.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatatu, 13 Novemba 2017

UJENZI HOLELA NDIO CHANZO CHA MAFURIKO

Mkurugenzi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Moh’d aliyesimama akitoa Taarifa ya athari za Mvua za Vuli za Mwaka 2017 zinazoendelea kunyesha Zanzibar na hatua zinazopendekezwa kuchukuliwa mbele ya Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar.

Wa kwanza Kulia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikiongoza Kikao hicho Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Wa kwanza kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed, Waziri wa Kilimo Mh. Hamad Rashid Mohamed, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh. Haroun Ali Suleiman na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma.

Kulia ya Mkurugenzi Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa ni Waziri wa Hbari Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Rashid Ali Juma ma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Mh. Haji Omar Kheir.
Balozi Seif akikiongoza Kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar kujadili Taarifa ya athari za Mvua za Vuli za Mwaka 2017 zinazoendelea kunyesha Zanzibar na hatua zinazopendekezwa kuchukuliwa.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Ujenzi holela kwenye njia za asili za maji hasa katika maeneo ya mabondeni, ujenzi wa miundombinu ya Bara bara usiozingatia uwepo wa misingi ya kupitishia maji ya Mvua sambamba na utupaji wa taka taka ovyo ndio sababu kubwa zinazopelekea kutokea kwa athari za mafuriko ya mvua katika sehemu mbali mbali Nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Moh’d alisema hayo wakati akitoa Taarifa ya Athari za Mvua za Vuli za Mwaka 2017 zinazoendelea kunyesha Zanzibar katika Kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.

Nd. Shaaban Seif Moh’d alisema ili kukabiliana na tatizo hilo linalojitokeza kila mwaka ipo haja ya kuyaekea uzio maalum wa kutoruhusu ujenzi katika maeneo hatarishi ili kupunguza uvamizi na ujenzi holela ambao unaonekana ndio chanzo cha athari hizo.

Alisema wakati umefika kwa Taasisi husika kutekeleza ipasavyo Sheria, Kanuni na Mikakati ya matumizi ya ardhi na mipango Miji sambamba na kuharakisha mpango wa kuyapima maeneo yatakayotumika kwa ajili ya ujenzi wa Nyumba za Makaazi.

Alieleza kwamba hatua hiyo mara nyingi huenda sambamba na ongezeko la idadi ya Watu inayoonekana kupanda kwa kasi hasa katika Wilaya za Magharibi ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar alifafanua kwamba Mvua zinazoendelea kunyesha licha ya kusababisha Vifo vya watu, uharibifu na upotevu wa Mali za Jamii lakini pia zilisababisha uharibifu wa Miundombinu ya Barabara Nchini.

Nd. Shaaban alisema Tathmini ya awali iliyofanywa na Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar kwa kushirikiana na Kamati za Maafa za Wilaya imebainisha kwamba jumla ya Nyumba 183 zimeathirika kwa kujaa maji katika Mkoa Mjini Magharibi.

Alisema Mvua hizo zilisababisha kubomoka kwa baadhi ya kuta za nyumba na Makaro ya Maji Machafu hali ambayo inaweza kusababisha kutokea kwa Majanga mengine yakiwemo magonjwa ya miripuko.

Mkurugenzi Shaaban alisema kwa mujibu wa Taarifa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Kanda ya Zanzibar, kiwango cha Mvua kiliripotiwa kutokea Tarehe 26 Oktoba Mwaka 2017 kimefikia Milimita Mia 288.5 kwa muda wa saa Ishirini na Nne.

Alisema Kiwango hicho ni kikubwa zaidi na hakijawahi kuripotiwa katika Mkoa wa Mjini Magharibi tokea Mwaka 1998 ambapo Mvua ya Milimita Mia 197.6 kwa siku iliripotiwa.

Hata hivyo alifafanua kwamba kwa upande wa Kisiwa cha Pemba Mvua za msimu huu wa Vuli zinaendelea kunyesha vyema katika kiwango cha kawaida bila ya kuleta athari yoyote.

Wakichangia Taarifa hiyo ya athari za Mvua za Vuli za Mwaka 2017 zinazoendelea kunyesha Baadhi ya Wajumbe wa Kamati hiyo walisema athari za mafuriko ya Mvua zitaendelea kuripotiwa kila msimu iwapo hatua za kudhibiti maeneo hatarishi hazitachukuliwa ipasavyo.

Walisema mashamba mengi ya Kilimo yamevamiwa kwa shughuli za Ujenzi wa Nyumba za Makaazi kiasi kwamba wahusika wa utoaji wa vibali bila ya kuzingatia Sheria wanastahiki kuwajibishwa sambamba na Baadhi ya Madiwani waliohusika na uzembe huo kuripotiwa Chamani kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Hata hivyo Wajumbe hao walieleza kwamba ipo hatua ya maendeleo iliyofikiwa katika kufuata Sheria na Taratibu za Ujenzi kwa baadhi ya Watu waliopitia Taasisi inayosimamia Ardhi kwa kuyatumia vyema maeneo ya ujenzi wa Nyumba za kuishi na matokeo yake kupunguza usumbufu pamoja na msongamano.

Akiahirisha Kikao hicho Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema elimu kwa Umma lazima iendelee kutolewa ili kusaidia kupunguza maafa yanayoweza kuepukwa.

Balozi Seif alisisitiza umuhimu wa Wafadhili wanaojitolea kusaidia Maendeleo ya Jamii katika maeneo tofauti wanawajibika kufikiria kuzingatia Sheria, Sera na Taratibu za Nchi ili kupunguza migongano na hitilafu ndogo ndogo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
13/11/2017.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni