.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Ijumaa, 1 Desemba 2017

RATIBA LIGI YA VODACOM, KOMBE LA AZAM

Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa sasa imesimama kwa takribani majuma mawili.

Sababu kubwa ya kusimama kwa ligi hiyo ni kupisha Kombe la Chalenji la CECAFA - michuano inayoratibiwa na Baraza la Soka kwa nchi za Afrika Mashariki (CECAFA).

Michuano ya CECAFA itafikia ukomo Desemba 17, mwaka huu na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetoa ratiba mara baada ya michuano hiyo.

Desemba 22, 23, 24 na 26, zitakuwa siku za mechi za kuwania Kombe la Shirikisho la Azam yaani Azam Sports Federation Cup (ASFC).

Mechi zitakazochezwa katika siku hizo zitafahamika Desemba 5, mwaka huu ambako imepangwa droo ya timu 64 zitakazocheza Raundi ya Tatu ya ASFC.

Timu 64 maana yake ni kuwa timu 16 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara; timu 24 za Ligi Daraja la Kwanza na timu 24 ambazo zimefuzu kutoka hatua awali; ya kwanza na pili.

Baada ya michezo hiyo, ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom itaendelea tena kwa michezo ya raundi ya 12 itakayofanyika Desemba 29, 30 na 31 kabla ya ligi tena kusimama kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi.

WATANZANIA HAWA KAZINI CECAFA

Baraza la Mpira wa Miguu la nchi za Afrika Mashariki, limeteua Watanzania wanne (4), kuendesha michuano ya kuwania Kombe la Chalenji inayoandaliwa na CECAFA.

Watanzania hao ni Alhaji Ahmed Mgoyi aliyeteuliwa katika Idara ya Mashindano huko CECAFA wakati mwingine ni Sunday Kayuni ambaye ameteuliwa katika Idara ya Ufundi.

Mgoyi ameteuliwa kutokana na uzoefu na uwezo wa wake wa kusimamia mashindano ya kimataifa huku akiwa na rekodi ya kusimamia vema mashindano hayo yalipofanyika kwa mara ya mwisho nchini Tanzania mwaka 2015 wakati Kayuni ni Mkufunzi anayetambuliwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Wengine ambao wameteuliwa kuendesha michuano hiyo ni Waamuzi wawili.

Waamuzi hao ni Elly Sasii (mwamuzi wa kati) na Soud Lilla (Mwamuzi Msaidizi). Tayari wateuliwa wote wako Kenya kwa ajili ya michuano hiyo.

MWAMUZI MTANZANIA KUCHEZESHA KOMBE LA DUNIA 2018
Mtanzania Jonesia Rukyaa Kabakama ameteuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), kuchezesha fainali zijazo za Kombe la Dunia kwa wanawake (Algarve Cup) zitakazofanyika nchini Ureno, mwezi Februari, mwakani.

Jonesia ambaye ni mwanamke ameteuliwa kupuliza filimbi katika fainali hizo ambazo hukutanisha timu mahiri zilizofanya vema katika michuano ya kila Bara.

Lakini kabla ya kwenda Ureno, Jonesia anatarajiwa kushiriki semina maalumu iliyoandaliwa na FIFA. Semina hiyo itafanyika Doha, Qatar kuanzia Februari 12- 16, mwakani.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania linampongeza Mwamuzi Jonesia kwa kuteuliwa na FIFA kuchezesha fainali za Kombe la Dunia na kuhudhuria semina hiyo muhimu kwa maendeleo ya mpira wa miguu.

Waamuzi wengine walioteliwa kutoka Afrika Lidya Abebe wa Ethiopia, Glady Lengwe wa Zambia na Salima Mukansanga wa Rwanda.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni