MAMLAKA ya Hifadhi ya Ngorongo (NCAA) imedhamini mashindano ya Ngorongoro Marathon kama sehemu ya njia ya kukuza utalii kwenye eneo hilo lenye vivutio vya pekee duniani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo (Aprili 11) jijini Tanga, Naibu Mhifadhi wa NCAA Asangye Bangu, alisema mashindano hayo yatakuwa na faida kubwa kwenye nyanja za utalii na kuwezesha watu wengi ndani na nje ya nchi kuvutiwa na hifadhi hiyo.
"Tumeamua kudhamini mashindano haya ya Ngorongoro Marathon yanayofanyika Aprili 21, mwaka huu. Nia ya kudhamini mashindano haya, kwanza ni kufanikisha mashindano yenyewe na pili ni kuweza kutangaza utalii wetu.
"Tunaamini sisi Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro tuna dhima kubwa kuona watalii wa ndani na nje wanaongezeka. Lakini ili waongezeke ni lazima tutumie njia mbalimbali za kutangaza vivutio vya Hifadhi za Ngorongoro ambavyo ni vya kipekee duniani" alisema Bangu.
Bangu alisema Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, pia imekuwa na changamoto ya ujangili na uvamizi, hivyo kwa kutumia mashindano hayo, watawaeleza wananchi wajue umuhimu wa hifadhi hizo kwa maslahi ya nchi.
"Suala la kushirikisha jamii katika matukuo mbalimbali ni muhimu sana, ili wananchi waweze kujua Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inafanya kitu gani.
Lakini pia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, imekuwa ikikabiliwa na masuala ya ujangili na uvamizi, hivyo tukikutana na wananchi tunawapa elimu ya kutosha juu ya hifadhi yetu" alisema Bangu.
Kaimu Meneja Mahusiano wa Hifadhi ya Ngorongoro Joyce Mgaya amewahamasisha wanawake na wasichana kushiriki mbio hizo, kwani ni fursa kwa wao, kwanza kuwa sehemu ya kushiriki mashindano ambapo watapata uzoefu mbalimbali, lakini pia wataweza kuijua Hifadhi ya Ngorongoro na shughuli zao, kama sio na wao kuweza kufanya utalii wa ndani.
"Tunataka kutumia mashindano haya kuwaeleza kuwa Watanzania, kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, tuna rasilimali nyingi ikiwemo miti na wanyama, bila jitihada za pamoja tunaweza kujikuta rasilimali hizo zinatoweka, hivyo ni muhimu kwetu kuweza kutunza hifadhi hiyo, kwa kutumia mashindano haya tunaamini ni sehemu ya mafanikio ya kulinda rasilimali hizo" alisema Mgaya.
Naye Meneja Huduma za Utalii Paul Fisso, alisema mashindano hayo yatahusisha kilomita 21, kilomita tano na kwa watoto kilomita mbili na nusu, ambapo itakuwa kwa pande zote wanawake na wanaume na washindi wote watapata zawadi.
Mashindano ya Ngorongoro Marathon 2017, ambayo kwa mara ya kwanza yalidhaminiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA). Mamlaka hiyo inadhamini kwa mara ya pili mwaka huu.
Mashindano ya Ngorongoro Marathon 2017, ambayo kwa mara ya kwanza yalidhaminiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA). Mamlaka hiyo inadhamini kwa mara ya pili mwaka huu.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni