.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumatatu, 4 Desemba 2017

DR. SHEIN AFUNGUA MKUTANO WA 47 WA KIMATAIFA WA KUWAANDAA WATAFITI CHIPUKIZI WA BARA LA AFRIKA

Rais wa Zanzibar Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Muhamed Shein alisema Kiwango duni cha uwajibikaji katika misingi ya kuendesha Utawala Bora Kisiasa na Kiuchumi miongoni mwa Nchi za Bara la Afrika kimekuwa kikichangia na kusababisha migogoro isiyokwisha ambayo huwaathiri Wananchi walio wengi ndani ya eneo kubwa la Bara hilo. 

Alisema hicho ni moja ya kitu hatari kinachosababisha kuporomoka kwa Uchumi, Maendeleo na Ustawi wa Jamii Barani Afrika changamoto inayopaswa kutoa fursa kwa Waafrika wenyewe kutafakati kwa kina njia gani yenye muelekeo wa mafanikio katika masuala ya kufanikisha Maendeleo na Utawala Bora.

Dr. Ali Muhamed Shein alisema hayo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif wakati alipokuwa akiufungua Mkutano wa 47 wa Kimataifa wa kuwaandaa Watafiti Chipukizi wa Bara la Afrika katika dhana nzima ya kusaidia mataifa yao Kitaaluma uliofanyika katika Hoteli ya Kimataifa ya Maunt Meru Mkoani

Arusha. Mkutano huo unaofanyika kila baada ya Miaka Miwili katika Mataifa Wanachama huandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Uchumi Afrika { AERC } kwa lengo la kuwandaa Vijana waenye vipaji katika masuala ya Tafiti mbali mbali zikiwemo Uchumi, Kilimo, Uhandisi na Afya.

Rais wa Zanzibar alisema Mataifa mengi Barani Afrika yamekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya Watu hasa Vijana kasi ambayo inahitaji nguvu kubwa zitakazozaa maarifa za Kiutafiti katika masuala ya Uchumi ili itoe afueni ya Maendeleo ya muelekeo wa matumaini.

Alisema uwajibikaji wa pamoja katika umuhimu wa kuandaa nguvu za kiutendaji kwa kuwashirikisha Wananchi na hasa Vijana wenye Vipaji vya Utafiti wa kawaida ndani ya Taasisi za Kitaaluma unaweza kuzinyanyua Kiuchumi Nchi za Afrika katika kipindi kifupi.

Dr. Shein alisema Warsha na Mikutano hiyo ya kuwakusanya Vijana Watafiti Chipukizi inasaidia kuamsha hamasa ya mijadala ya Maendeleo, namna ya uendeshaji wa Utawala pamoja na Mahusiano yenye muelekeo wa kujenga mazingira bora ya uwajibikaji.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alisema katika mfumo wa kulikwamua Bara la Afrika Kiuchumi ameiagiza Taasisi ya Utafiti wa Uchumi Afrika { AERC } Kutafuta mbinu na maarifa zaidi ya kuona Mikutano, Mijadala na hata Warsha za kuwakutanisha Watafiti wa Uchumi wa Bara hili inafanyika mara mbili kwa Mwaka.

Alisema mpango huo unaweza kuhamasisha chachu ya Utafiti kwa Wanataaluma hao wa mambo ya Uchumi jambo ambalo linaweza kufungua njia ya haraka za kupunguza au kuondosha kabisha Changamoto zinazolikabili Bara la Afrika hasa katika masuala ya Ajira.

Dr. Shein alisema hatma njema ya mafanikio ya Maendeleo ya Kiuchumi kwa Wananchi waliomo ndani ya Mataifa ya Bara la Afrika inaweza kuchomoza hatua kwa hatua iwapo Wanataaluma hao 100 wa Utafiti wa Uchumi kutoka zaidi ya Nchi 25 za Afrika wataamaua kutumia vyema Kizalendo ujuzi wao.

Rais wa Zanzibar aliupongeza na kuushukuru Uongozi mzima wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi Afrika { AERC } kwa uamuzi wake wa kuwakusanya Wataalamu Watafiti wa Masuala ya Kiuchumi Barani Afrika kwa nia ya kusaidia Uchumi wa Bara la Afrika na Watu wake.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi Afrika {AERC } Prosefa Lemma Denbet alisema Watafiti wa Taasisi hiyo wamekuwa wakifanya utafiti kwa kushirikiana na Taasisi nyengine ya Kimataifa takriban kwa Miaka 30 sasa.

Profes lemma alisema ushirikiano huo kwa kiasi kikubwa umesaidia kuibua Watafiti Chipukizi Barani Afrika ambao kwa sasa wamekuwa cheche wa muelekeo wa Matumaini kwa Mataifa wanayotoka.

Alisema katika dhana nzima ya nguvu za uwajibikaji katika sekta ya Utafiti AERC imeweka utartibu maalum wa kuwatumia Wataalamu mbali mbali waqzoefu waliobobea katika fani hiyo ili kusaidi maarifa yanayoweza kuongeza nguvu na kasi ya uvumbuzi hasa katika masuala ya Kiuchumi.

Akimkaribisha Mgeni rasmi kuufungua Mkutano huo wa 47 wa Kimataifa wa kuwaandaa Watafiti Chipukizi wa Bara la Afrika Gavana Mkuu wa Benki ya Tanzania { BOT } Profesa BennoNdulu alisema kinachohitajika kwa Watu wa Afrika wakati huu ni kuangalia muelekeo wa namna gani Mataifa ya Bara la Afrika yanavyojikita katika uimarishaji wa uchumi kwa kuzingatia Utawala Bora.

Profesa Benno alisema kutokana na mabadiliko ya Dunia yanayokwenda kwa kasi kupitia mfumo wa kisasa wa Teknolojia ya Mawasiliano, Jamii za Waafrika wanalazimika kubadilika kwa haraka ili waende na wakati huo.

Alitahadharisha kwamba changamoto za Rushwa, migomo ya mara kwa mara , uhabawa vyombo vya usafiri zinazooneka kuzielemea Bara la Afrika iwapo hazikutizamwa na kuchukuliwa hatua zinazofaa zinaweza kuviza maendeleo ndani ya Nchi za Bara la Afrika.

Utafiti wa Uchumi Afrika {AERC } iliyoasisiwa Mwaka 1988 ina Wanachama kutoka Mataifa ya Ghana, Kenya, Malawi, Msumbiji, Nigeria,Rwanda, Afrika Kusini, Uganda, Zambia na Tanzania.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiingia ndani ya Ukumbi wa Hoteli ya Mount Meru Arusha kwa ajili ya kuufungua Mkutano wa 47 wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi Afrika { AERC } kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Braza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi Afrika { AERC } Profesa Lemma Senbet akitoa Taarifa ya Taasisi yake kwenye Mkutano wa Watafiti Chipukizi wa Afrika hapo Mount Meru Arusha.
Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa 47 wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi Afrika { AERC } wakifuatilia matukio mbali mbali yaliyokuwa yakitendeka ndani ya Ukumbi wa Hoteli ya Mount Meru kwenye Mkutano wa Watafiti Chipukizi wa Afrika ulioandaliwa na Taasisi ya AERC.
Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa 47 wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi Afrika { AERC } wakifuatilia matukio mbali mbali yaliyokuwa yakitendeka ndani ya Ukumbi wa Hoteli ya Mount Meru kwenye Mkutano wa Watafiti Chipukizi wa Afrika ulioandaliwa na Taasisi ya AERC.
Mwenyekiti wa Mkutano wa 47 wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi Afrika { AERC } Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania {BOT} Profeza Benno Ndulu akiuendesha Mkutano wa 47 wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi Afrika { AERC }.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiufunguza Mkutano wa 47 wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi Afrika { AERC } kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Braza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein unaofanyika katika Hoteli ya Kimataifa ya Mount Meru Mkoani Arusha.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni