WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haina mpango wa kuanzisha maeneo mapya ya utawala hadi ikamilishe kuboresha miundombinu kwenye maeneo iliyoyaanzisha.
“Ili kutimiza azma hiyo, Serikali katika mwaka wa fedha 2017/2018 imetenga kiasi cha shilingi bilioni 412.38 kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo, Serikali imetenga shilingi bilioni 16.985 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya majengo ya ofisi na makazi ya viongozi katika mikoa yote mipya,” amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Julai 5, 2017), bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa saba wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Septemba 5, mwaka huu.
“Katika mgawo huo, mkoa wa Njombe umetengewa jumla ya shilingi bilioni 3.34; mkoa wa Katavi umetengewa jumla ya shilingi bilioni 3.080; mkoa wa Simiyu umetengewa jumla ya shilingi bilioni 3.775, mkoa wa Geita umetengewa jumla ya shilingi bilioni 2.978 na mkoa wa Songwe umetengewa jumla shilingi bilioni 3.812,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 61.7 kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri 64 ambapo kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 28.7 ni kwa ajili ya kukamilisha majengo ya ofisi katika Halmashauri 44 na shilingi bilioni 33 ni kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri mpya 20.
Sambamba na hatua hizo, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto imetoa vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa vyenye thamani ya shilingi bilioni 2.9 pamoja na kununua magari ya kubebea wagonjwa katika Halmashauri 67.
Waziri Mkuu amesema miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na Serikali ni pamoja na kuendeleza juhudi za ugatuaji wa madaraka kwenda katika Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na kuongeza mgawo wa fedha za ruzuku ya maendeleo inayopelekwa kwenye vyombo hivyo.
Amesema Serikali inachukua hatua hizo ili kuhakikisha kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini zinatimiza malengo ya kuanzishwa kwake kwa mujibu wa Ibara ya 145 na 146 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
40480 - DODOMA.
JUMATANO, JULAI 5, 2017
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni