Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya
Mikopo ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Abdul-Razaq
Badru akiongea na waandishi wa habari kuhusu upangaji mikopo kwa
mwaka wa masomo 2017/2018 leo (Jumatano, Oktoba 18, 2017) katika
ofisi za HESLB jijini Dar es salaam. Kushoto kwake ni Kaimu
Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo wa HESLB Dkt. Veronica
Nyahende (Picha: HESLB).
Waombaji wa Mwaka wa Kwanza
Tunapenda kuwafahamisha waombaji wa
mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2017/2018 kuwa, baada ya
uchambuzi wa maombi yao, Orodha ya Awamu ya Kwanza yenye wanafunzi
10,196 wa mwaka wa kwanza waliofanikiwa kupangiwa mikopo imekamilika.
Kiasi cha Tshs 34.6 bilioni
kimetengwa kwa ajili ya wanafunzi hao 10,196. Kwa ujumla, Tshs 108.8
bilioni zitatolewa kwa wanafunzi 30,000 wa mwaka wa kwanza kwa mwaka
wa masomo 2017/2018.
Orodha hiyo ya kwanza inapatikana
kwenye tovuti ya Bodi ya Mikopo (www.heslb.go.tz) na itatumwa kwa
vyuo husika. Orodha nyingine (batches) zitafuata kadri taratibu za
udahili na uchambuzi zinavyokamilika. Lengo ni kutoa majina ya wote
waliofanikiwa kupata mkopo kabla ya vyuo kufunguliwa mwishoni mwa
mwezi huu wa Oktoba, 2017.
Orodha hii ya wanafunzi 10,196
imepatikana baada ya kupokea na kuchambua Awamu ya Kwanza ya majina
ya wanafunzi 32,495 waliopata udahili katika chuo kimoja. Itakumbukwa
kuwa moja ya sifa kuu za kupata mkopo ni mwombaji kupata udahili
katika taasisi ya elimu ya juu inayotambuliwa na Serikali.
Wanafunzi waliopata udahili katika
chuo zaidi ya kimoja na ambao wana sifa za kupata mikopo, watapangiwa
mikopo baada ya kuchagua na kuthibitisha chuo watakachojiunga kwa
ajili ya masomo.
Tshs 318 bilioni zatengwa kwa ajili
ya wanaoendelea na masomo
Wakati huohuo, tunapenda
kuwafahamisha wanafunzi wa elimu ya juu wanaoendelea na masomo na
umma kwa ujumla kuwa tunatarajia kuanza kutuma vyuoni fedha za mikopo
ya wanafunzi wanaoendelea na masomo ambao wamefaulu mitihani yao
kuanzia leo, Jumatano, Oktoba 18, 2017.
Kiasi cha Tshs 318.6 bilioni
kitatolewa kwa wanafunzi 93,295 wanaoendelea na masomo kwa mwaka wa
masomo 2017/2018. Tayari Serikali imeshatoa fedha hizo na lengo la
Bodi ni kuhakikisha fedha zinafika vyuoni kabla ya kufunguliwa kwa
vyuo ili kuwaondoloea wanafunzi usumbufu.
Hitimisho
Bodi ya Mikopo inawasihi waombaji wa
mikopo kuwa na subira wakati ikiendelea kukamilisha maandalizi ya
orodha zinazofuata za wanafunzi waliopata mikopo. Tutaendelea kutoa
taarifa kwa vyombo vya habari na tovuti ya Bodi mara kwa mara.
Mwisho.
Imetolewa na:
ABDUL-RAZAQ BADRU
MKURUGENZI MTENDAJI
JUMATANO, OKTOBA 18, 2017
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni