WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi Msaidizi wa Pembejeo wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Bw. Shenal Nyoni ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili kwa kuongeza gharama za pembejeo kwa kushirikiana na baadhi ya mawakala wa pembejeo za kilimo.
Amesema Serikali italipa madeni yote ya mawakala wa pembejeo za kilimo mara baada ya kukamilisha uhakiki na kujiridhisha juu ya uhalali wake, sababu bado inawahitaji mawakala ili kushirikiana nao katika kuhudumia wakulima kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Aprili 10, 2017) katika kikao alichokiitisha kwenye Makazi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma kati yake na mawakala wa pembejeo za kilimo pamona na Maofisa kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
“Gharama ya madeni ni kubwa kuliko pembejeo zilizosambazwa. Hii inatokana na udanganyifu mkubwa unaofanywa na mawakala kwa kushirikiana na watendaji wa Serikali wanaohusika na masuala ya pembejeo,”
Amesema kuwa kwenye eneo la pembejeo kuna matatizo makubwa kutokana na baadhi ya Maofisa kuzungumza na mawakala na kuongeza gharama za pembejeo kwa lengo la kuibia Serikali na kisha kugawana fedha. “Sasa Serikali haiwezi kulipa madeni ya kutengenezwa bali tutawalipa stahili zenu baada ya uhakiki kukamilika kama nilivyosema awali,”.
Waziri Mkuu ameongeza mawakala wa pembejeo waliwasilisha Serikali deni la sh. bilioni 65.4 kwa huduma waliyoitoa katika mikoa 25 ambapo Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi imekamilisha uhakiki wa madeni hayo kwa mikoa 10 ya Morogoro, Iringa, Njombe, Ruvuma, Songwe, Rukwa, Katavi, Kigoma, Kilimanjaro na Arusha ambayo madeni yake ni asilimia 70 ya madeni yote.
Amesema ripoti ya uhakiki wa mikoa nane kati ya 10 imetoka (imebaki Katavi na Kigoma) na kubainisha kuwa mikoa hiyo inadai sh. bilioni 36 kati ya hizo sh. bilioni 11 bado zinaendelea kuhakikiwa, sh. bilioni 14 zimekataliwa hivyo siyo madeni halali, sh. bilioni 8.2 ndiyo deni halali na sh. bilioni 2.3 zinachungizwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Waziri Mkuu amesema uhakiki wa madeni kwa mikoa 15 iliyobakia ambayo madeni yake ni asilimia 30 unaendelea ambapo amewasihi mawakala hao kuwa wavumilivu katika kipindi ambacho Serikali inafanya uhakiki kwa kuwa inataka itende haki kwa kila mtu kulipwa deni lake kwa kiwango kinachostahili na watakaobainika kufanya udanganyifu watachukuliwa hatua za kisheria.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, S.L.P 980, DODOMA
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni