.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumanne, 21 Novemba 2017

WAMBURA AWATIA SHIME WAKUFUNZI WA WAAMUZI

Makamu Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Michael Wambura amesema, kuna uwezekano mkubwa Bara la Afrika, likatoa idadi kubwa ya waamuzi katika fainali za michuano mikubwa hususani Kombe la Dunia.

Wambura alisema hayo Jumatatu Novemba 20, 2017 kwenye Ukumbi wa ILO, Dar es Salaam wakati aifungua kozi Wakufunzi wa Waamuzi kutoka sehemu mbalimbali barani Afrika.

Kozi ya wiki moja ya Wakufunzi wa waamuzi hatua ya tatu ‘Futuro III’ inayofanyika Tanzania kwa nchi 26 kushiriki. Jumla ya Washiriki 58 wanashiriki kozi hiyo kutoka nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania.

Kozi hiyo ina wakufunzi sita wakiwamo Carlos Henriques na Dominic Chiellens wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), ambao Wambura aliwataka wakufunzi wanaofundishwa mbinu mbalimbali kufanya kazi kwa weledi ili kutimiza ndoto hiyo ya Afrika.

“Waamuzi wa Afrika wana uwezo. Ninyi wakufunzi ni wa kufanya waamuzi wetu kuwa na uwezo zaidi. Ni Aibu kwa Bara kubwa kama Afrika lenye nchi wanachama 54 wa FIFA kuwa na waamuzi wachache katika fainali za Kombe la Dunia.
“Tuazimie kuwa na waamuzi wa kutosha katika fainali kubwa kama hizo,” Amesema Wambura ambaye alipigiwa makofu na washiriki kwa kuwatia shime wakufunzi.

GRASSROOTS YAFANYIKA KWA MAFANIKIO LINDI

Kozi ya makocha wa mpango wa Grass Roots unaolenga wachezaji mpira wa miguu (wasichana na wavulana) wenye umri kati ya miaka 6-12, imefanyika kwa mafanikio mkoani Lindi.

Kozi hiyo ilifungwa rasmi Jumapili Novemba 19, 2017 na Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi.

Akifunga kozi hiyo iliyoshirikisha walimu 30 wa shule za msingi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Lindi kwenye Uwanja wa Ilulu Lindi, Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga amewakumbusha kuwa elimu waliyoipata waitumie kama chachu ya kukuza soka la Tanzania,

"Mkoa wa Lindi umepata bahati kubwa sana kupata elimu hii kwani awali tulijua ni kwa ajili ya Mkoa wa Dar ila kumbe hata sisi huku Lindi Vijijini tunatambuliwa na TFF, Nitatoa ushirikiano kwa waalimu wote 30 waliopata mafunzo ili tuweze kukuza soka letu hasa Wilaya yetu ya Lindi,” amesema.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi amewapongeza washiriki wote waliopata kozi hiyo huku akiwahasa kutumia elimu waliyoipata kufundishia michezo mashuleni.

"Waalimu sina shaka na nyie, nyie ni bado vijana natambua elimu mliyoipata itaufanya mkoa wa lindi kupata vijana wengi wakiume na wakike ambao watapata elimu ya soka kutoka kwenu, ikumbukwe dhumuni la TFF ni kutoa elimu kwenu ili nyie mkaitumie kwa vijana mashuleni,” amesema.

Madadi amewataka washiriki kuitumia vizuri nafasi hiyo waliyoipata kwa kwenda kuwafundisha na kuupenda mpira wa miguu watoto wadogo wenye umri kati ya miaka 6-12.
Ikumbukwe kozi hii ya Grass Roots kwa mwaka huu imefanyika mara mbili ambapo mwezi Septemba na Oktoba zilifanyika Dar kwenye Ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania kwa kushirikisha waalimu wa shule za msingi na Sekondari kutoka mkoa wa Dar es Saalam.

SIRI YA NINJE KILIMANJARO STARS

Kocha Mkuu wa timu ya mpira wa miguu ya Tanzania Bara, ‘Kilimanjaro Stars’, Ammy Conrad Ninje, amesema kwamba ameteua kikosi hicho kwa kuzingatia mambo makuu matatu.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Ninje alitaja kikosi cha wachezaji 20 kitakachoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji mwaka huu wa 2017 ambako amesema: “Kwanza nataka mchezaji ambaye ana njaa ya mafanikio…

“…Sehemu pekee ya kupata mafanikio ni pamoja na kucheza timu ya taifa. Pili, nataka wchezaji wanaofundishika na tatu nataka wachezaji wanaokubali kufundishika,” amesema Ninje.

Ninje - Kocha wa Daraja ‘A’ la Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA), alitaja kikosi hicho Jumamosi Novemba 18, 2017 kwenye Ukumbi wa Hosteli za TFF, Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.
Kikosi hicho kinachotarajiwa kuingia kambini Jumapili Novemba 26, mwaka huu jijini Dar es Salaam kina makipa Aishi Manula (Simba SC) na Peter Manyika (Singida United).

Walinzi ni Gadiel Michael (Young Africans), Boniphace Maganga (Mbao FC), Kelvin Yondani (Young Africans), Kennedy Juma (Singida United), Erasto Nyoni (Simba SC) na Mohammed Hussein (Simba SC).

Viungo wa kati ni Himid Mao ambaye ni Nahodha (Azam FC), Jonas Mkude (Simba SC), Hamis Abdallah (Sony Sugar/Kenya), Mzamiru Yassin (Simba SC), Raphael Daud (Young Africans), Shizza Kichuya (Simba SC), Abdul Hilal (Tusker/Kenya) na Ibrahim Ajib (Young Africans).

Washambuliaji ni Mbaraka Yussuph (Azam FC), Elias Maguri (Dhofar/Mascat, Oman), Daniel Lyanga (Fanja FC/Mascat) na Yohana Mkomola (Ngorongoro Heroes).

Benchi la Ufundi linaundwa na yeye Ninje ambaye ni Kocha Mkuu, Fulgence Novatus (Kocha Msaidizi), Patrick Mwangata (Kocha wa Makipa), Danny Msangi (Meneja), Dkt. Richard Yomba (Daktari wa timu), Dkt. Gilbert Kigadye (Daktari wa Viungo) na Ally Ruvu (Mtunza Vifaa).

Katika michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Desemba 3, mwaka huu, Kilimanjaro Stars imepangwa Kundi ‘A’ pamoja wenyeji Kenya, Rwanda na Libya ambayo ni timu mwalikwa kutoka Kaskazini mwa Afrika.

Kilimanjaro Stars ambayo imewahi kutwaa mara tatu taji hilo la Chalenji tangu kuanzishwa kwake, itaaza kampeni za kurudisha heshima yake dhidi ya Libya katika kundi hilo la A utaofanyika Desemba 3, mwaka huu.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni