.

.

.

.

.

.

.

.
KARIBUNI TUHABARIKE, TUELIMISHANE, TUPEANE HABARI ZA KUKUFANYA UTABASAMU KIDOGO NA MATUKIO YALIYOFANYIWA UCHUNGUZI WA KINA TOKA KILA PEMBE CONTACTS: +255 787 377 722 Email: drweyunga@gmail.com PIA UNAWEZA KUNI FOLLOW KUPITIA INSTAGRAM YANGU @drweyunga | TANGAZA NASI ILI UWAFIKIE WATU WENGI ZAIDI.

Alhamisi, 7 Desemba 2017

WAZIRI MKUU AFUNGUA JENGO LA UMOJA WA MATAIFA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua ofisi ya Umoja wa Mataifa na kusema uamuzi huo ni hatua muhimu ya kuendeleza mchakato wa Serikali wa kuhamia Dodoma.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Alhamsi, Desemba 7, 2017) wakati akizungumza na viongozi na watumishi wa taasisi za Umoja wa Mataifa waliohudhuria hafla ya ufunguzi rasmi wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa Dodoma, katika eneo la Mlimwa, Manispaa ya Dodoma.

“Wote mtakubaliana nami kwamba uzinduzi wa ofisi hii ya Umoja wa Mataifa ni hatua muhimu sana ya kuendeleza mchakato wa Serikali wa kuhamia Dodoma. Pia, inafungua mlango mpya utakaowezesha ofisi zote za kibalozi na mashirika ya kimataifa kujenga ofisi zao hapa Dodoma na kuhamia mapema,” alisema.
Alisema anatambua kwamba kwamba wapo viongozi na watendaji wenye hofu ya kuhamia na kuanza maisha mapya Dodoma. “Baadhi ya watendaji wanaogopa changamoto za kuhamisha watoto wao na wenza wao ili kuanza maisha mapya. Napenda kuwatoa hofu kwamba Dodoma ni mahali pazuri pa kuishi na kuna fursa nyingi,” alisema.

Alisema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu iliyopo ya huduma za jamii na miundombinu ya barabara, maji, umeme na mawasiliano ili iwe bora zaidi. Alitumia fursa hiyo kuwasihi waombe maeneo ya ujenzi kwa ajili ya ofisi na makazi.

Aliushukuru Umoja wa Mataifa kwa kuiteua Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazotekeleza mfumo mpya wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa kuungana na kutekeleza shughuli zake kwa pamoja kama familia moja ya Umoja wa Mataifa yaani “UN Delivering as One”.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga alisema Umoja wa Mataifa unayo mashirika 50 na kwamba mashirika 23 kati ya hayo, yanafanya kazi zake hapa nchini.

Alisema wizara yake kwa kushirikiana na Manispaa ya Dodoma, watahakikisha kuwa mashirika hayo yanapatiwa viwanja vya kutosha ili kujenga ofisi zao mapema iwezekanavyo.

Mapema, Mwakilishi Mkazi wa UNDP na Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania; Bw. Alvaro Rodriguez alisema wamefurahi kupata fursa ya kuwa taasisi ya kwanza ya kimataifa kuwa na Ofisi yake kwenye makao makuu ya nchi hapa Dodoma
“Tumefurahi kujumuika kwa pamoja hapa Dodoma, lakini tunaahidi kuwa na sisi tutahamia kwa awamu kama ambavyo Serikali imekuwa ikifanya. Hili litategemea upatikanaji wa viwanja na majengo kwa ajili ya ofisi, kwa hiyo wafanyakazi wetu nao watahamia taratibu,” alisema.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
ALHAMISI, DESEMBA 7, 2017

Hakuna maoni :

Chapisha Maoni