Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) ipo kwenye mazungumzo na Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (TADB) yanayolenga kuwanufainisha wakulima visiwani Zanzibar kwa kuwapati mikopo ya gharama nafuu ili kuongeza tija katika kilimo visiwani humo.
Wakizungumza katika mkutano wa pamoja wenye lengo la kujadiliana namna bora za kushirikiana katika kumkomboa mkulima mdogo visiwani humo, watendaji wakuu wa taasisi hizo wamesema kuwa kwa kutambua umuhimu wa sekta ya kilimo na mkazo wa serikali za katika kuwaongezea kipato wananchi wanaojishughulisha katika kilimo; Benki hizo zinapanga kuchagiza hupatikanaji wa fedha za gharama nafuu kwa wakulima hao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa PBZ, Bw. Juma Ameir amesema kuwa Benki yake inatambua umuhimu wa kilimo nchini hivyo ipo tayari kushirikiana na TADB ili kuweza kutimiza malengo la serikali ya kuwakwamua katika umaskini wa kipato wakulima nchini.
Naye, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga amesema ushirikiano na PBZ utachagiza kuhamasisha mabenki na taasisi nyingine za kifedha kutoa fedha kwenye mnyororo mzima wa kilimo ili kusaidia mapinduzi katika ya kilimo kwa wakulima visiwani humo.
Makubaliano hayo yanalenga kuitumia PBZ kama mdau atakayetumika kusimamia fedha zenye masharti nafuu na endelevu kutoka TADB na wadau wengine ili kuinua ushiriki wa wakulima wadogo katika mfumo wa kifedha visiwani humo.
Mkurugenzi Mtendaji wa PBZ, Bw. Juma Ameir (kulia) akizungumza na wageni kutoka TADB (kushoto) wakati walipofika Ofisini kwake kujadiliana masuala mbalimbali yenye lengo la kuwanyanyua wakulima visiwani humo.
Mjumbe wa Bodi ya TADB, Bibi Rehema Twalib (kulia) akizungumza wakati walipotembelea Makao Makuu ya Benki ya Watu wa Zanzibar. Kushoto ni mjumbe mwengine wa Bodi ya TADB, Bw. Hussein Mbululo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Bw. Francis Assenga (kulia) akieleza lengo la ushirikiano wa kati ya Benki ya Kilimo na Benki ya Watu wa Zanzibar kwa Mkurugenzi Mtendaji wa PBZ, Bw. Juma Ameir (hayupo pichani) wakati wa kikao cha pamoja cha Benki hizo
Mkurugenzi Mtendaji wa PBZ, Bw. Juma Ameir akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na wageni kutoka TADB (haupo pichani) wakati walipofika Ofisini kwake kujadiliana masuala mbalimbali yenye lengo la kuwanyanyua wakulima visiwani humo.
Wadau walioshiriki kikao hicho wakifuatilia mijadala yenye lengo la kuboresha makubaliano hayo yatakayomnyanyua mkulima mdogo wa visiwani Zanzibar.
Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa TADB, Bw. Augustino Chacha (kushoto) akizungumzia fursa za mikopo inayotolewa na Benki hiyo wakati walipotembelea Makao Makuu ya Benki ya Watu wa Zanzibar
Mjumbe wa Bodi ya TADB, Bw. Hussein Mbululo akizungumza wakati wa mkutano huo.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni