Rais wa Malawi, Joyce Banda amelivunja baraza lake la mawaziri kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya ufisadi serikalini.
Taarifa toka Malawi zinasema maafisa wa serikali wamekuwa wakikutwa na pesa zikiwa zimefichwa chini ya vitanda vyao na kwenye magari yao.
Mwezi uliopita afisa mmoja mkuu katika wizara ya fedha Paul Mphwiyo, aliyeonekana kuwa afisa mmoja mkuu wa serikali ambaye anaonekana wazi hadharani kupinga sana ufisadi, alipigwa risasi na kujeruhiwa.
Wahisani wa kimataifa wamekuwa wakimtaka rais Banda kuchukua hatua kukabiliana na ufisadi.
Malawi ni taifa masikini na hutegemea sana msaada kutoka kwa Muungano wa Ulaya na nchi nyingine za Magharibi.
Rais Banda amesema kuwa mawaziri wapya watateuliwa hivi karibuni bila ya kutoa maelezo zaidi.
Aliitisha mkutano wa dharura wa baraza la mawaziri kabla kutangaza kulivunja.
Kwenye mkutano na waandishi wa habari, Rais Banda alisema kuwa ameunda jopo maalum likijumuisha polisi na maafisa wa serikali kufanya ukaguzi wa matumizi ya pesa za serikali katika idara zote za serikali.
Hakuna maoni :
Chapisha Maoni