.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Jumapili, 31 Desemba 2017

WAPINZANI WENGINE 19 WAREJEA CCM RUANGWA

WANACHAMA 19 kutoka vyama vya upinzani katika kata za Matambarare na Mnacho wilayani Ruangwa mkoani Lindi, wamekabidhi kadi zao na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM). 

Wanachama hao kutoka vyama vya CUF na CHADEMA, walikabidhi kadi zao kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana jioni (Jumamosi, Desemba 30, 2017) wakati alipokuwa akizungumza na wakazi wa kijiji cha Matambarare Kusini kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo.

Waziri Mkuu yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka, na ameamua kukagua miradi ya maji, ujenzi wa zahanati na kuzungumza na wananchi katika wilaya hiyo.

Akiwa katika kijiji cha Matambare Kusini, Waziri Mkuu alipokea wanachama 17 ambao kati yao 13 wanatoka Chama cha Wananchi (CUF) na wanne wanatoka Chama cha Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA).

Akiwa katika kijiji cha Ng’au kata ya Mnacho, wilayani humo, Waziri Mkuu alipokea wanachama wawili, Bw. Swibert Mwambe kutoka CUF na Bw. Paskali Rogert wa CHADEMA.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake 17, Mzee Said Bakari Makungwa (maarufu kama Ustaadh Makungwa) alisema alikuwa muasisi wa chama cha TANU pamoja na CCM mwaka 1977 kilipozaliwa, na alishika nyadhifa mbalimbali hadi alipoamua kuondoka.

“Jamani nimerudi nyumbani, na mtu akirudi nyumbani huwa haadhibiwi,” alisema Ustaadh Makungwa mwenye umri wa miaka 80 na kuamsha kicheko kwenye mkutano huo.

Alisema yeye anataka kuwakumbusha wananchi waliohudhuria mkutano mambo manne aliyoyasisitiza Baba wa Taifa, hayati Mwl. Julius K. Nyerere ambayo ni watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.

Kuhusu ardhi, alisema wanaRuangwa wamepewa ardhi na Mwenyezi Mungu ili iwape mazao na madini. “Watu ni sisi ambao tunapaswa tutumie vema rasilmali tuliyopewa katika ardhi,” alisema.

Kuhusu siasa safi, Ustaadh Makungwa alisema: “Kuna siasa safi gani zaidi ya hii tuliyonayo sasa? Utaitafuta wapi zaidi ya kwa Mheshimiwa Magufuli? Safari hii, kafikisha bei ya korosho hadi sh. 4,045 kwa kilo moja. Nani kama Magufuli?” alihoji Mzee Makungwa.

Kuhusu uongozi bora, Mzee Makungwa alisema Mheshimiwa Magufuli ameonyesha njia akisaidiwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. “Kazi ya viongozi ni kuonyesha njia. Sasa wewe kugeuka kushoto au kulia unatafuta nini?” alihoji.

“Hebu niambieni Ruangwa ya juzi na ya leo ziko sawa?,” alijohi na kujibiwa kwamba haziko sawa. “Mimi nimerudi nyumbani, ninaomba msamaha pale nilipowaudhi. Kwa sababu ya umri wangu, ninaijua vema historia ya CCM, njooni kwangu mchukue historia ya chama,” alisema huku akishangiliwa.

Waziri Mkuu anaendelea na ziara ya jimboni kwake kwa kuzindua kampeni ya kitaifa ya upandaji miche bora na mipya.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, DESEMBA 31, 2017.

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni