akibadilishana
mawazo na Kundi la Mchakato wa kuwapata Wanachama Wawili wa
kuiwakilisha Zanzibar katika Bunge la Afrika Mashariki.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
itaendelea kulitumia kundi lililoshiriki mchakato wa kuwania nafasi
Mbili za Zanzibar katika Ubunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika ya
Mashariki kutokana na upeo wa maarifa waliyonayo yaliyodhihrisha
kulitumikia Taifa Kizalendo.
Kundi hilo la Wanachama 34 wa Chama
cha Mapinduzi wenye ujuzi, Uzoefu na fani za Kada Tofauti Kitaaluma
limeibua wenzao wawili Bibi Maryam Ussi Yahya na Nd. Hasnuu Ali
Makame waliofanikiwa kuipeperusha Bendera ya Zanzibar katika Bunge la
Afrika Mashariki.
Akizungumza na Wanachama hao katika
kikao cha kuwashukuru baada ya kumaliza salama mchakato wao hapo
Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi alisema Taifa linatambua uwezo na sifa
walizonazo wanachama hao kiasi kwamba Serikali itaendelea kuwatumia
kila wakati.
Balozi Seif alisema upo umuhimu kwa
Wasomi hao wa CCM kuendelea kukitumikia Chama cha Mapinduzi { CCM }
katika mfumo wa Kitaaluma zaidi hasa kutokana na Historia kubwa ya
chama hicho Barani Afrika na Duniani kwa ujumla.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
aliwapongeza wanachama wa chama cha Mapinduzi waliojitokeza kutumia
haki yao ya Kidemokrasia ya kuwania fursa ya kugombea Ubunge wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Balozi Seif alisema kitendo hicho
kimeonyesha wazi jinsi gani Demokrasia inavyozidi kuimarika Nchini
tokea kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya Kisiasa unaotekelezwa na
Mataifa mengi hivi sasa ndani ya Ukanda wa Afrika Mashariki.
Aliwataka wabunge Wastaafu wa Bunge
la Jumuiya ya Afrika Mashariki waendelee kutumia uzoefu wao katika
kipindi chao cha kupumzika ili Taifa lizidi kupiga hatua kubwa ya
Kiuchumi na Maendeleo kupitia ndani ya maarifa na mgongo wao.
“ Taifa linatambua sifa na uzoefu
wao na Daima Serikali zote mbili zitaendelea kuwatumia kila inapobidi
kufanya hichi kwa nia ya kuchota maarifa waliyonayo kutokana na
uzoefu huo”. Alisema Balozi Seif.
Alisema Serikali imefarajika na
kutambua mchango mkubwa uliotekelezwa na Wanachama hao Wastaafu
katika utumishi wao wa Umma wa Afrika Mashariki pamoja na wale
Wanachama waliojitokeza kuwania nafasi hiyo.
Wakitoa shukrani na nasaha zao
baadhi ya Wanachama hao kwa niaba ya wenzao walisema Chama cha
Mapinduzi kimebadilika na kusababisha kupungua kwa mizengwe jambo
ambalo faraja imetanda kuona jinsi gani watu walipewa dhamana ya
kusimamia majukumu yao wanazingatia zaidi sheria, kanuni na taratibu
zilizowekwa.
Walisema jitihada za kubadilisha
muundo katika utekelezaji wa majukumu umezingatia sera na uwajibikaji
mzuri uliotukuka na waliishukuru Kamati ya Sekriterieti ya Chama cha
Mapinduzi kwa uadilifu wake katika kipindi chote cha mchakato wa
kuchuja wagombea hao.
“ Ukarimu uliyoonyeshwa na wajumbe
wa Sekriterieti hiyo katika kutoa ushauri na maelekezo ambao
tuliushuhudia wakati wa zoezi hilo umetupa faraja na kubaini
mabadiliko makubwa yaliyopo hivi sasa ndani ya CCM”. Walinakiliwa
wakisema Wagombea hao.
Hata hivyo Wanachama hao
wamemthibitishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM pamoja na
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar kwamba licha ya kupungua kwa kura
zao katika mchakato huo lakini wameahidi kuwa tayari kukitumikia
chama chao pamoja na Serikali wakati wowote watakapohitajika.
Nao kwa upande wao Wateuliwa Wawili
wa Ubunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashiriki upande wa Zanzibar
Mh. Maryam Ussi Yahya na Mh. Hasnuu Ali Makame wameahidi kuchota
mawazo yote watakayopewa na washirika wenzao pamoja na Wananchi wote
na kuyawasilisha kwenye Vikao vya Bunge hilo.
Walisema Bunge la Jumuiya ya Afrika
Mashariki linazingatia elimu zote licha ya mawazo ya baadhi ya Watu
kufikiria zaidi Fani ya Sheria lakini kinachohitajika zaidi ni Mbunge
husika kujitambua kwa kuelewa Nchi yake inahitaji kitu gani
kuchukuliwa hatua zinazofaa ndani ya Bunge hilo.
Mapema Naibu Katibu Mkuu wa Chama
cha Mapinduzi aliyeambatana na Kundi hilo Dr. Abdulla Juma Abdulla
Mabodi alisema zoezi la mchakato wa uchaguzi huo lilikuwa gumu
kutokana na sifa walizokuwa nazo wagombea wote.
Dr. Mabodi alisema licha ya
kukamilika kwa zoezi hilo alisisitiza umuhimu ushirikiano kati ya
Uongozi wa Ofisi Kuu na Kundi hilo la Wanachama kwa vile pande zote
mbili zimelenga kustawisha maisha na faraja ya Wananchi wa Visiwa vya
Zanzibar.
Alisema Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui
ni jengo tu la chama kama yalivyo majengo mengine ya Chama hicho
katika Mikoa, Majimbo na Matawi. Hivyo Wanachama wote wako huru
kuwasilisha mawazo au mabo waliyonayo yenye mustakabala mzuri wa
kujenga Chama hicho.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar
11/4/2017.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni