Wajumbe wa Kikao cha Pamoja kati ya Chama cha Ushirika cha Wauza Madagaa cha Tusiyumbishane kilichopo eneo la Maruhubi mjini Unguja na ugeni wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB). Kikao kilijadilia changamoto zinazozikabili Ushirika huo na namna TADB inavyoweza kuwasaidia katika kuendeleza ushirika huo.
Na mwandishi wetu, Zanzibar
Chama cha Ushirika cha Wauza Madagaa cha Tusiyumbishane kilichopo eneo la Maruhubi mjini Unguja kimeiomba Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuwasaidia katika kuendeleza ushirika wao kwa kuwapatia mikopo na mahitaji mengine ili kuboresha huduma zao.
Akizungumza katika kikao cha pamoja kilichofanyika katika eneo la ushirika huo mjini Unguja, Mwenyekiti wa Tusiyumbishane, Bw. Haji Omar Haji amesema licha ya fursa kubwa iliyopo kwenye eneo la ukaushaji wa madagaa, ushirika wao unakabiliwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu na ufinyu mkubwa wa upatikanaji wa fedha za mtaji kwa ajili ya kuboresha huduma zao.
Bw. Haji ameongeza ukosefu wa mikopo ya uhakika imekuwa ni changamoto kubwa inayochangia kurudisha nyuma ukuaji wa biashara hiyo hivyo kuwa kikwazo katika kupambana na umaskini wa kipato miongoni mwa washirika wa umoja huo hivyo akaiomba benki hiyo kuwawezesha ili kuongeza tija ya shughuli zao.
“Uduni wa mitaji ya uhakika inachangiwa kwa kiasi kikubwa na mabenki na taasisis nyingine za kifedha kushindwa kutuwezesha sie wajasiriamali wa hali ya chini kwa kukosa sifa wazitakazo, hivyo tunaiomba TADB kutuwezesha ili tuongeze tija katika shughuli zetu,” Bw. Haji aliongeza.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga amesema kuwa Benki yake imesikia kilio cha umoja huo, na watatimiza ndoto zao ili kuweza kutimiza ndoto za Serikali za kuanzisha TADB ili kusaidia wakulima na wavuvi wadogo kukabiliana na mapungufu ya upatikanaji wa mikopo katika sekta ya kilimo na uvuvi kuchagiza mapinduzi katika kilimo nchini.
Bw. Assenga ameongeza kuwa sekta ya uvuvi hasa ufugaji wa samaki ni mojawapo ya minyororo ya mwanzo inayopatiwa mikopo kwa ajili ya uongezaji wa thamani mazao na mifugo mbalimbali hasa katika uongezaji wa thamani wa mazao yatokanayo na samaki nchini.
Ameongeza kuwa Benki yake imejipanga kuendeleza uongezaji wa thamani wa eneo la uvuvi na ufugaji wa samaki ili kuongeza tija kwa wakulima na wafugaji wa samaki wadogo nchini.
“Benki inatoa mikopo na kusaidia uwekezaji kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya masoko kwa ajiili ya kuboresha kilimo na uvuvi hasa ufugaji wa samaki nchini,” alisema Bw. Assenga.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni